Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lajipanga kujiimarisha kwa vifaa vya Sh260 bilioni.

Mariam John 0936Hrs   Juni 19, 2024 Habari
  • Mwanza kupata helicopta pamoja na boti ya uokozi.
  • Vifaa kuanza kuwasili Septemba 2024.


Mwanza. Serikali imesema imetenga Sh260 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya uokozi kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ambalo limekuwa likikabiliwa na upungufu mkubwa wa vifaa hivyo, jambo lililokuwa likiathiri utendaji wake.

Kwa muda sasa wananchi wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uokozi jambo linalosababisha kuchelewa kwa msaada wa haraka pale unapohitajika.

Matahalan matukio ya hivi karibuni yaliyozua mijadala na ukosoaji mkubwa wa vifaa duni vya uokozi kwa jeshi hilo ni pamoja na maporomoko ya matope huko Hanang mkoani Manyara na pamoja na ajali ya kuanguka kwa ndege Ziwa Victoria Novemba 5, 2022 iliyotokea mkoani Kagera.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji John Masunga aliyekuwa akizungumza leo Juni 18, 2024 mara baada ya kuwavisha nishani maofisa 65 wa jeshi hilo amewaambia wanahabari kuwa vifaa hivyo vitatumika kukabiliana na majanga na kurahisisha shughuli za uokoaji.

“Kwa muda mrefu Jeshi la Zimamoto limekuwa na changamoto ya vifaa vya uokoaji, Serikali imeliona hilo na kuanzia mwezi Desemba mwaka huu vifaa hivyo vitakuwa vimenunuliwa na na kuanza kutolewa kwenye ofisi za uokoaji nchi nzima,” amesema Masunga

 Maofisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakiwa kwenye gwaride muda mfupi kabla hawajaanza kuvishwa nishani na Kamishina Jenerali wa jeshi hilo John MasungalPicha.Mariam John/ Nukta

Masunga ameongeza kuwa kutokana na madhari ya mkoa wa Mwanza, Serikali imepanga kuwapatia ndege aina ya helicopta pamoja na boti ya uokozi.

“Mwanza tumezingatia ununuzi wa helkopita na boti kwa sababu mbili kwanza uwepo wa makazi ya milimani lakini visiwa vingi vilivyopo ndani ya Ziwa Victoria, hivyo iwapo kutatokea janga la namna yoyote, vifaa hivyo vitasaidia katika uokoaji wa haraka,” ameongeza Masunga.

Kamishina huyo amesisitiza suala la wananchi kupeleka ramani za ujenzi wa makazi yao ili wapate ushauri kutoka kwa jeshi hilo namna ya kujenga nyumba zao ili iwe rahisi kufikiwa pale kunapojitokeza janga la aina yoyote.

Aidha, Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Elikana Balandwa amewataka wote waliokabishiwa dhamana ya kuhakikisha usalama wa raia na mali zao kutekeleza majuku yao ipasavyo.

“Niwatake mliovishwa nishani leo kuwa bora kwa wengine na kuendelea kuzingatia maadili ya kazi zenu,”amesema Balandya

Related Post