Ufaulu ya darasa la nne washuka kwa asilimia 3.35
- Necta wasema watahiniwa waliopata daraja E wameongezeka kwa asilimia 3.5
- Licha ya kushuka kwa ufaulu wanafunzi milioni 1.3 wamefaulu kwa daraja A,B,C na D.
Dar es Salaam. Huenda siku ya leo itakuwa nzuri na mbaya kwa wazazi na wanafunzi baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa upimaji wa kitaifa (SFNA) wa darasa la nne kwa mwaka 2022 huku ufaulu ukishuka kidogo kwa asilimia 3.35.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mtihani huo leo Januari 4, 2022 jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi amesema asilimia 82.5 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo wamefaulu.
“Watahiniwa milioni 1.3 kati ya milioni 1.5 wenye matokeo wamefaulu mtihani kwa kupata madaraja A, B,C na D,” amesema Amasi mbele ya wanahabari.
Miongoni mwa watahiniwa waliofaulu mtihani huo, wasichana ni 694,547 sawa na asilimia 52.5 na wavulana ni 626,153 (asilimia 47.4).
Wanafunzi milioni 1.7 walisajiliwa kufanya mtihani huo uliofanyika Oktoba 26 na 27, 2022 ukihusisha masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Hesabu, Sayansi na Maarifa ya Jamii.
Kati yao, wanafunzi milioni 1.5 sawa na asilimia 92 ndio waliofanya mtihani huo ambapo kati yao, wasichana walikuwa 819,675 sawa na asilimia 51.4.
Wanafunzi 126,296 sawa na asilimia 7.5 hawakufanya mtihani huo kutokana na sababu mbalimbali wakiwemo wavulana ni 74,972.
Soma zaidi
-
Necta yatangaza matokeo ya kidato cha pili ufaulu ukishuka
-
Sayansi, hesabu zaendelea kuwaliza wanafunzi kidato cha pili 2022
Wakati idadi ya ufaulu ukishuka idadi ya watahiniwa walioshika mkia kwa kupata daraja E imeongezeka kwa asilimia 3.35 ukilinganisha na idadi ya waliofeli mwaka jana.
“Wataniwa 271,535 wamepata alama E sawa na asilimia 17.05,” imesema taarifa iliyotolewa na Amasi.
Hiyo ni sawa kusema takriban watahiniwa wawili kati ya 10 wamefeli mtihani huo.
Mbali na waliopata daraja E, watahiniwa 61,330 sawa na asilimia 3.8 wamepata daraja A), huku waliopata daraja B wakiwa 223,063 sawa na asilimia 14.1.
Sambamba na hao watahiniwa 534,510 sawa na asilimia 33.5 wamepata daraja C huku watahiniwa 501,797 sawa na asilimia 31.5 wamepata daraja D.
Hiyo ni sawa kusema asilimia 65 au takriban watahiniwa 7 kati ya 10 wamepata daraja C na D ambalo kwa mpangilio wa Necta wamefaulu.