Prof Mkenda: Rasimu ya mabadiliko ya mitaala ya elimu imekamilika
- Yatakakuwa mabadiliko makubwa ya pili ya mtaala tangu mwaka 1960.
- Baada ya kupitishwa na Serikali rasimu hiyo itajadiliwa kwenye mjadala wa kitaifa kabla ya utekelezaji.
Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema rasimu ya mabadiliko ya mitaala ya elimu kuanzia elimu ya shule ya msingi mpaka chuo kikuu imekamilika ili ijadiliwe na kupitishwa kuendana na mazingira ya sasa ya elimu.
Waziri Mkenda aliyekuwa akizungumza katika mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam amesema rasimu hiyo ina mabadiliko makubwa yatakayokuwa na manufaa kwenye mfumo wa elimu ya Tanzania.
“Rasimu ya mapitio ya mitaala imekamilika na ina mabadiliko makubwa sana kwenye mfumo wa elimu, pengine makubwa sana kuliko yaliyowahi kutokea ndani ya nchi yetu,” amesema Waziri Mkenda.
Prof Mkenda amesema mabadiliko hayo yaliyofanyika kwenye mitaala ya elimu ni ya pili ambapo mabadilko ya kwanza yalifanyika mwaka 1960 wakati wa uongozi wa Rais wa kwanza Tanzania Mwalimu Julius Nyerere.
Mabadiliko hayo ya rasimu ya mtaala wa elimu yamefanyika na Kamati za Kitaifa za Maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo na Mitaala iliyoundwa na waziri huyo miezi michache iliyopita.
Pia rasimu hiyo imefanyiwa kazi na kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo maaskofu, mashekhe, walimu, wamiliki wa shule binafsi pamoja na wataalamu kutoka nje ya nchi ili kupata uzoefu kutoka katika nchi zilizoleta mageuzi ya elimu na kufanikiwa na zile ambazo hazikufanikiwa.
Soma zaidi
Mara baada ya rasimu hiyo kupitiwa na viongozi wa Serikali itawekwa mezani na kujadiliwa na wadau mbalimbali wa elimu na wananchi kupitia mjadala wa kitaifa wa mabadiliko ya rasimu ya mtaala huo utakaofanyika hivi karibuni.
Kwa muda sasa, kumekuwa na mjadala mpana kuhusu elimu ya Tanzania ambapo baadhi ya watu hasa wasomi wamekuwa wakipendekeza mitaala ifanyiwe marekebisho kuendana na mabadiliko ya sasa ya sayansi na teknolojia.
Hata hivyo, baadhi wamekuwa wakipendekeza mabadiliko yakifanyika yazingatie hali halisi ya nchi, tamaduni zake ili kuvifaidisha vizazi vya sasa na baadaye katika kujiletea maendeleo kutoka kwa wasomi wake.
Awali Rais Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akihutubia kwenye mahafali hayo amekipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kuanza kupitia mitaala yake ili kuhakikisha kinatoa elimu ujuzi.
Pia Rais Samia amevitaka vyuo vyote nchini kufanya mapitio ya mitaala yake kama ambavyo UDSM wanafanya ili kutoa ujuzi unaohitajika na jamii.
“Nichukue fursa hii pia kutoa rai kwa vyuo vingine vyote kuiga mfano wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa manufaa ya Taifa letu,” amesema Rais Samia.
Latest