Jinsi ya kuzuia matangazo YouTube

Lucy Samson 0238Hrs   Septemba 05, 2023 Teknolojia
  • Ni pamoja na kuzuia ‘personalized ads’ na kutumia program maalumu zinazozuia matangazo.
  • Kuzuia matangazo kunaweza kukosesha mapato kwa watengeneza maudhui.

Dar es Salaam. Maendeleo katika sekta ya teknolojia ya mawasiliano yamefanya matumizi ya mitandao ya kijamii kupigiwa chapuo kila uchwao. Tofauti na zamani, hivi sasa mtu asipotumia mitandao ya kijamii huonekana mshamba (asiyejua vitu).

Baadhi ya majukwaa ya kidijitali kama YouTube yamegeuka kuwa vyanzo vya kutegemewa vya taarifa, kupata ujuzi, pamoja na burudani, ambapo kwa wamiliki wa akaunti zinazochapisha maushui hayo ni sehemu ya kujiingizia kipato.

Kwa mujibu  wa takwimu za robo ya pili ya mwaka 2023 (Aprili-Juni 2023) zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) YouTube ndio mtandao unaotumiwa zaidi na Watanzania.

Mpaka kufikia Juni 2023 Gigabaiti milioni 50.1 za intaneti zilitumika kwenye mtandao huo ndani ya kipindi cha miezi mitatu ikifuatiwa na mitandao mingine maarufu kama Facebook, TikTok, Whatsapp pamoja na Instagram.

Hiyo inamaanisha kuwa mtandao huo ndiyo unaofuatiliwa zaidi na watanzania, jambo linaloufanya kutumiwa zaidi katika kutangaza bidhaa au huduma mbalimbali.


Soma zaidi


Hata hivyo, wakati mwingine matangazo hayo huwa kero kwa watazamaji na wafuatiliaji wa mtandao huo kutokana na kukatisha maudhui wanayoyatazama mara kwa mara.

Catherine Mosses, mmoja wa watumiaji wa mtandao huo ameiambia Nukta Habari kuwa wingi wa matangazo kwa siku za karibuni umekuwa kero kwake.

“Siku hizi matangazo yamekuwa mengi mpaka kero…kila mahali matangazo mpaka YouTube,” amesems Mosses.

Kama wewe ni mtumiaji wa mtandao wa YouTube na hupendi kubughudhiwa na matangazo hayo wakati unaperuzi mtandao huo kwa kutumia simu au kompyuta, mbinu hizi zinaweza kuwa suluhu.

Zuia ‘personalized ads’ 

‘Personalized ads’ ni matangazo yanayotokana na vitu unavyopendelea, mfano kama ukiingia YouTube unapenda kutazama video kuhusu urembo basi matangazo mengi unayopata wakati mwingine unapotumia mtandao huo yatahusiana na urembo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Google support aina hii ya matangazo inaweza kuzuilika kwa kufanya ‘setting’ katika simu au kompuya ya mtumiaji.

Kuzuia matangazo ya Youtube kwenye simu unachotakiwa kufanya ni kufungua Youtube, nenda kwenye ‘Setting’, bonyeza kitufe kilichoandikwa  ‘privacy’ kisha bonyeza ’google ads setting’ ambayo itakupeleka moja kwa moja sehemu ya kuzuia matangazo hayo.

Ikiwa unatumia kompyuta fungua Youtube kisha nenda kwenye ‘setting’ ikifunguka bonyeza palipoandikwa ‘channel’ kisha itakupeka moja kwa moja kwenye ‘advance setting’  ambapo chini kabisa utaona kitufe cha kuruhusu au kuzuia matangazo hayo.

Namna ya kuzuia matangazo ya YouTube kwa wanaotumia kivinjari cha Safari hususan wanaotumia simu za iPhone.PichalClario

Fanya usajili wa malipo

Njia nyingine ya kuepuka matangazo  ya Youtube yanayotokea mara kwa mara wakati wa kutazama video zinazopakiwa katika mtandao huo ni  kwa kufanya usajili wa malipo (premium subscription) ili kuyaondoa.

Mbali na kutazama video bila matangazo Youtube inasema ukilipia utaweza kupakua video na kutazama nje ya mtandao pamoja na kutazama  programu nyingine skrini yako ikiwa imezimwa.

Tumia programu za kuzuia matangazo

Kwa mujibu wa mtaalamu wa kompyuta Bonny Wilson, kuna programu nyingi zinazowezesha simu zenye mfumo wa Android, iOS au aina yoyote ya komputa kuzuia matangazo kuingia wakati anatumia mtandao wa Youtube.

“Programu kama AdGuard, AdBlock Plus, na uBlock Origin (kwa iOS) zinaweza kusaidia kupunguza matangazo,” amesema mtaalamu huyo.

Kwa kompyuta unaweza kutumia program kama ‘dBlock, uBlock Origin, na AdGuard’. Unachotakwa kufanya ni kuhifadhi kwenye kwenye kifaa chako kisha kuruhusu zizuie matangazo.

Tumia Kivinjari (browser) kinachozuia matangazo

Wilson ameongeza kuwa baadhi ya vivinjari (browser) vinavyotumika katika katika kompyuta au simu vimetengenezwa kuzuia matangazo moja kwa moja na kumpa mtumiaji uhuru wakati wote anapotumia mtandao.

“...kwa mfano ‘Brave’ na ‘Safari’ ni vivinjari vya kiwango cha juu kwenye iOS vinavyoweza kupunguza matangazo…kwa kompyuta unaweza kusanikisha ‘Firefox au Brave ukatumia kulingana na mahitaji yako,” ameongeza Bonny.

Aidha, Mtaalamu huyo ameongeza kuwa kuzuia matangazo, kunaweza kuathiri mapato ya wamiliki wa wavuti na watengeneza maudhui hivyo anawashauri watumiaji wa YouTube kutumia programu za kuzuia matangazo kwa uwajibikaji.

Wazalishaji maudhui hupata faida na kulipwa na mtandao wa Youtube kutokana na idadi ya matangazo yanayotizamwa na watu wanaofuatilia maudhui yao.

Related Post