100 wagundulika kuwa na dalili za saratani Mwanza

Mariam John 0736Hrs   Machi 01, 2024 Afya & Maisha
  • Asilimia 45 wahundulika kuwa na tezi dume.
  • Nusu ya wagonjwa wa saratani hufariki nchini kila mwaka.

Mwanza. Wananchi zaidi ya 100 kutoka Wilaya za Sengerema na Nyamagana za mkoani Mwanza pamoja na Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wamegundulika kuwa na dalili za awali za ugonjwa wa saratani.

Dalili hizo zimebainika baada ya uchunguzi wa kitabibu kufuatia kampeni ya upimaji wa magonjwa bure iliyoendeshwa na Hospitali ya Rufaa ya Bugando inayolenga kupunguza athari na vifo vitokanavyo na magonjwa ya saratani.

Waliobainika kuwa na saratani ni kati ya wagonjwa 500 waliojitokeza katika kampeni hiyo ambapo majibu ya vipimo yanaonesha asilimia 45 ya wagonjwa wamegundulika kuwa na dalili za saratani ya tezi dume.

Itakumbukwa kuwa  mwaka 2021 kanzi data ya wagonjwa wa Saratani  iliyopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume kwa asilimia 21%.

Hii ina maana kuwa, katika kila wagonjwa 10 wa saratani wawili kati yao wanaugua saratani ya tezi dume.

Mkuu wa idara ya mionzi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Magreth Magambo amesema miongoni mwa sababu inayochochea vifo vya wagonjwa wa saratani ni pamoja na mila potofu kuhusu ugonjwa huo.

“Wananchi wengi wana imani potofu kuhusu ugonjwa huu, wapo ambao hawataki kabisa kuamini kuwa wana  ugonjwa wa saratani na wengine wanakimbilia tiba mbadala kwa ajili ya matibabu ambazo zinawasababishia madhara zaidi,” amesema Magambo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo Dk. Fabian Massaga amesema takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka wananchi zaidi ya elfu kumi wenye umri kati ya miaka 15 wanagundulika kuwa na changamoto ya saratani na kati yao  wananchi elfu sita wanapoteza maisha sawa na asilimia 50 ya wagonjwa wote.

Dk Massaga ametaja sababu zinazochangia watu hao kupoteza maisha kuwa ni kuchelewa kufika sehemu za kupatia huduma za afya aidha kwa kutokuwa na fedha au kutumia tiba mbadala ambazo haziendani na ugonjwa husika.

“Kwa kulitambua hilo, hospitali ya kanda imeamua kufanya kampeni ya upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza kwa wananchi wa Wilaya za Nyamagana, Sengerema na Busega ili kurudisha fadhila kwa wananchi ili waweze kupata huduma,”amesema Dk. Massaga.

Related Post