Watoto wadogo katikati ya kuisaka elimu madarasa ya awali Tanzania-2
- Wataalamu wa saikolojia na wa elimu na makuzi ya watoto wanasema kumpeleka mtoto shule mapema kunadumaza akili.
- Mtaala mpya wa elimu ya awali watajwa kuwa suluhu
Dar es Salaam. Baada ya kuangazia namna hali ya uandikishwaji wa watoto wenye umri mdogo ilivyo nchini Tanzania, leo tunaangazia athari za kumpeleka mtoto shule akiwa kwenye umri mdogo pamoja na hatua za Serikali kutatua changamoto hiyo.
Kwa mujibu wa wanasaikolojia na wataalamu wa elimu na makuzi ya watoto, kumpeleka mtoto shule akiwa katika umri mdogo kunaweza kumsababishia akili yake kudumaa au kukataa kabisa kuendelea na shule siku za mbeleni
“Akili ya mtoto huwa inakuwa kwa hatua mbalimbali, kumuwahisha shule ni kama kuruka steji ya ukuaji wa mtoto, mwisho wa siku unakuta akili ya mtoto inadumaa au anachukia kabisa shule,” anasema Patrick Motto mwanasaikolojia kutoka Shirika la Brac Tanzania.
Mbali na kudumaa huko kwa akili, Motto anasema ikiwa mtoto atatumia muda mwingi shuleni na kukosa kabisa muda wa kucheza kutadumaza hata ukuaji wa mwili.
Naye Mwanasaikolojia Flolian Buhohela anasema mtoto aliye chini ya umri wa miaka mitatu anatakiwa kutumia muda mwingi akiwa na wazazi wake ili aweze kupata malezi, kujifunza maadili na tabia njema.
“Unapompeleka mtoto shule akiwa mdogo anaenda kujifunza tabia mpya ambazo hatuwezi kujihakikishia kwamba ni tabia njema au tabia mbaya ambazo pengine wazazi watashindwa kuzirekebisha hapo baadaye,” anasema Buhohela.
Mwanasaikolojia huyo anashauri kabla ya mtoto kupelekwa shule ni vyema mzazi, mlezi au mwalimu kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo uwezo wa kuelewa mambo, uwezo wa kuongea na kujifunza.
“Nashauri tuangalie hivyo vigezo na ikiwa mtoto anaweza kuvifanya kabla ya kuamua kumpeleka mtoto shule,” anasisitiza Buhohela.
Moja kati ya majukumu ya mzazi ni kuhakikisha elimu bora kwa mtoto wake . Picha Lucy Samson
Inaathiri afya ya akili
Mdau na mchambuzi wa masuala ya elimu Ayoub Mangi anasema kuna uwezekano mkubwa wa kudumaza akili ya mtoto pale anapowahishwa shule.
Mdau huyo anesema kinachomsaidia mtoto kuelewa darasani ni utayari na kukomaa kwa ubongo. Ukimlazimisha au kumuwahisha shuleni na akafundishwa vitu vikubwa kuliko uwezo wake akili hudumaa.
“Unashangaa mtoto anafika darasa la kwanza au la pili anaanza kushuka kimasomo na unajiuliza sababu ni nini kumbe ulimuwahisha mtoto shule wakati ambao haukutakiwa,” anasema Mangi.
Kimsingi mtoto wa miaka sifuri mpaka miaka minne huwa wanahitaji malezi ambayo yanalenga kujifunza mfano kucheza na udongo, au kutengeneza vifaa vidogo vidogo vya kuchezea.
Michezo hii inasaidia kukomaza mikono ya mtoto ili iwe rahisi kwake kushika kalamu au penseli wakati wa kuanza shule utakapofika na sio kusoma hesabu au kupewa kazi za nyumbani kama baadhi ya walimu wanavyofanya.
“Mtoto akianza mapema kusoma atakutana na matatizo makubwa mawili atachukia kusoma au atapata changamoto ya kusahau kile alichosoma,” anasema Mangi.
Mbali na hayo mchambuzi huyo anashauri ikiwa ni lazima sana mtoto kwenda shuleni chini ya umri wa miaka mitatu basi atumie muda mwingi kucheza kwa sababu michezo inaimarisha afya ya mwili na akili.
Soma zaidi
-
Watoto wadogo katikati ya kuisaka elimu madarasa ya awali Tanzania
- Yakufikirisha shule ya Twibhoki matokeo kidato cha nne 2022
Serikali tengenezeni mtaala mpya
Wadau wa elimu wanasema ili kuhakikisha utolewaji wa elimu bora itakayoendana na umri wa mtoto ni vyema Serikali kutengeneza mtaala mpya utakaoelekeza elimu wanayotakiwa kupewa watoto chini ya miaka mitatu.
“Wenye mamlaka ya kudhibiti vitu vinavyoendelea ni Wizara ya Elimu na Tamisemi kwa sababu wao ndiyo wenye dhamana basi waandae mitaala mipya itakayowezesha hawa watoto kuanzia mwaka mmoja na nusu kusoma,” anasema Dk Kimaro Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Mbali na mitaala hiyo wadau hao wa elimu wanashauri wazazi kuwawafundisha watoto wao nyumbani kuliko kuwaruhusu wakapate elimu iliyo juu ya uwezo wao.
“Kama nyumbani kuna mazingira wezeshi ni bora mtoto ajifunze nyumbani kama hatapata mazingira mazuri ya kujifunza, kulala na kucheza cheza wanaweza wakamuharibu kuliko kumjenga,” anaongeza Dk Kimaro.
Licha ya maoni ya wadau hao wa Elimu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imekwisha kujipanga kuboresha mtaala wa kujifunzia elimu ya awali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda katika hotuba ya bajeti ya wizara yake, mwaka wa fedha 2022/23 anasema Serikali inaendelea kukusanya maoni kuhusu mitaala inayotumika katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na ualimu kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu.