Makosa ya kibinadamu chanzo cha ajali Mwanza

Mariam John 0432Hrs   Machi 26, 2024 Habari
  • Asilimia kubwa ya ajali hizo husababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwemo kushindwa kufuata kanuni za barabarani.
  • Mafunzo kwa madereva yanaweza kupuguza matukio ya ajali za barabarani.

Mwanza.Wakati Tanzania ikikabiliana na ajali za barabarani Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Dk. Prosper Mgaya anasema asilimia kubwa ya ajali hizo husababishwa na makosa ya kibinadamu ikiwemo kushindwa kufuata kanuni za barabarani.

Dk. Mgaya ameyasema hayo Machi 25, 2024  katika kikao na wadau wa usafirishaji kutoka Mikoa ya Mwanza, Geita na Mara ambapo amesema ili kumaliza tatizo hilo lazima madereva wapate mafunzo ya ziada.

“Kuna mafunzo special (maalum) yanaitwa ‘Defensive driving’ yanayomsaidia dereva yoyote anapoona kwamba kuna viashiria vya ajali vinataka kutokea afanyeje ili kuepusha hiyo ajali,” amesema Dk. Mgaya.

Kauli ya Dk.Mgaya inakuja wakati ambao Tanzania inafanya jitihada kukabiliana na ongezeko la ajali za barabara ni jambo linalosababisha vifo na majeruhi.

Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) inaonesha kuongezeka kwa ajali hizo kwa asilimia 0.1 huku vifo vikifikia asilimia 63.

Ajali hizo ni zile zilizorekodiwa kati ya mwezi Januari hadi Novemba mwaka 2023 na kufanya jumla ya ajali 1,595 ikiwa ni ongezeko la ajali moja tu kulinganisha na ajali 1,594 zilizoripotiwa mwaka 2022.


Soma zaidi: SanLG waonya hatari ya bodaboda feki zinazoingizwa Tanzania


Aidha, Dk. Mgaya amebainisha kuwa zipo sababu nyingine zinazopelekea ajali za barabarani ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara pamoja na usimamizi legevu wa sheria.

Mbali na mafunzo kwa madereva, chuo cha NIT kimefanya mafunzo kwa wadau wengine wa usalama barabarani ikiwemo wasanifu na wasimamizi  wa  barabara, wasimamizi wa sheria za usalama barabarani na vyama vya watumiaji wa usafiri.

“Tunaamini tukifanya kazi kwa pamoja basi ajali za barabarani tutazipunguza,” amesema Dk. Mgaya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Msala amekitaka chuo hicho kujenga chuo kingine mkoa wa Mwanza kitakachosaidia katika masuala ya utoaji elimu ya barabarani kitendo ambacho kitapunguza ajali hizo.

Pia amewataka wadau wa usafirishaji kuwa mabalozi katika utoaji wa elimu kwa wananchi na madereva ambao ndio wamekuwa sababu ya ajali hizo.

Related Post