Wanafunzi zaidi ya 2,400 wa elimu ya juu wanufaika na mikopo ya HESLB

Daniel Samson 0820Hrs   Oktoba 29, 2018 Habari



  • Wanafunzi 12,071 watapangiwa mikopo katika awamu inayofuata ili kukamilisha idadi iliyopangwa ya wanafunzi 40,000.
  • Utoaji wa mikopo hutegemea ulinganifu wa orodha ya waombaji na udahili wa vyuo inayotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
  • Idadi ya wanafunzi waliopata mikopo hadi sasa ni sawa na asilimia 69.8 ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaotarajiwa kupata mikopo hiyo.

Wanafunzi wapatao 2,397 wa elimu ya juu wamepangiwa mikopo katika awamu ya pili ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 na kufanya idadi ya wanufaika wa mwaka wa kwanza kufikia 27,929. 

Idadi hiyo ya waliopata mikopo hiyo muhimu ni sawa na asilimia 69.8 ya wanafunzi 40,000 wa mwaka wa kwanza au sawa na wanafunzi saba kwa kila 10 ya wanaotarajiwa kupatiwa mkopo na bodi hiyo yenye makao yake makuu Mwenge jijini hapa.

 Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru imesema kuwa idadi ya wanafunzi waliobaki wapatao 12,071 watapangiwa mikopo katika awamu inayofuata ili kukamilisha idadi iliyopangwa.

"Orodha ya majina ya wanafunzi hao  27,929 waliokwishapangiwa mikopo inapatikana kwenye tovuti ya HESLB na itatumwa kwenye vyuo husika kwa ajili ya hatua zaidi za kukamilisha malipo ya mikopo hiyo," amesema Badru.

Serikali iliidhinisha ya Sh427.5 bilioni kwa ajili ya kuwapangia wanafunzi wapatao 123,285 wa elimu ya juu ikijumuisha wale wanaoendelea na wale wa mwaka wa kwanza wa 2018/2019 ambao baadhi wameanza kuripoti katika vyuo mbalimbali nchini.


Zinazohusiana: 


Hata hivyo idadi ya wanafunzi waliopata mkopo mwaka huu imeongezeka ikilinganishwa na mwaka 2017/2018 ambapo Serikali ilitenga bajeti ya Sh427 bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ambapo waliopata mikopo hiyo walikuwa 33,244 kati ya zaidi ya 66,000 waliotuma maombi.

Oktoba 17 mwaka huu, wakati HESLB ikitangaza orodha ya majina ya wanafunzi waliopata mikopo awamu ya kwanza, Badru alinukuliwa akisema upangaji mikopo unategemea orodha ya wanafunzi waliodahiliwa kutoka TCU ambapo mpaka sasa imefikia wanafunzi 49,000. 

Related Post