Maeneo manne ya kipaumbele bajeti ya Serikali 2020-2021
- Maeneo hayo manne ni pamoja na kufungamanisha sekta ya kilimo na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda.
- Serikali imepanga kutumia Sh34.4 trilioni katika bajeti ya mwaka 2020/2021.
- Hata hivyo, Serikali itakuwa na kibarua cha kuwianisha mapato na matumizi na kuimarisha ulipaji wa kodi kwa hiari.
Dar es Salaam. Wakati Serikali ikipanga kutumia Sh34.4 trilioni katika bajeti ya mwaka 2020/2021, imesema bajeti hiyo itajikita katika maeneo manne ya kipaumbele ikiwemo kufungamanisha sekta ya kilimo na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda.
Matumizi hayo ya Serikali yanakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 21.7 ya Pato la Taifa kutoka Sh33.1 trilioni ya mwaka 2019/2020. Matumizi ya kawaida yanakadiriwa kuwa Sh21.6 trilioni sawa na asilimia 13.7 ya Pato la Taifa na matumizi ya maendeleo yanakadiriwa kuwa Sh12.6 trilioni.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametaja maeneo hayo wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa na mwongozo wa maandalizi na mpango wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 wiki iliyopita bungeni jijini Dodoma.
“Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2020/21 yameandaliwa kwa kuzingatia maeneo manne ya kipaumbele yanayojumuisha miradi ya kielelezo iliyobainishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano,” inaeleza sehemu ya hotuba ya Dk Mpango.
Maeneo ya kipaumbele pamoja na baadhi ya miradi itakayopewa kipaumbele kwa mwaka 2020/21 ni kujenga viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini hususan za kilimo na kuimarisha Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ili viweze kuhudumia wananchi wengi na kuchochea mageuzi ya viwanda Tanzania.
“Kuanzisha na kuendeleza maeneo ya viwanda (Industrial parks) na Kanda Maalum za Kiuchumi; kuboresha utendaji kazi na kutumia taasisi za umma za utafiti na huduma za viwanda,” amesema Waziri huyo.
Zinazohusiana:
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019/2020
- Dk Mpango-Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
Eneo la pili litakuwa ni kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu, kwa mujibu wa Dk Mpango Serikali itaimarisha upatikanaji wa elimu na huduma za ustawi wa jamii ikiwemo kuboresha huduma za afya, upatikanaji wa huduma za maji safi na salama vijijini na mijini; kuimarisha usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Pia jitihada zitaelekezwa katika kuimarisha shughuli za utawala bora ikiwemo Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; kuendelea kutekeleza sera ya elimumsingi bila ada, kusomesha wataalam na mafundi wengi wenye fani na ujuzi maalum; na kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu nchini.
Eneo lingine ambalo Serikali italifanyia kazi ni kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya nishati na usafirishaji (reli, madaraja, barabara na bandari), usafiri wa anga na usafiri wa majini (magati, meli na vivuko).
Katika kipindi hicho Serikali itaandaa Mpango wa tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) kwa kuzingatia matokeo ya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake unaisha mwaka 2020/2021.
Maeneo hayo ya vipaumbele hayatofautiana na yale ya mwaka 2019/2020 ambapo Serikali iliweka nguvu katika kuboresha miundmbinu na ujenzi wa uchumi wa viwanda ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.
Hata hivyo, Serikali itakuwa na kibarua kigumu kutekeleza malengo yake ikizingatiwa kuwa inatakiwa kuendelea kuwianisha mapato na matumizi na kuimarisha ulipaji wa kodi wa hiari kwa kutekeleza Mpango wa Kusimamia Vihatarishi vya Mwitikio wa Ulipaji Kodi.
Pia kutekeleza Mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji; kukuza soko la fedha la ndani; kuendeleza majadiliano na washirika wa maendeleo na taasisi za fedha za nje na kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ili kupata taarifa za uwekezaji wa sekta hiyo katika uchumi.