Rais wa Hungary kuzuru Tanzania kwa siku tatu

July 17, 2023 10:36 am · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Rais wa kwanza mwanamke kuongoza taifa hilo.
  • Atapokelewa na Rais Samia Ikulu ya Magogoni Julai 18, 2023.

Dar es Salaam. Rais wa Hungary Katalin Novák, anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini Tanzania kuanzia leo Julai 17 mpaka Julai 20, 2023 ambapo atapokelewa na kufanya mazungumzo na  Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan Julai 18, 2023.

Novák ni Rais wa kwanza mwanamke kuongoza nchi ya Hungary ambapo alichaguliwa mwezi Mei, 2022 akiwa na umri wa miaka 44 jambo ambalo limevunja rekodi katika historia ya nchi hiyo kupata Rais kijana.

Katarina Nuvak ni Rais wa kwanza kutoka Hungary kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania.

Zuhura Yunus, ambaye ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, aliyekuwa akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Julai 17 2023, amebainisha kuwa Tanzania na Hungary zimekuwa na mahusiano mazuri katika nyanja za diplomasia, uchumi, pamoja na kibiashara kuanzia miaka ya 1980 .

“Uhusiano kati ya Tanzania na Hungary umeshamiri zaidi katika sekta ya elimu ambapo baadhi ya Watanzania wamefadhiliwa kusoma shahada, shahada za uzamili pamoja na uzamivu katika masomo ya kimkakati ikiwemo Sayansi, Hisabati pamoja na Mawasiliano,” amesema Zuhura


Soma zaidi:


Mwaka 2020 zaidi ya Watanzania 30 walifadhiliwa kwenda kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini Hungary kwa muda wa miaka mitatu 2021/23.

Hii ni ziara ya pili ya kiongozi wa juu wa nchi kutoka nje ya Bara la Afrika, ikitanguliwa na ile iliyofanywa na Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris ambaye aliwasili nchini mwezi Machi 2023.

Wasemavyo wachambuzi

Richard Feruzi ambaye ni mchambuzi wa masuala ya diplomasia  ameiambia Nukta Habari kuwa ujio wa Rais wa Hungary inaweza kupanua fursa za ushirikiano wa kiuchumi wakati huu ambao Tanzania inatekeleza sera ya diplomasia ya uchumi.

“Serikali ya Tanzania inajaribu kuingia mikataba ya ushirikiano na baadhi ya mataifa yaliyoendelea, Hungary inatoka Bara la Ulaya ambalo limeendelea kwa vitu vingi kuliko nchi za Afrika hivyo Tanzania ina nafasi ya kunufaika na ushirikiano wa kibiashara au wa kimkakati,” amesema Feruzi.

Kwa mujibu wa tovuti ya takwimu za uchumi ya OEC mwaka 2021 bidhaa zilizosafirishwa kutoka Hungary kwenda nchini Tanzania zilikuwa na thamani ya Dola 15 milioni za Marekani sawa na Sh36.5 bilioni za Tanzania.

Tovuti hiyo imebainisha kuwa bidhaa zilizosafirishwa kutoka Tanzania kwenda Hungary  zina thamani ya Dola 759,000 sawa na Sh1.8 bilioni za Tanzania.

Mashine za viwandani ndio bidhaa zilizoingizwa zaidi nchini kutoka Hungary wakati Tanzania ilisafirisha zaidi tumbaku ghafi pamoja na malighafi zinazotumika kutengenezea vifaa vya kielektroniki.

Mchangano wa uingizaji na usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Hungary.PichalOEC

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW