Mwanzo, mwisho wa Bernard Membe
- Amefariki leo asubuhi majira ya saa mbili katika hospitali ya Kairuki.
- Atakumbukwa kwa mchango wake katika kuimaridha diplomasia Tanzania na Afrika.
- Rais Samia amlilia, atuma salamu za rambirambi.
Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe amefariki dunia leo asubuhi katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa Membe alipata changamoto ya kifua na kupelekwa alfajiri ya leo hospitalini hapo na baadaye kufariki.
Kwa mujibu wa Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha hospitali ya Kairuki, Arafa Juba aliyeongea na gazeti la Mwananchi amethibitisha kuwa kifo hicho kimetokea majira ya saa mbili asubuhi.
“Ni kweli Membe aliletwa asubuhi hapa akapatiwa matibabu na wataalam kama ilivyo kawaida mgonjwa anapokuja hospitali, lakini Mungu alimpenda zaidi akafariki saa mbili asubuhi,” amesema Juba.
Membe amefariki akiwa na umri wa miaka 69, ambapo sababu ya kifo chake haijabainishwa wazi kutokana na taratibu za kitabibu kutoruhusu hilo.
Membe ni nani
Bernard Membe ni mwanasiasa na mwanadiplomasia mashuhuri nchini Tanzania na Barani Afrika ambaye amewahi kuhudumu katika nafasi kadhaa nyeti serikalini ikiwemo Idara ya Usalama wa Taifa, waziri wa Mambo ya Nje pamoja na kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.
Benard ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto saba wa familia ya mzee Kamillius Antony Chitakile na Cecilia John Membe ambapo alizaliwa Novemba 9, 1953 katika kijiji cha Rombo, Kata ya Chiponda mkoani Lindi.
Membe ametumikia nafasi mbalimbali ikiwemo Kamanda wa Vijana wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, na Katibu wa Sekretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama Cha Mapinduzi.
Zinazohusiana:
Amekuwa Mbunge wa Jimbo la Mtama kwa awamu tatu tofauti mpaka mwaka 2015, ambapo alichaguliwa kuwakilisha jimbo hilo kwa mara ya kwanza waka 2000.
Mwaka 2006 aliteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, ambapo Oktoba 2006 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini na kisha Januari 2007 akateuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa.
Membe alihudumu katika nafasi hiyo hadi 2015, akiwa ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi mfululizo, akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.
Akiwa katika wizara hiyo, Tanzania ilipata ugeni wa viongozi wakubwa duniani kama Rais George W. Bush mwaka 2008 na Baraka Obama (2013) wote wa Marekani,.
Wengine ni Xi Jinping wa China (2013) , Joachim Gauck wa Ujerumani (2015), Jacob Zuma wa Afrika Kusini (2014) , Mwana Mfalme wa Malkia (2011) wa Uingereza, na Mwana wa Mfalme wa Japan mwaka 2014.
Baadhi ya nyadhifa ambazo Membe amewahi kushika tangu mwaka 2006 ni pamoja na Mwenyekiti Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika, Addis Ababa, Ethiopia, Mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Katibu wa Sekretarieti ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa ya CCM pamoja na kuwa Mwenyekiti Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Bernard Membe (kulia) akionesha kadi yake ya uanachama wa CCM baada ya kukabishiwa na aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka katika kijiji cha Rondo, Mkoani Lindi. Picha l Salma Mkalibala/DW.
Kufukuzwa na kurejea ndani ya CCM
Februari 28, 2020 Membe alifukuzwa uanachama wa CCM na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya kwa kile kilichotajwa kuwa na mwenendo usiofaa ndani ya chama hicho.
Membe alijiunga na ACT-Wazalendo Julai 15, 2020 na kugombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho ambapo alipata akura 81,129 sawa na 0.5% ya kura zote.
Kauli maarufu ya Membe
Kauli maarufu inayokumbukwa kutoka kwa Membe ni ile aliyoitoa wakati wa harakati za uchaguzi mkuu mwaka 2020 akiwa visiwani Zanzibar ambapo aliwaambia wafuasi wa ACT kile atakachokifanya endapo atachaguliwa kuwa rais.
“Nikishaapishwa na kusaini wino wangu mwekundu pale, kwenye uwanja wa taifa jioni tutakuwa na tafrija lakini nasema tena siku inayofuata nitaagiza viongozi wote wa dini waliotoka Zanzibar wakaamishiwa kule watarudishwa hapa Zanzibar,”
Januari Mosi 2021 Membe alijiuzulu unachama wake ACT kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kilele cha mvutano kati yake na chama hicho baada ya kutofautiana na viongozi wenzake.
Machi 31, 2022 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, chama hicho kilitangaza kumpokea Membe na kumrejeshea uanachama wake baada ya kuandika barua za kuomba msamaha zaidi ya mara tatu ambapo alirejeshewa kadi yake Mei 29, 2022.
Aacha fidia ya Sh9 bilioni
Kutokana na kile alichokiita kuchafuliwa jina lake na gazeti la Tanzanite,Membe alifungua kesi mahakamani akimshtaki Mkurugenzi wa gazeti hilo Cyprian Musiba ambapo baada ya kushinda shauri hilo mahakama ilimuamuru Musiba kulipa zaidi ya Sh9 bilioni kama fidia.
Rais Samia atuma salamu za rambirambi
Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na Watanzania kutoa salamu za pole kwa familia, ndugu na marafiki kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe.
Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi. Pole kwa familia, ndugu, jamaa & marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina. pic.twitter.com/tqN34ubqtC
— Samia Suluhu (@SuluhuSamia) May 12, 2023
Latest



