WhatsApp sasa kuja na huduma ya ‘Channel’

Davis Matambo 0922Hrs   Juni 08, 2023 Teknolojia
  • Itakuwa na uwezo wa kuwakusanya zaidi ya watu 1,000.
  • Hautaweza kuona picha wala namba ya wafuasi wa chaneli husika.
  • Kuanza kupatikana Columbia na Singapore kwanza.

Dar es Salaam, Katika kuendelea kujiimarisha dhidi ya ushindani kwenye soko la mitandao ya kijamii mtandao wa mawasiliano wa WhatsApp umefanya maboresho mengine yanayokuwezesha kuunda au kujiunga na ‘chaneli’ ili uweze kutoa au kufaidi huduma mbalimbali.

Itakumbukwa awali mtandao wa huo ulikuwa unaruhusu kuunda kundi ambalo ukomo wake ilikuwa watu 250 tu na baadae wakafanya maboresho yaliyoruhusu hadi  watu 1,000 kupitia (broadcast) na sasa wametambulisha Channel ambayo itaruhusu mkusanyiko wa watu wengi zaidi.

Maboresho haya yatakuwezesha kuunda chaneli au kujiunga na chaneli hizo kwa kadri utakavyokuwa unapenda ambapo kutakuwa na sehemu maalumu ya kutafuta aina gani ya chaneli unayotaka kujiunga na pia unaweza kupata kiungo maalumu kupitia barua pepe au kwa kualikwa.

Faragha imezingatiwa


Tofauti na kwenye  makundi ambapo namba za watu waliomo ndani yake huwa zinaonekana kwenye maboresho haya wameondoa uwezekano wa mtu kuona picha pamoja na namba za wanachama  au mmiliki wa chaneli hiyo.

Hautaweza kupiga picha za ndani ( kuscreenshot ) au kuhamisha jumbe zilizopo kwenye chaneli husika kama mmiliki amezuia hayo kufanyika.

Katika taarifa yao iliyotolewa leo na mtandao wa WhatsApp imefafanua kuwa jumbe katika chaneli hizo utakaa kwa siku 30 kabla ya kufutika  ingawa wanafanyia kazi maboresho ya kufanya jumbe zifutike mapema zaidi.

“Tutawapa uwezo viongozi wa makundi kuamua uwezo nani ajiunge na upatikanaji wa chaneli hiyo, hata hivyo baadhi ya chaneli hazitakuwa na mfumo unaozikinga na mashambulizi ya wadukuzi bali tutaweka kwa chaneli zinazomilikiwa na taasisi au mashirika yasiyo ya kiserikali,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo

Mabadiliko haya yataanza kuonekana kwanza kwa watumiaji wa mtandao huo wa mawasiliano walioko nchini Colombia pamoja na Singapore ambapo watafanya kwanza majaribio kadhaa kabla ya watu wote kuanza kufaidi huduma hiyo.


Zinazohusiana


Wapo nyuma ya muda 

Hata hivyo mabadiliko hayo huenda yasipokelewe kwa shangwe sana kwa kuwa tayari watumiaji wa mtandao wa Telegram unaomilikiwa na raia wa Urusi Pavel Durov wanafaidi huduma hizo.

Mara kadhaa Durov ambaye mtandao wake una wafuasi takriban bilioni moja amekuwa akitupa vijembe kwa mshindani wake Mark Zuckerberg anayemiliki mitandao ya Instagram, Facebook pamoja na WhatsApp kuwa anaiga kile ambacho yeye alikifanya miaka mingi iliyopita.

Mtandao wa Whatsapp unatumiwa na watu zaidi ya bilioni tano ulimwenguni na inaaminika ndio jukwaa la mawasiliano linalotumika zaidi.

Related Post