Bernard Membe afariki dunia, Rais Samia, Watanzania wamlilia
- Rais Samia asema alikuwa na weledi katika kuitumia nchi.
- Watanzania nao wasema watamkumbuka kwa uzalendo wake.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na Watanzania kutoa salamu za pole kwa familia, ndugu na marafiki kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe.
Membe (69) aliyewahi pia kuwa mgombea Urais mwaka 2020 kwa tiketi ya Chama Cha ACT-Wazalendo amefariki leo asubuhi katika hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa Membe alipelekwa hospitalini hapo akisumbuliwa na maumivu ya kichwa.
Rais Samia kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Membe kwa sababu aliitumikia nchi kwa weledi katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi. Pole kwa familia, ndugu, jamaa & marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina. pic.twitter.com/tqN34ubqtC
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) May 12, 2023
Baadhi ya wanasiasa na wananchi wamejitokeza kuomboleza kifo cha Membe huku wakimuelezea kama mtu aliyelipenda Taifa lake. Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amesema hakuna maneno yanayoweza kueleza mshtuko mkubwa alioupata kufuatia taarifa ya msiba huo, zaidi ya kumshukuru Mungu kwa maisha ya Membe.
“Mwanasiasa mahiri, mwanadiplomasia maarufu na mwakilishi wa wananchi,” amesema Zitto katika ukurasa wake wa Twitter.
Amesema kwa niaba ya wanachama wa ACT Wazalendo ambao Membe aliwahi kuwa mwanachama mwenzao anatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi wote.
Naye Mwandishi wa habari, Ezekiel Kamwaga ambaye hivi karibuni alifanya mahojiano na marehemu amesema katika mazungumzo yao Membe alimjulisha kuwa anaandika kitabu cha utatuzi wa migogoro Afrika.
Hata hivyo, Kamwaga amesema hatasoma kitabu hicho kwa sababu membe amefariki dunia.
“Kitabu ambacho sitasoma Kwenye mazungumzo yangu marefu ya mwisho na @BenMembe alinieleza anaandika kitabu na alikipa jina la “The Politics of Conflicts and Conflicting Politics in Africa”,” amesema.
Soma zaidi:
Chadema watoa Salamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema Membe aliitumikia nchi katika ngazi mbalimbali na alikua hazina muhimu kwa Taifa.
“Raha ya milele umpe ee bwana, na mwanga wa milele umuangazia. Apumzike kwa amani,” amesema Mbowe katika ukurasa wake wa Twitter.
Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kifo cha Bernard Membe kimemhuzunisha akisema mwanasiasa huyo, alikuwa zaidi kaka yake licha ya tofauti za kisasa zilizopo kati yao.
“My Great friend Beard Membe RIP hata baada ya kuondoka utaendelea kuwa rafiki yangu.Bwana Yesu Bwana na Mwokozi wetu akusamehe dhambi zako akukaribishe kwake Mbinguni Amina,” amesema Charles Kazeze (@charles_kazeze), mtumiaji wa Twitter.
Mtumiaji mwingine wa mtandao wa Twitter, Ruwaichi Meela amesema atamkumbuka kwa utanashati wake na zungumza yake.
Membe Alihudumu katika nafasi ya Waziri wa Mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa kati ya mwaka 2007 hadi 2015, wakati wa uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Membe aliwahi pia kuwa Mbunge wa jimbo la Mtama, alikochaguliwa mwaka 2000 na kuhudumu hadi mwaka 2015.
Latest
