Necta yatangaza matokeo ya kidato cha pili ufaulu ukishuka

January 4, 2023 10:23 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ufaulu wa jumla washuka kwa asimia 7.4.
  • Zaidi ya nusu ya watahiniwa wapata daraja la nne. 
  • Wasichana waongoza kwa ufaulu kwa asilimia 52.5 zaidi ya wavulana.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili kwa mwaka 2022 huku ufaulu ukishuka kwa asilimia 7.4 ikilinganishwa mwaka 2021.

Watahiniwa 539,645 kati ya 633,537 wenye matokeo waliofanya mtihani huo Novemba 2022, wamefaulu sawa na asilimia 85.18

Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athuman Amasi aliyekuwa  akitangaza matokeo hayo leo Januari 4, 2022 jijini Dar es Salaam amesema kati ya watahiniwa waliofaulu asilimia  52.5 ni wasichana.

“Kati ya watahiniwa 539,645 waliofaulu wasichana ni 283,541 sawa na 52.5  na wavulana ni 256,104 sawa na asilimia 47.5,” amesema Amasi.

Jumla ya wanafunzi 690,341 walisajiliwa kufanya mtihani Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili uliofanyika Novemba mwaka jana huku wasichana  wakiwa 367,013 sawa na asilimia 53.16 na wavulana 323,328 sawa na asilimia 46.84. 

Kati ya wanafunzi waliosajiliwa, wanafunzi 635,130 sawa na asilimia 92 walifanya mtihani huo wakiwemo wasichana 342,210 sawa na asilimia 93.24 na wavulana 292,920. 

Amasi amesema watahiniwa 55,211 sawa asilimia 8 kati ya watahiniwa waliosajiliwa hawakufanya mtihani huo, huku wavulana wakiwa ni 30,408 sawa na asilimia 9.40.


Soma zaidi


Viwango vya ufaulu wa madaraja navyo vyashuka

Hata wakati matokeo ya ufaulu wa jumla yakishuka hali ni mbaya zaidi kwenye ufaulu wa madaraja ya masomo.

Kwa mujibu wa Necta, ni asilimia 7.65 ya wanafunzi waliofanya mtihani huo wamepata daraja la kwanza. Hiyo ni sawa na kusema wanafunzi takriban nane kwa kila 100 waliofanya mtihani huo ndiyo wamepata daraja la kwanza. 

“Watahiniwa 47,885 sawa na asilimia 7.65 wamefaulu kwa daraja la kwanza,” amesema Amasi.

Ufaulu wa wanafunzi waliopata daraja la kwanza umeshuka kwa asilimia 5.2 ukilinganisha na matokeo ya mwaka 2021 ambapo wanafunzi 75,770 sawa na asilimia 12.58 ya wanafunzi waliofanya mtihani walipata daraja hilo la dhahabu.

Watahiniwa 45,288 sawa na silimia 7.15 wamepata daraja la pili, huku watahiniwa 74,359 sawa na asilimia 11.74 wamepata daraja la tatu huku zaidi ya nusu (asilimia 58.74) ya watahiniwa wakiangukia daraja la nne.

Watahiniwa 93,892 sawa na asilimia 14.82 wameshika mkia kwenye matokeo hayo kwa kupata daraja sifuri.

Enable Notifications OK No thanks