Jinsi ya ‘kuautomate’ machapisho kwenye mitandao ya kijamii

Davis Matambo 1052Hrs   Agosti 23, 2023 Teknolojia
  • Inasaidia kuokoa muda kwa kupanga mapema utakachopenda kuchapisha
  • Unaweza kutumia huduma hii kwenye Facebook, Instagram na X

Dar es Salaam. Ukuaji wa teknolojia umechochea matumizi ya mitandao ya kijamii duniani kote, sasa hivi haitumiki kwa mawasiliano ya watu binafsi pekee bali taasisi na baadhi ya kampuni hutumia mitandao hiyo kutangaza bidhaa au huduma ili kuvutia wateja.

Ili tuone taarifa kwenye mitandao ya kijamii ni lazima zichapishwe, lakini je?. Unafahamu kuwa si lazima uwe na simu au kompyuta mkononi muda wote ili uweze kupakia maudhui husika kwenye kurasa zako.

Ipo hivi, kila mtandao wa kijamii umewekewa kipengele kinachoruhusu mtumiaji kupangilia idadi ya machapisho anayotaka, muda pamoja na siku ya kuchapishwa kulingana na mahitaji ya mhusika.

Makala hii imedadavua namna unavyoweza kupangilia na kuchapisha katika kurasa za mitandao ya Facebook, Instagram pamoja na X (zamani Twitter).

Facebook na Instagram 

Hatua ya kwanza ni kuingia kwenye ukurasa wako wa meta business suite, kupitia jukwaa hili unaweza kusimamia shughuli zako za biashara kwenye mtandao wa Facebook na Instagram.

Hakikisha kuwa akaunti zako za Facebook na Instagram zimeunganishwa na Meta business suite yako kwani unaweza kuchagua kuchapisha katika jukwaa mojawapo au yote mawili kwa pamoja.

Kisha anza kutengeneza chapisho jipya kupitia mahali palipoandikwa ‘Create post’ na kuongeza picha, video sambamba na kuchagua mwonekano wa chapisho kwa hadhira yako.


Soma zaidi


Baada ya kuchapisha maneno, kuongeza picha na video, hatua inayofuata ni kutengeneza ratiba ya chapisho lako kwa kubonyeza kitufe cha ‘schedule’. Chagua tarehe na muda ambao unataka chapisho hilo kuonekana kwenye Facebook na Instagram.

Kabla ya kuthibitisha ratiba, soma vyema na kukagua maelezo yako ili kuhakikisha kila kitu ni sahihi, ukiridhika bonyeza kitufe cha ‘publish’ na baada ya hapo ‘post’ yako itakuwa tayari kuifikia hadhira kwa muda mwafaka ulioweka.

Mtandao wa X (zamani Twitter)

Ingia kwenye ukurasa wako, weka  ujumbe unaotaka kuchapisha, ongeza picha au video kama ungependa kuviambatanisha, nenda sehemu ya ‘Schedule’ hapo utaelekezwa kwenye kalenda kupanga tarehe na muda wa siku ambayo ‘post’ yako ungependa ionekane mtandaoni.

Ukimaliza kuchagua siku na muda utaelekezwa kwenye hatua ya kuthibitisha, kisha bonyeza kitufe cha ‘Schedule’ hapo utakua umekamilisha taratibu za kufuatwa na muda utakapofika chapisho litaonekana kwenye akaunti yako.

Muonekano wa ukurasa wa mtandao wa X sehemu unayoweza kupanga muda wa chapisho lako. PichalDavis Matambo/Nukta

Inaokoa muda 

Kwa kiasi kikubwa njia hii inaweza kukusaidia kuokoa muda wako ambao ungeutumia kila siku kuandaa maudhui na kutenga muda wa kuchapisha unaweza kuutumia kufanya shuhuli nyingine za uzalishaji na kuinua kipato chako.

Lucy Samson ambaye ni Meneja wa kurasa za mitandao ya kijamii ya JikoPoint ameiambia Nukta Habari kuwa mbinu hiyo inaokoa muda na kurahisisha kazi.

“kama kazi ni ya kufanya masaa mawili kila asubuhi ‘automation’ inasaidia kazi hiyo na wewe kufanya kazi nyingine,” amesema Samson ambaye pia ni mwandishi wa habari wa kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Afrika.

Related Post