Watumiaji wa X (Twitter) sasa kupiga video call

Davis Matambo 0745Hrs   Septemba 02, 2023 Teknolojia
  • Ni hatua ya kimkakati kushindana na mitandao mingine inayotoa huduma hiyo.
  • Kupatikana kwa watumiaji wa aina zote za simu na kompyuta.

Dar es Salaam. X, mtandao wa kijamii ambao awali ulijulikana kama Twitter, umetangaza mipango yake ya kuzindua simu za video na sauti ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma zake kwa wateja na kuukabili ushindani unaozidi kuibuka kwenye teknolojia ya mawasiliano.

Vipengele hivyo vipya vitaruhusu watumiaji kuwasiliana wao kwa wao kupitia programu hiyo bila uhitaji wa namba za simu, na kufanya X kuwa miongoni mwa mitandao inayoweza kutoa huduma hiyo.




Mitandao ya kijamii ya WhatsApp, Telegram, Instagram, Facebook pamoja na Snapchat tayari ilikuwa na uwezo huo hivyo kwa X kuboresha mtandao huo ni kuimarisha ushindani na kuwafanya watu waendelee kutumia zaidi mtandao huo ulionunuliwa  kwa mabilioni ya fedha.

Mabadiliko hayo yanakuja siki chache  tangu mtandao huo uanze kutoa malipo kwa watu wanaozalisha maudhui kwenye mtandao huo, ambao hulipwa kwa kulingana na idadi ya watu waliotazama na kutoa maoni kwenye machapisho yao.

Hata hivyo, Elon Musk ambaye ndiye mmiliki wa mtandao huo, hajabainisha ni lini haswa huduma hii itaanza kutumika lakini ameweka bayana kuwa itawafaidisha na kupatikana kwa watumiaji wa simu janja za aina zote yaani android na iOS pamoja na kompyuta. 


Soma zaidi


Afisa Mafunzo na Utafiti kutoka Nukta Africa Daniel Samson, ambaye amekuwa akitumia mtandao huo katika shughuli zake ameiambia Nukta Habari kuwa Elon anajaribu kuwa karibu na watumiaji ndio maana siku za karibuni amekuwa akifanya mabadiliko makubwa kwenye mtandao huo.

Mabadiliko mengine yaliyofanywa na Musk tangu alipoinunua Twitter mwezi Oktoba 2022, kwa zaidi ya Sh110 trilioni ni pamoja na chapa ya jukwaa hilo, kurejesha watumiaji waliofungiwa, kufuta kipengele cha kumzuia mtu na kuanzisha mfumo wa malipo.

X inalenga kuwa nafasi ya mbele dhidi ya Meta Platforms kampuni inayomiliki mtandao wa Facebook, Instagram, WhasApp na Threads ambayo pia inapanua huduma zake na kujumuisha huduma za uhalisia pepe ‘virtual reality’ na ‘metaverse’.

Hata hivyo, mabadiliko ya X yanazua utata kwa baadhi ya watumiaji ambao wasiwasi wao ni kuhusu faragha, ikiwa jukwaa hilo litajidhatiti kwa uthabiti kulinda mawasiliano baina ya waongeaji dhidi ya wasiohusika.

Kwa sasa mawasiliano rasmi kwa njia ya video hufanyika zaidi kupitia mtandao wa Zoom, Google meeting, Microsoft, Skype pamoja na Switchboard.

Related Post