Rais Samia: Kifo cha Membe kimeacha pengo kubwa

May 15, 2023 10:18 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na mchango wake katika kulinda utu na heshima ya mtu ndani na nje ya Tanzania. 
  • Mchango wake katika kukuza uhusiano wa kimataifa na ujirani mwema  kuenziwa na kukumbukwa. 
  • Rais Samia awapa pole wafiwa, asema msiba ni wa Watanzania wote.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kifo cha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Benard Membe, kimeacha pengo kubwa kwa familia, Watanzania na mataifa ya jirani aliyoyafanyia kazi ya kulinda utu pamoja na heshima ya mtu.

Rais Samia aliyekuwa akitoa salamu za rambirambi wakati wa  kuuaga mwili wa Membe leo Mei 14, 2023 amewaambia Watanzania kuwa kifo cha Membe kimewasikitisha watu wengi ndani na nje ya Tanzania kwa kuwa  alikuwa mtu mashuhuri na mwanadiplomasia mahiri.

“Ndugu Membe alikuwa mtu muungwana sana, mchapakazi na aliyependa maendeleo ya nchi na wananchi wake, si tu katika taifa lake bali hata mataifa mengine.., kifo chake kimeacha pengo kubwa sio tu katika familia, bali kwa Tanzania na mataifa ya jirani aliyoyafanyia kazi ya kulinda utu na heshima ya mtu,” amesema Rais Samia kwa huzuni.

Samia ameongeza kuwa, kwake yeye Membe alikuwa ni kaka wa karibu aliyependa kufundisha na  kutoa maarifa yake kwa wengine kwa kuwa  wamefanya kazi pamoja katika Baraza la Mawaziri pamoja na Halmashauri ya Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Zinazohusiana


Pamoja na hayo, Rais Samia ameungana na Watanzania wote kutoa salamu za rambirambi kwa wafiwa na wote walioguswa na msiba huo kwani umewagusa watu wengi ndani na nje ya Tanzania kutokana na umahiri wa Membe katika uga wa diplomasia.

“Msiba huu si wenu peke yenu ni wetu sote, ingawa athari na machungu ya msiba huu kitakuwa upande wenu…, kwa hakika nguzo kuu imeondoka ninamuomba Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na awape subra wafiwa wote katika kipindi hiki cha majonzi mnachopitia,”  amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Stergomena Tax amesema Membe alifanya kazi kubwa ya kukuza diplomasia kati ya Tanzania na mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa.

“Mchango wake katika kukuza uhusiano wa kimataifa na ujirani mwema kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali nje ya bara la Afrika utaendelea kubaki kama historia njema ya taifa letu, wizara hii imenufaika sana na utumishi uliotukuka wa Membe na tutaendelea kumkumbuka na kumuenzi,”  amesema Dk. Tax.

Shughuli ya kuuaga mwili wa Bernard Membe aliyefariki baada ya kuugua ghafla Mei 12, 2023 imefanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Tanzania, na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa.

Kwa mujibu wa ratiba rasmi iliyotolewa na familia ya Membe, ibada ya misa takatifu itafanyika kesho Mei 15, 2023 katika kanisa la Mtakatifu Joseph jijini Dar es Salaam kisha  mwili wake utasafirishwa kwenda Mkoani Lindi, kwa ajili ya maziko ambapo atazikwa Mei 16, 2023 kijijini kwao Rondo katika jimbo la Mtama.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...