RC Mwanza ahimiza wafugaji kuongeza kasi ya ufugaji ng’ombe wa maziwa

May 30, 2024 4:47 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema kuna fursa nyingi za ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. 
  • Unywaji wa maziwa nchini wafikia lita 67.5 kati ya lita 200 zinazoshauriwa na WHO.

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda, amewataka wafugaji kuongeza kasi ya ufugaji wa wa ng’ombe wa maziwa ili kuongeza upatikanaji wa zao hilo kwa wingi.

Mtanda ametoa maagizo hayo wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya maziwa inayoendelea jijini Mwanza na kubainisha kuwa bado kuna idadi ndogo ya ng’ombe wa maziwa hali inayosababisha baadhi ya wananchi kutomudu gharama za maziwa hayo hivyo kusababisha idadi ndogo ya watumiaji.

“Katika kipindi cha mwaka 2023/24 kulikuwa na ng’ombe wa maziwa takribani milioni 1.4 nchini ambapo hutoa wastani wa lita bilioni 3.9 kwa mwaka, pia kulikuwa na viwanda 130 vya maziwa vilivyokuwa vinasindika lita milioni 81 za bidhaa hiyo na kuuzwa hapa nchini,” amesema Mtanda.

Kwa upande wa mkoa wa Mwanza mtanda amesema una jumla ya ng’ombe wa maziwa 16,223  ambao huzalisha wastani wa lita 81,115 kila siku.

Hata hivyo, kiwango hicho bado ni kidogo kulinganisha na mahitaji ya wananchi milioni 3.6 waliopo mkoani humo.


Soma zaidi:Afrika inavyoweza kukabiliana na baa la njaa


Unywaji  wa maziwa badobado Tanzania

Kiongozi huyo amebainisha kuwa hali ya unywaji wa maziwa kitaifa katika kipindi cha mwaka 2023/24 inaonesha mtu mmoja alikunywa lita 67.5 kiasi ambacho ni kidogo  kulinganisha na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mtu mmoja kunywa lita 200 za maziwa kwa mwaka mmoja.

“Sasa wapo watu wanakunywa glasi nyingi za bia kuliko maziwa, ushauri unatolewa angalau kwa siku mtu upate glasi moja, nichukue fursa hii kuwahamasisha wananchi wa Mwanza, Kanda ya Ziwa na Watanzania kwa ujumla kuongeza kasi ya unywaji maziwa yaliyosindikwa, yamethibishwa kuwa bora na salama,” amesema Mtanda.

Kwa mujibu wa Mtanda, mpango uliopo ni kuongeza uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa kupitia shamba la Serikali la Mwabuki ambalo limepokea majike 500 ya ng’ombe wazalishwe na kusambazwa kwa wafugaji wa Kanda ya Ziwa ili kuongeza uzalishaji na desturi ya unywaji maziwa mkoani humo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Maziwa (TDB) Zacharia Masanyiwa amesema tasnia ya maziwa inachangia asilimia mbili ya pato la Taifa, lakini fursa bado zipo nyingi katika sekta ya maziwa na kuwataka wananchi wazichangamkie.

Kauli ya Masanyiwa imeungwa mkono na Msajili wa Bodi ya Maziwa, Profesa George Msalya aliyebainisha thamani ya maziwa yanayozalishwa nchini kufikia Sh1.3 bilioni na kwamba yana mchango mkubwa wa kujenga uchumi wa nchi yetu na ajira ya kudumu kwa wananchi.

Enable Notifications OK No thanks