Serikali kulenga shabaha tano za uchumi mwaka 2019-2020
- Shabaha hizo ni pamoja na kuongeza mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya Pato la Taifa (GDP).
- Miradi itakayochagiza shabaha hizo ni reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme mto Rufiji, ujenzi wa barabara na usambazaji wa umeme vijijini.
- Itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na vihatarishi vya utekelezaji wa mpango 2019/20 ikiwemo upungufu wa rasilimali fedha na mtikisiko wa kiuchumi wa kimataifa.
Dar es Salaam. Katika kuhakikisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2019/20 unatekelezeka, Serikali imesema inakusudia kufikia shabaha kuu tano za uchumi ikiwemo kuongeza mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya Pato la Taifa.
Shabaha hizo zitachagizwa na miradi ya kipaumbele ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme mto Rufiji, ujenzi wa barabara na usambazaji wa umeme vijijini.
Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango ameliambia Bunge leo wakati akiwasilisha hotuba ya Hali ya Uchumi mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2019/20 kuwa shabaha hizo ni kukua kwa pato halisi la Taifa kufikia asilimia 7.1 mwaka 2019 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7 mwaka 2018.
Serikali itaendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja kati ya asilimia 3 hadi asilimia 4.5 katika kipindi chote cha mwaka wa fedha unaoanza Julai 1 mwaka huu, ameeleza.
Dk Mpango amesema shabaha nyingine ni kuongeza mapato ya kodi kwa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi za ndani na kubuni vyanzo vipya vya mapato.
“Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.1 ya Pato la Taifa (GDP) mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 12.1 mwaka 2018/19,” amesema Dk Mpango.
Amesema matumizi ya Serikali yanatarajiwa kuwa asilimia 22.7 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20; na nakisi ya bajeti ikijumuisha misaada itakuwa asilimia 2.3 mwaka 2019/20.
Zinazohusiana:
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019/2020
- Dk Mpango-Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
Hata hivyo, Dk Mpango amesema katika kuzifikia shabaha hizo, Serikali itahakikisha inatoa kipaumbele kwa miradi ya viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini ili kukuza wa uchumi wa viwanda hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, madini na uvuvi.
Pia amesema Serikali itafungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwa kuendelea kusomesha kwa wingi wataalam kwenye ujuzi na fani mbalimbali, kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za tiba katika hospitali za rufaa za mikoa, kanda na Taifa na kuimarisha upatikanaji wa maji mijini na vijijini.
Miradi mingine itakayopewa kipaumbele ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha ‘Standard Gauge’; mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa mto Rufiji (Megawati 2,115); na kuboresha Shirika la Ndege Tanzania.
“Miradi mingine ni pamoja na: Kuboresha miundombinu ya reli za TAZARA, Tanga – Arusha, usafiri wa reli Dar es Salaam pamoja na kuboresha injini na mabehewa ya treni; ujenzi na ukarabati wa vivuko; na usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa REA,” amesema Dk Mpango.
Wakati Serikali ikijipanga kulenga dhabaha hizo tano, itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na vihatarishi vya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa 2019/20 vya upungufu wa rasilimali fedha, ushiriki mdogo wa sekta binafsi, umiliki wa ardhi na utatuzi wa migogoro, uharibifu wa mazingira na usalama mtandaoni.
Lakini pia vihatarishi vya nje ambavyo ni mtikisiko wa kiuchumi kikanda na kimataifa, matukio asilia, migogoro ya ndani na ya kimataifa na mabadiliko ya tabia nchi.