Matukio makubwa yaliyotikisa Tanzania mwaka 2021
- Ni pamoja na kifo cha Rais John Magufuli na viongozi wengine wa kisiasa.
- Kuapishwa kwa Rais Samia kama Rais wa kwanza Mwanamke Tanzania.
- Tanzania yakubali chanjo ya Corona kwa mara ya kwanza.
Dar es Salaam. Kwa Watanzania wengi, mwaka 2021 haukuwa “easy” kwani kila mtu alikuwa na mapito yake. Wapo waliopoteza ndugu, ajira huku wengine fursa zikiwaponyoka.
Hata hivyo, Watanzania siyo watu wa kukata tamaa kwani licha ya mapito yaliyoambatana na mwaka 2021, waliamka, kukaza kamba za viatu vyao na kuendeleza mwendo.
Wakati kila Mtanzania akipitia lake, haya ni baadhi ya matukio makubwa ambayo huenda yatauweka mwaka 2021 kwenye kalenda za kumbukumbu za historia nchini.
Rais Dk John Magufuli afariki dunia
Haikuwa kitu ambacho kilitegemewa kwani hakukuwa na taarifa za wazi kuhusu ugonjwa wake lakini mshumaa ulizimika ghafla na kuacha simanzi kubwa Watanzania.
Machi 17 mwaka huu, Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan akiwa mkoani Tanga majira ya usiku alitangaza kifo cha Rais John Magufuli kutokana na matatizo ya moyo akiwa katika hospitali moja jijini Dar es Salaam.
Taarifa hiyo iliwashtua Watanzania kwa sababu walifikiri Hayati Magufuli angemalizia kipindi chake cha pili cha uongozi na kukamilisha mipango aliyokuwa nayo ikiwemo kuifanya Tanzania ya viwanda na miradi mkubwa kama reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na bwawa la kuzalisha umeme la Nyerere katika mto Rufiji.
Siku chache baada ya kifo chake, kuanzia Dar es Salaam, Zanzibar, Mwanza na hadi Chato mkoani Geita alipopumzishwa kwenye nyumba yake ya milele, maelfu ya watu walijipanga barabarani kuusindikiza mwili wake kama ishara kuwa alianza alama isiyofutika katika mioyo yao.
Viongozi waandamizi wafariki dunia kwa nyakati tofauti
Mbali na Hayati Magufuli, wapo viongozi wengine ambao walikuwa na ushawishi wa kisiasa kuanzia Tanzania Bara hadi visiwani ambao pia waliwaaga Watanzania mwaka huu.
Miongoni mwa vifo hivyo ni cha aliyekuwa Katibu Mkuu kiongozi, Balozi John Kijazi; aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho.
Waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, Balozi Bakari Mwapachu naye ameaga dunia kabla mwaka 2021 haujaisha.
Waziri wa zamani Ofisi ya Rais (Muungano na Mazingira), Dk Mohamed Seif Khatib; aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servecius Likwelile na Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Benno Ndulu.
Soma zaidi
- Namna ya kutokomeza matukio ya ubakaji Tanzania
- Unyanyasaji kingono: Jinamizi la afya ya akili
- Mambo ya kufanya wakati wa mapumziko ya mwisho wa mwaka
Tanzania yapata Rais wa kwanza mwanamke
Nchi ya Tanzania iliyopo Afrika Mashariki Machi 17, 2021 ilimteua Samia Suluhu Hassan kuwa rais wake wa kwanza mwanamke tangu ilipopata uhuru mwaka 1961.
Kabla ya kushika wadhifa huo, Rais Samia alikuwa Makamu wa Rais tangu 2015 katika Serikali ya awamu ya tano iliyokuwa inaongozwa na Hayati John Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 kutokana na matatizo ya moyo. Magufuli pia alikuwa rais wa kwanza kufariki akiwa madarakani Tanzania.
Samia ambaye atashikilia wadhifa wa urais kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa urais mpaka 2025, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania ameweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa juu zaidi nchini.
Aina ya kuchukua hatamu kwa Samia ambaye anakuwa rais wa pili wa Tanzania kutokea Zanzibar imetokea kwa mara ya kwanza, yaani kwa rais kufariki akiwa madarakani na makamu wake kuchukua nafasi.
Rais Samia aliapishwa rasmi siku mbili baada ya kifo cha hayati Dk Magufuli. Picha| DW.
Tanzania yakubali chanjo dhidi ya corona
Mnamo Julai 24mwaka huu, Tanzania ilipokea kwa mara ya kwanza dozi milioni 1.05 za chanjo aina ya Jassen inayotengenezwa na kampuni ya Johnson and Johnson ya nchini Marekani.
Hili ni tukio la kihistoria kwa Tanzania kwani chanjo hii ilikuja kama afua dhidi ya ugonjwa wa Corona ambao unaitesa dunia kwa sasa.
Chanjo hiyo ilizinduliwa na Rais Samia Agosti 3 ambaye aliwahakikishia Watanzania kuwa ni salama na kufuta mashaka ya mtangulizi wake Hayati Magufuli ambaye alionyesha kutokukubaliana na chanjo na kuwataka Watanzania wamtegemee Mungu katika mapambano ya ugonjwa huo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman mbowe akamatwa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe alikamatwa akiwa mkoani Mwanza akijiandaa kufanya kongamano la Katiba Mpya na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi, jambo ambalo limeibu gumzo kila mahali duniani.
Mbowe na wenzake Halfan Bwire Hassan, Abdillahi Ling’wenya, Adamu Hassan Kasekwa wanaokabiliwa na mashtaka sita yakiwemo ya kula njama ya kutenda kosa na kufadhili fedha kwa ajili ya vitendo vya ugaidi.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akishuka katika gari la Magereza kuhudhuria kesi yake mahakani. Picha| Habari Leo.
Unakumbuka tukio lipi ambalo hutalisahau mwaka 2021?
Latest