Rais Magufuli amng’oa Kichere TRA, ateua waziri mpya wa viwanda
Aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda (kulia) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere ambao leo teuzi zao zimetenguliwa. Picha|Daniel Samson.
- Ametengua uteuzi wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere.
- Naibu Waziri wa Kilimo achukua nafasi ya Kichere ikichukuliwa na Edwini Mahede aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda.
- Uamuzi huo unakuja siku moja baada ya Rais Magufuli kukutana na wafanyabiasha Ikulu jijini Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Rais John Magufuli kukutana na wafanyabiashara, Ikulu Jijini Dar es Salaam ili kujadiliana changamoto mbalimbali za uendeshaji biashara nchini, leo ametengua uteuzi wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Juni 8, 2019) na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais Magufuli amemteua Innocent Bashungwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara ambapo anachukua nafasi ya Kakunda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
“Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Bashungwa alikuwa Naibu Waziri wa Kilimo,” inaeleza taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa.
Mabadiliko hayo katika Wizara ya Viwanda na Biashara yanakuja ikiwa imepita miezi zaidi ya sita tangu Rais Magufuli amfute kazi aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage kwa madai kuwa alishindwa kusimamia vizuri bei ya zao la korosho.
Bei ya korosho ilileta msuguano kati ya wakulima na wanunuzi binafsi kabla ya Serikali kuingilia kati na kuinunua korosho yote ya wakulima kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo.
Hata hivyo, mpaka leo baadhi ya wakulima hawajalipwa fedha zao, huku Serikali ikinukuliwa kwa nyakati tofauti kuwa “hakuna mkulima atakayedhulumiwa haki yake ya malipo ya korosho.”
Soma zaidi:
- Dk Mpango atoa onyo kali kwa watumishi TRA
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
- Serikali yatoa maagizo mazito kwa wanunuzi wa korosho
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage, joto la korosho likipanda
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Edwin Mahede kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye anachukua nafasi ya Kichere ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
“Kabla ya uteuzi huo, Mhede alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara. Uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara utafanywa baadaye,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Kufuatia uamuzi huo, Kichere ameteuliwa kuwa Katibu Tawala mkoa wa Njombe ambapo anachukua nafasi ya Erick Shitindi ambaye amestaafu.
Mabadiliko hayo yanakuja, baada ya wafanyabiashara waliokutana na Rais Magufuli jana kulalamikia mazingira magumu ya ufanyaji biashara nchini ikiwemo mlundikano wa kodi zisizoendana na hali halisi katika maeneo ya uzalishaji.
Mhe. Rais Magufuli atengua uteuzi wa Waziri wa Viwanda na Biashara na Kamishna Mkuu wa TRA. Afanya uteuzi wa nafasi hizo. pic.twitter.com/vUGrCMtY3R
— Gerson Msigwa (@MsigwaGerson) June 8, 2019