Rais Samia aeleza sababu ya panga pangua wizara ya habari  akiwaapisha viongozi wateule Zanzibar

December 10, 2024 3:17 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Asema mabadiliko hayo yatasaidia kukuza sekta ya teknolojia ua mawasiliano ikiwemo satelite na uchumi wa kidigitali
  • Awataka wateule kufanya kazi kwa bidii.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amewaapisha viongozi walioteuliwa katika nafasi mbalimbali huku akieleza sababu za kuipangua Wizara ya habari kutoka Wizara ya Habari ,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari hadi kwenda katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa ni kukuza wizara hizo kwa kasi.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza katika hafla ya kuwaapisha viongozi hao leo Disemba 10, 2024, katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar amesema Wizara hiyo imepelekwa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuruhusu ukuaji wa sekta ya mawasiliano na teknolojia hususan uchumi wa kidigitali.

“Tangu tumeanza wizara hii nimeona ‘concentration’ inaenda kwenye sekta ya habari na huku kwingine mnafanya vizuri lakini hatuendi kwa kasi ile ambayo inatakiwa tuende, nimewakopa habari nimepeleka kule ili ‘mconcentrate’ kwenye teknolojia ya habari,” amesema Rais Samia.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akimuapisha Profesa Palamagamba John kuwa Waziri wa  Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Picha/ Ikulu Mawasiliano.

Kwa mujibu wa Rais Samia kuitenga Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari kutasaidia kukuza mawasiliano ndani na nje ya nchi huku ikiimarisha Kampuni ya Simu (TTCL) pamoja na Shirika la Posta yajiendeshe kibiashara.

“Kuna kazi ya kutuunganisha sisi na nchi jirani kupitia mkonga ambao tumefanya kazi nzuri lakini bado tunatakiwa kuendelea kufanya kazi ndani ya nchi hapa tunazungumzia masuala ya satelite na hiyo ndiyo kazi kubwa sana…

…Nataka waziri na timu yako mkashughulike sana na mambo hayo na ndiyo maana habari nimeitoa kwenu nimeipeleka kwenye michezo, sanaa na mambo mengine.”amesema Rais Samia.

Kabla ya kuhamishiwa katika Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo sekta ya habari ilikuwa ikiunda Wizara ya Habari, Mawasiliano,Teknolojia ya Habari ikiongozwa na Waziri Jerry Silaa.

Kwa sasa sekta ya habari itakuwa chini ya wizara hiyo ikiongozwa na Waziri Prof. Palamagamba Kabudi ambaye awali alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.

Fanyeni kazi kwa bidii

Aidha, Rais Samia amewaagiza viongozi wote walioapishwa kila mmoja katika nafasi yake na eneo alopangiwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii huku wakizingatia wana mwaka mmoja wa kutimiza majukumu yao kabla ya kuachia madaraka.

“Nataka mkafanye kazi vizuri, mwaka huu ndio wa kuonyesha kwamba Serikali ipo na tunafanya kazi mkashirikiane na mtakao wakuta na mfanye kazi vizuri sio mlo hapa tu hata wengine mlioko hapa mmeanza ‘kurelax’ huko nendeni mkafanye kazi. Lindeni majimbo lakini nendeni mkafanye kazi,” amesema Rais Samia. 

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwaapisha viongozi wapya walioteuliwa leo wakiwemo Mawaziri na Mabalozi katika sekta mbalimbali Ikulu ndogo ya Tunguu Zanzibar. Picha / Ikulu Mawasiliano.

Rais Samia pia amewaagiza viongozi hao kila mmoja katika kitengo chake kuhakikisha anaenda kutataua changamoto zote zilizopo ili kuimarisha sekta walizopangiwa.

“Kwakua tunakwenda na kasi ya ukuaji wa Sekta ya mawasiliano na teknolojia si tu hapa ndani ya nchi lakini dunia nzima lakini pia kama mnavyojua tulikuja na mkakatiawa uchumi wa kidigitali ambao ukiutizama vizuri mkakati ule unataka shughuri ya peke yake..nimeona concertation kubwa inakwenda katika sekta ya habari na huku kwingine mnafanya vizuri lakini hatuendi na kasi ambayo inatakiwa,” amesema Rais Samia wakati akitoa maagizo.

Enable Notifications OK No thanks