Mtaala wa elimu vyuoni utakavyobadili taswira ya ajira Tanzania
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda akiangalia vitabu na vitu mbalimbali wakati alipozindua maabara ya sayansi na tehama katika Chuo Cha Ualimu Butimba. Picha | Mariam John.
- Utawawezesha wahitimu kupata ujuzi wa kujiajiri na kuboresha maisha.
- Unaweza kuipunguzia Serikali mzigo wa ajira.
- Serikali yasema uko katika hatua za mwisho za uandaaji.
Mwanza. Serikali imesema iko katika hatua za mwisho za kupokea maoni ya mabadiliko ya mtaala wa elimu vyuoni utakaowawezesha wakufunzi na walimu kuwafundisha wanafunzi ujuzi wa ziada ili waweze kujitegemea baada ya kuhitimu masomo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali tayari imeshatenga bajeti ya kuboresha mtaala huo na utekelezaji wake utaanza mara baada ya kupokea maoni.
Prof Mkenda ambaye alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa majengo ya maabara za sayansi na Tehama katika Chuo cha Ualimu Butimba mkoani Mwanza amesema mtaala huo utakaojulikana kama mafunzo ya amali utaongeza ujuzi na vstadi muhimu kwa wahitimu.
Amesema mtaala huo utamsaidia mtu anapomaliza elimu ya chuo awe na uwezo wa kujiendeleza kimaisha bila kutegemea kuajiriwa moja kwa moja.
“Sisi tumeamua tutakuwa tunaita mafunzo ya amali, tuongeze mafunzo haya kwenye mitaala yetu maana yake tuongeze michezo, mziki, kilimo uvuvi, ufugaji, uselemala, ufundi uwashi na nguo ili pale mhitimu anapomaliza aweze kuchagua kuanza maisha yake,” amesema Mkenda.
Sehemu kubwa ya mabadiliko ya mtaala huo ni kuwaanda walimu na wakufunzi mahiri kufundisha ili wanafunzi watakapohitimu wapate maarifa na ujuzi uliokusudiwa.
“Kila mwaka wahitimu 11, 000 huhitimu idara ya elimu na hatuwezi kuwaajiri wote na kwenye sera mpya ya elimu ili uje upate ajira ya ualimu utatakiwa tena kufanya mtihani, utapigwa na kausaili, …ualimu lazima iwe ni moja ya sekta inayolindwa (one basic protective) kama tunavyoprotect madaktari,” amesema Profesa Mkenda.
Mkuu wa Chuo cha Ualimu Butimba, Nicholaus Magige amesema wakufunzi wapo tayari na mahiri na wote watatekeleza maboresho yoyote yanayotolewa katika mtaala na katika sera ya elimu.
“Wanafunzi wapo tayari pale yanapotokea mabadiliko wanashirikishwa na waweze kuona namna bora ya kuingia kwenye mfumo mpya na hata hayo mabadiliko kwenye mtaala ujao wakufunzi wapo tayari kuyapokea na kuanza kuyatekeleza,” amesema Magige.
Mratibu wa mradi wa kuendeleza elimu ya ualimu, Cosmas Mahenge amesema zaidi ya wakufunzi 1,300 waliopo kwenye vyuo 35 vya ualimu nchini wamekwishapatiwa mafunzo hayo ya aina mbalimbali yakiwemo ya masomo ya kufundishia na kitaaluma.
“Tumetoa mafunzo hayo hasa ukizingatia mtaala wa sasa umelenga kujenga umahiri kwa wanafunzi na kutumia mbinu shirikishi pia walimu hao wamepata mafunzo ya tehama,” amesema Mahenge.