Jinsi ya kuhariri na kuficha meseji zako WhatsApp

Davis Matambo 0722Hrs   Mei 24, 2023 Teknolojia
  • Ni mabadiliko ambayo yanatarajiwa kuboresha mawasiliano na kuingeza faragha
  • Yameanza kuonekana katika baadhi ya watumiaji wengine wakitakiwa kusubiri 

Dar es Salaam, Je! Umewahi kutuma ujumbe kupitia mtandao wa Whatsap kisha ukagundua haukuwa umeandika ujumbe huo  kwa usahihi lakini ukashindwa kurekebisha kutokana na ulikuwa umeshamfikia mhusika?

Na je umewahi kutamani kuficha baadhi ya jumbe zako katika Mtandao wa Whatsap ili  wengine wasizione zaidi ya wewe mwenyewe tu, lakini ukawa unashindwa kufanya hivyo.

Kama jibu ni ndiyo basi ondoa shaka kwa kuwa  suluhu ya matamanio yako imepatikana, na hii ni baada ya mtandao huo wa mawasiliano ulimwenguni kufanya maboresho kadhaa ikiwemo kumpa uwezo mtumaji wa ujumbe uwezo wa kuhariri ujumbe wake ndani ya dakika 15 pamoja na kuficha baadhi ya jumbe.

Mabadiliko haya yanatarajiwa kuboresha mawasiliano na kupunguza makosa yanayoweza kujitokeza kwa kutuma ujumbe usio kamili au usio sahihi.

Unawezaje kuhariri ujumbe wako.

Hatua ya kwanza unatakiwa kugusa na kushikilia ujumbe ambao unahitaji kuuhariri mpaka utakapopata machaguo ya kitendo unachotaka kufanya ambapo utachagua hariri (edit)

Hatua ya pili ni kuhariri ujumbe unaoutaka kisha utautuma tena kwa mhusika,  na ili kubaini kuwa ujumbe huo umehaririwa juu yake kutakuwa na maandishi yanayosomeka ‘imehaririwa’

Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba mpokeaji ujumbe ataarifiwa kwamba ujumbe umehaririwa, kwa hivyo ni muhimu kuwa makini wakati wa kuandika ujumbe wako au kuusoma upya kabla hujautuma ili kuepusha mkanganyiko.

Mfano wa namna mtu anavyoweza kuhariri ujumbe wake ndani ya Mtandao wa huo.PichalWhatsApp

Mazungumzo sasa kuwa faragha

Whatsapp imetambulisha mabadiliko mapya kwenye mtandao huo ambapo sasa mtumiaji wake anaweza kuficha baadhi ya jumbe zisionekane ambapo atalazimika kuweka nambari ya siri ili jumbe hizo zionekane pale tu atakapotaka.

Haya huenda ndio mabadiliko ambayo wengi wameyafurahia zaidi, vijana wa Tanzania wangesema ‘wameupiga mwingi’ kwani yataimarisha faragha na kudhibiti ile tabia ya baadhi ya watu kusoma jumbe zisizowahusu.

Ili kuficha mazungumzo yako kwenye WhatsApp cha kwanza chagua ujumbe unaotaka kuuficha, kandamiza kwa muda mpaka utakapopata machaguo kisha utachagua neno (lock) na ujumbe wako sasa utakuwa umefichwa.

Kumbuka, hautapokea taarifa yoyote kukuarifu kama kuna ujumbe mpya katika zile ulizoficha hivyo itakulazimu uwe unatazama mara kwa mara ili kubaini kama kuna ujumbe mpya.

Utaonaje ujumbe uliofichwa?

Ikiwa unataka kuupitia ujumbe uliofichwa, ni rahisi kwanza fungua mtandao wako wa Whatsapp ambapo moja kwa moja utakupeleka sehemu ya kupokelea ujumbe hapo utakandamiza sehemu iliyoandikwa WhatsApp kwa kidole chako na taratibu kishushe kuelekea chini.

Hatua itakayofuata utatakiwa kuweka nambari za siri au alama ya kidole kulingana na aina ya ulinzi uliochagua wakati ukificha jumbe hizo.

Hata hivyo mabadiliko haya hayapatikani kwa watumiaji wote wa mtandao huo,  utalazimika kusubiri kwa muda ili kuipata huduma hiyo ambayo imeanza kupatikana katika baadhi ya mataifa na kusasisha programu ya mtandao huo mara kwa mara ili uweze kufaidi huduma hizo.

Mabadiliko hayo yalitangazwa kwa mara ya kwanza Mei 15, 2023 na kisha kuboreshwa tena Mei 22, 2023 ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meta Mark Zuckerberg inayoimiliki mtandao huo alionesha mfano kupitia mtandao wa Facebook.

Mfano wa namna mtu anavyoweza kuficha ujumbe wake katikta mtandao wa WhatsApp.PichalWhatsApp

Related Post