Punda wanavyorahisisha maisha ya wakazi Iziwa, Mbeya
- Baadhi huwatumia kama chanzo cha kipato, hukodisha mmoja kwa Sh5,000 hadi 7,000 kwa siku.
- Hutumika zaidi kubeba mizigo mizito ikiwemo mazao.
- Ni kutokana na jiografia ya maeneo hayo kuwa ya milima na miinuko mikali.
Mbeya. ‘Punda afe mzigo ufike’ ni msemo maarufu wa Kiswahili unaotumika sana nchini Tanzania, ambao unasawili uwezo wa mnyama huyo kubeba na kusafirisha mizigo mizito kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia yaliyowezesha uwepo wa nyanja mbalimbali za usafirishaji kama vile magari, pikipiki au baisikeli, bado katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania, punda anatumika kama chombo cha usafiri.
Ukiwa katika maeneo ya Ghana, Ilemi, Isanga na Itiji katikati ya jiji la Mbeya nyakati za asubuhi ni kawaida kuwaona wanyama hao wakiwa wanasagwa na mizigo yao mgongoni kuelekea sokoni.
Punda hao wanatokea katika kata ya Iziwa nje kidogo ya jiji la Mbeya ambapo ili uweze kufika kwenye kata hiyo itakulazimu kutembea kwa zaidi ya umbali wa kilomita saba ukitumia barabara ya vumbi peke yake ambayo inaunganisha kata hiyo na kata nyingine.
Kata hiyo ina jumla ya mitaa mitano ambayo ni Iduda, Ilungu, Imbega, Isengo na Isumbi na ambayo jigrofia yake ni miinuko na milima mikali inayochangia hali ya maendeleo ya barabara kuwa duni kufika maeneo mbalimbali ya kata hiyo ikiwemo kuiunganisha na kata nyingine za mjini.
Jestina Ndele, Mkazi wa Kata ya Iduda ambaye pia ni mfugaji wa Punda ameiambia Nukta Habari kuwa anafurahia kufuga wanyama hao kwa kuwa wanamsaidia katika shughuli zake za kila siku ikiwemo kusafirisha mazao kutoka shambani hadi nyumbani.
Jestina Ndwele akiswaga punda wake kuelekea nyumbani akiwa amebeba zaidi ya debe 6 za mahindi.PichalSamuel Ndoni
Jestina anamiliki punda watatu ambapo kila siku asubuhi hubeba viazi kutoka Iziwa hadi mjini kuviuza na wakati wa kurudi wanyama hao hubeba mahitaji ya nyumbani aliyoyanunua mjini.
“Punda wangu mmoja ana uwezo wa kubeba hata debe sita za mahindi na viazi vingi, pia ana uwezo wa kupita maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi na bodaboda kutokana na kuwepo na milima mingi na miinuko mikubwa’’ amesema Ndele.
Umuhimu wa punda kwa Jestina haupo tu kwenye uwezo wa kubeba mizigo mizito ambayo usafiri wa pikipiki maarufu kama boda boda usingeweza, bali wanyama hao wana uwezo wa kuhimili barabara zenye milima mikali iliyosheheni katika eneo hilo.
Kwa upande wake Eda Mwando, ambaye nae ni Mkazi wa Kata hiyo hiyo ya Iduda, yeye hutumia punda kuchota maji ambayo yapo umbali wa takribani kilomita tatu kutoka kijijini kwao ambapo punda mmoja ana uwezo wa kubeba kati ya ndoo sita hadi nane za maji, zenye ujazo wa lita 20.
Eda amesisitiza kuwa, kama angeamua kuchota kiwango hiko cha maji kwa kujitwisha ndoo kichwani basi huenda angetumia siku nzima na hivyo kuathiri shughuli nyingine za kiuchumi.
Punda ni mchongo
Wakati Eda na Jestina wao wakitumia punda kama chombo cha usafiri, hali ni tofauti kwa Nesi Saimon ambaye yeye hutumia kama chanzo cha mapato.
Saimoni anawashukuru punda kwa kuwa walimsaidia kupata kiasi cha fedha iliyotosha kununua kiwanja baada ya kuuza punda 10 kati ya aliokuwa nao ambapo kila mmoja alimuuza kwa Sh170,000.
Kwa sasa Saimon amesaliwa na punda sita ambao huwakodisha kwa watu wengine kwa ajili ya kubebea mizigo ambayo mara nyingi ambapo hutoza Sh5,000 kwa punda mmoja kwa siku.
Kwa kutambua umuhimu wa punda katika kata hiyo, Diwani wa kata ya Iziwa Kefasi Mwasote ameiambia Nukta Habari kuwa viongozi na kata na mitaa hutumia mikutano ya hadhara kuhamasisha wananchi kuwa na angalau punda mmoja kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali.
Punda mmoja ana uwezo wa kuishi takribani miaka 100 akiwa na nguvu pamoja ari ya kubeba mizigo. PichalSamuel Ndoni
Kiongozi huyo wa kata anasema punda mmoja ana uwezo wa kuishi takribani miaka 100 akiwa na nguvu pamoja ari ya kubeba mizigo, lakini anaweza kupata changamoto ikiwa hapati chakula cha kutosha, kujinyonga baada ya kubeba mizigo mizito au matatizo wakati wa muda wa uzazi.
‘’Mimi binafsi nimefuga punda, na nilikuwa nakodisha punda mmoja kwa sh. 7,000 kwa siku, hivyo nilikuwa nina uwezo wa kuingiza sh.48,000 kwa siku kwa sababu nina jumla ya punda nane, pia ukiwa na wanyama hawa hauwezi kuweka vibarua wa kubeba mizigo, hivyo unaokoa pesa nyingi, kubwa zaidi ninachojivunia nimejenga nyumba kwa ajili ya wanyama hawa’’ amebainisha Mwasote.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa kata ya Iziwa Demistus Nafilisa, mpaka mwaka 2022 kata hiyo ilikuwa na jumla ya punda 45, ingawa huenda ikawa zaidi ya hapo kutokana na asili ya wanyama kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na shughuli zao za kila siku za kubeba mizigo.
Kwa mujibu wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi (2022) kata hiyo ina jumla ya watu 3,834 ambapo kati yao wanaume ni 1,804 na wanawake ni 1,096 na kwamba zaidi ya nusu ya wakazi wake wanajihusisha na shughuli za kilimo cha mazao ya chakula, matunda na biashara.
Je unafahamu punda ni mnyama wa aina gani? Uhusiano wake na binadamu upoje? Ungependa kujua namna ya kufuga na vitu unavyopaswa kuzingatia. Usikose kusoma sehemu ya pili ya makala hii itakayoitwa ‘mfahamu mnyama punda kiundani’
Makala hii imeandikwa na Samuel Ndoni, mwandishi wa habari aliyepo jijini Mbeya anapatikana kwa nambari za simu 0677202000 au barua pepe samuelndoni@gmail.com