Bajeti ya Wizara ya Nishati Tanzania yapungua kwa Sh1.1 trilioni

Lucy Samson 0710Hrs   Aprili 24, 2024 Habari
  • Kiwango hicho cha bajeti kilichoombwa kimeshuka kwa asilimia 38.2. 
  • Bajeti iliyoombwa kwa mwaka ujao wa fedha ni Sh1.88 trillioni kutoka Sh3 trilioni iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2023/24.

Dar es Salaam.Serikali ya Tanzania imepunguza bajeti ya Wizara ya Nishati kwa Sh 1.1 trilioni baada ya kuliomba Bunge liidhinishe Sh1.8 trilioni kwa ajili ya matumizi ya mwaka wa fedha wa 2024/25 licha ya kuwepo mahitaji makubwa ya huduma za nishati nchini. 

Kiwango hicho cha bajeti kilichoombwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko bungeni leo (Aprili 24, 2024) kwa ajili ya mwaka wa fedha unaoanza Julai 1, kimeshuka kwa asilimia 38.2 kutoka Sh3 trilioni iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2023/24.

Miongoni mwa mambo yanayosubiri fedha itakayoidhinishwa na Bunge baada ya kuijadili bajeti hiyo ni pamoja na mradi wa usambazaji wa umeme vijijini pamoja na kumaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini ambayo imekuwa kero kubwa kwa baadhi ya maeneo nchini.

Miradi mingine ni kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG) na ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (East  African Crude Oil Pipeline - EACOP) na ukamilishwaji wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Julius Nyerere (JNHPP) ifikapo Desemba 2024.

Dk. Biteko amewaeleza wabunge kuwa fedha hizo alizoomba kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kwa ajili ya shughuli mbalimbali za wizara na taasisi zilizo chini yake.

“Sh1.7 trilioni sawa na asilimia 95.2 ya bajeti yote ya wizara ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo, kati ya fedha hizo, Sh1.5 trilioni ni fedha za ndani na Sh258.8 bilioni ni fedha za nje,” amesema Dk Biteko.


Soma zaidi:Bajeti ya Muungano na Mazingira yapaa kwa Sh6.3 bilioni


‘Mpunga’ wa miradi ya maendeleo wapungua

Wakati bajeti ya wizara hiyo ikipungua kwa ujumla, fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo nayo imepungua kwa Sh 814.2 bilioni kutoka Sh2.6 trilioni iliyotengwa mwaka wa fedha unaoishia mwezi Juni mwaka huu.

Mbali na ufinyu wa bajeti hiyo Waziri Biteko aliwahakikishia wabunge kuwa kuidhinishwa kwa fedha kuitafanya wizara yake kutekeleza vyema miradi yote iliyopangwa kwa mwaka huu wa fedha.

“Katika mwaka 2024/25 Wizara ya Nishati itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kusimamia, kuimarisha na kuendeleza sekta ya nishati, kwa lengo la kuhakikisha sekta hii inachangia ipasavyo katika maendeleo ya Taifa letu na watu wake kama inavyotarajiwa,” amesema Dk Biteko.

Kwa takriban miaka mitano sasa, miradi mikubwa ya nishati kama JNHPP iliifanya wizara hiyo kutumia kiwango kikubwa cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Madini Dk. David Mathayo amewaambia wabunge kuwa wizara hiyo imepokea bajeti kiduchu kutokana na kukamilika kwa baadhi ya miradi mikubwa ikiwemo  Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP).


“Kamati ilielezwa kwamba kupungua kwa bajeti hiyo ni kutokana na ukomo wa bajeti ya wizara na kukamilika mradi wa  bwawa la Julius Nyerere ambao bajeti yake ilikuwa Sh1.5 trilioni sawa na asilimia 51.72 ya bajeti yote ya maendeleo iliyotengwa kwa wizara,” amesema Dk. Mathayo.

Aidha, Mwenyekiti huyo amelitaka Shirika la Umeme (Tanesco) kuongeza kasi katika usimamizi wa miradi ya kuzalisha umeme ilikuwezesha nchi kuwa na utoshelevu wa umeme wa uhakika huku kipaumbele kikiwekwa katika maeneo uzalishaji kama migodi, viwanda na skimu za umwagiliaji.
 

Related Post