Wavuvi wa dagaa Mwanza walia na mabadiliko ya nyavu, umbali wa kuvulia

June 18, 2024 2:58 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Wasema mabadiliko hayo yanapunguza tija iliyoanza kupatikana kupitia uvuvi
  • Serikali yasisitiza ni kwa ajili ya kutunza mazingira na rasilimali za uvuvi Ziwa Victoria.

Mwanza. Wavuvi mkoani Mwanza wamekosoa utaratibu mpya wa kuvua dagaa uliotangazwa ambao unawataka kupunguza urefu na upana wa nyavu zao pamoja na kutovua umbali wa kilomita mbili kutoka ufukwe wa ziwa.

Utaratibu huo uliotakiwa kuanza kutumika Juni 15, 2024 unakuja wakati ambao tija ya uvuvi wa dagaa kupitia kufunga ziwa Victoria wakati wa mwandamo wa mwezi ikianza kuonekana.

Wavuvi hao wanaofanya shughuli zao katika Kisiwa cha Bwiro Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza wamebainisha kuwa pamoja na Serikali kuwa na nia njema ya kutunza mazalia ya samaki, itafutwe njia nzuri ambayo haitaathiri pande zote mbili.

Wambura Mwita ambaye ni ni Mvuvi wa dagaa katika kisiwa hicho amesema maelekezo hayo ya Serikali yamelenga kurudisha nyuma tija ya uvuvi iliyoanza kuonekana katika kipindi cha miezi zaidi ya 6 iliyopita.

“Maelekezo haya ya Serikali ya mara kwa mara yanatuchanganya kila mara wanabadilisha zana za kuvulia na juzi tumepokea barua nyingine ya kufanyia mabadiliko nyavu zetu kutoka mita 60 kwa 40 na kufikia mita 60 kwa 20,” amesema Mwita.

Kwa upande wake Mawazo Msilikale, ambaye ni Mwenyekiti wa Kisiwa cha Bwiro amewashauri viongozi wa mamlaka husika kuwashirikisha kwanza wananchi wananoishi katika maeneo hayo kabla ya kufanya maamuzi ili kupunguza athari zinazoweza kutokea.

Msilikale amesisitiza kuwa shughuli ya uvuvi inategemewa na zaidi ya kaya 6,000 ambapo watu wanaojishughulisha na uvuvi wanakadiriwa kufikia12,000.

“Tunaidadi kubwa ya watu na pale tunapowekewa masharti tunakosa cha kufanya kwakuwa idadi ya watu hawa wanategemea ziwa ili wale na watoto waende shule,” amesema Msilikale

Hata hivyo, mbali na mabadiliko ya mita hizo za nyavu, wavuvi hao pia wanalalamikia umbali wa eneo la kuvulia wakieleza kuwa kutokana na mwingiliano wa visiwa vilivyopo ziwani unaweza kusababisha mita zilizoainishwa kusababisha migogoro.

Kwamjibu wa nyaraka iliyotolewa  na  idara ya uvuvi  chini ya kifungu cha 4(3) cha sheria ya Uvuvi sura ya 279 inasema uamuzi huo ni kulinda na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini.

Waraka huo umeonyesha kuwepo kwa changamoto zinazo tokana na uvuvi wa dagaa wa kutumia wavu usiokuwa na ukomo hali inayosababisha wavuvi kuvua kwa wingi samaki wachanga aina ya sangara na aina nyingine ya samaki wasiokusudiwa jambo ambalo linasababisha uharibifu wa mazingira, mazalia ya samaki na kutishia uendelevu wa rasilimali za uvuvi Ziwa Victoria.

Mwenyekiti chama cha wavuvi Tanzania (Tafu), Bakari Kadabi amesema kama chama walishirikiana na Serikali kupitisha mabadiliko hayo na baadhi ya wavuvi wa dagaa walishiriki kupitisha maazimio hayo kwa maslahi ya sekta ya uvuvi.

Enable Notifications OK No thanks