Sayansi, hesabu zaendelea kuwaliza wanafunzi kidato cha pili 2022
- Somo la hesabu ndio lina ufaulu wa chini zaidi kuliko yote.
- Wanafunzi nane kati 10 waliofanya mtihani wamefeli.
- Baolojia, Fizikia na Kemia bado mambo magumu.
Dar es Salaam. Serikali na wadau wa elimu nchini Tanzania wataendelea kuwa na kibarua cha kutafuta mwarobaini wa kuongeza uelewa na ufaulu wa masomo ya sayansi na hesabu mara baada ya matokeo ya kidato cha pili kuonyesha ufaulu wa masomo hayo upo chini zaidi ya mengine.
Katika matokeo ya upimaji wa kitaifa ya kidato cha pili kwa mwaka 2022 yaliyotangazwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) Athumani Amasi, leo Januari 4, 2023 somo la hesabu ndio lina ufaulu wa chini zaidi kuliko masomo mengine baada ya wanafunzi nane kati ya 10 kufeli.
“Jumla ya wanafunzi 528,344 sawa na asilimia 83.44 ya watahiniwa wamepata daraja F (wamefeli) katika somo la Basic Mathematics (hesabu),” Amas amewaambia wanahabari jijini Dar es Salaam.
Huo ndio ufaulu wa chini zaidi katika masomo ya sayansi na hesabu ukifuatiwa na somo la Fizikia ambalo jumla ya wanafunzi 515, 734 sawa na asilimia 82 wamefeli.
Soma zaidi:
Kama yalivyo masomo mengine ya sayansi, zaidi ya nusu au asilimia 67 ya watahiniwa hao waliofanya mtihani wa Kemia Oktoba 2022 wamefeli. Hii ina maana kuwa takriban wanafunzi saba kati ya 10 wamefeli somo hilo muhimu katika kutafuta suluhu za kikemia kwa binadamu.
Pia mambo ni magumu katika somo la Baiolojia baada ya watahiniwa 335, 847 sawa na asilimia 53 au nusu ya waliofanya mtihani kufeli.
Kwa muda mrefu sasa wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari wamekuwa wakifeli vibaya masomo ya sayansi na hesabu jambo linalotishia mustakabali wa Tanzania katika kutumia vema fursa za maendeleo kupitia sayansi na teknolojia.
Miongoni mwa baadhi ya masuala ambayo wadau wa elimu wamekuwa wakiyapigia kelele kuongeza ufaulu wa masomo hayo ni kuondosha uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na hesabu nchini na kuongeza vitabu na zana nyingine za kufundishia.
Mwishoni mwa Septemba 2022 Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Esther Matiko alisema Serikali imeajiri asilimia 33 tu ya walimu waliohitimu masomo hayo katika vyuo mbalimbali. Hii ina maana kuwa ni mwalimu mmoja tu kati ya watatu wanaotakiwa kufundisha masomo hayo wameajiriwa na Serikali.
Katika kujibu hoja hiyo bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga aliliambia Bunge kuwa Serikali itaajiri zaidi ya walimu 40,000 ambapo kipaumbele kitakuwa kwa walimu wa masomo ya sayansi.
“Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) katika mwaka huu wa fedha imeshaomba kibali cha kuajiri walimu 42,697 kipaumbele kitakuwa walimu wa masomo ya Sayansi, Hisabati na wanaojitolea,” alisema Kipanga.