Pikipiki zatajwa kuchangia uharibifu wa kamera simu za iPhone
- Ni pikipiki zenye Injini kubwa.
- Uharibifu huo unaweza kutokea kama kuna mtikisiko mkubwa.
- Inashauriwa kutoambatana na simu kwa muda mrefu wakati ukitumia pikipiki zenye injini za aina hiyo.
Dar es salaam. Usafiri wa pikipiki ni maarufu katika maeneo mbalimbali ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam. Usafiri huo unatajwa kuwa ni wa haraka na usiokuwa na foleni kama ilivyo kwa magari binafsi na hata daladala.
Licha ya umuhimu wa usafiri huo katika shughuli za kila siku, umetajwa kuwa na madhara kadhaa ikiwemo ya kuchangia matatizo ya macho na ajali za barabarani na kusababisha majeraha na vifo.
Hivi karibuni, Kampuni ya Apple ya nchini Marekani, Inayotengeneza simu za iPhone na kompyuta za Mac imeweka wazi kuwa kamera zake zinaweza kuathiriwa na matumizi ya usafiri wa pikipiki zenye injini kubwa.
Kupitia tovuti yake ya huduma kwa wateja, “Support” Apple imeandika kuwa mitikisiko inayotokana na injini kubwa ikiwemo za pikipiki inaweza kusababisha uharibifu wa kamera za iPhone kwa kudhoofisha baadhi ya mifumo yake maalumu kwa kung’amua picha tulivu.
“Mitikisiko ya juu hasa inayotokana na injini kubwa za pikipiki inaweza kushusha ubora wa mfumo wa kamera,” imeandika Apple.
Tahadhari hii haiwahusu wale wanaotumia pikipiki zenye injini ndogo zikiwemo za uememe, scooter na mopeds. Picha| Cycle World.
Hapa ndipo shida inapoanzia
Huenda bado unajiuliza inakuwaje hili jambo likawawezekana. Kwa mujibu wa Apple, simu za iPhone zimetengenezwa na mifumo ya kuweza kunasa picha tulivu hata pale simu inapokuwa haijatulia mfano mkono wa mpiga picha unatetemeka au mtu anapopiga picha ya kitu kilichopo kwenye mwendo kasi mfano gari, mnyama na hata mtu.
Mifumo hiyo, inajulikana kama “optical image stabilization (OIS)” inayofanya kazi ya kuondoa ukungu kwenye picha.
Mfumo mwingine ni “auto focus” (AF) ambayo inafanya kazi ya kuweka umakini kwenye kitu kinachopigwa picha ili kitokee kama kinavyoonekana.
Licha ya kuwa mifumo hiyo imetengenezwa ili idumu kwa muda mrefu, Apple imesema kuwa, pale simu inapokuwa imechangamana na mitikisiko mizito ya pikipiki inaweza kuharibu utendaji kazi wa mifumo hiyo na kusababisha kupungua kwa ubora wa picha na video zinazopigwa na simu hiyo.
Mbunifu wa grafiki na mpiga picha, Siganje Julius ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa mara nyingi Apple inatoa maonyo haya kwa watumiaji wa bidhaa zake ili kulinda ubora wa vitu vyake kwani pale mambo yanapoenda mrama kwa baadhi, huacha maoni kwenye mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha kuharibu soko la bidhaa zake.
TANGAZO:

Julius amesema kamera za simu za iPhone zinatumika na baadhi ya wadau wa uzalishaji wa video na wapiga picha kutengeneza maudhui kutokana na ubora wake.
Kwa ambao hutumia pikipiki kurekodi baadhi ya matukio kama riadha za magari, riadha za watu huenda ndiyo wakawa kwenye hatari ya kamera zao kuathirika zaidi.
“Apple wamesema hii ni kwa pikipiki ambazo ni kubwa ambazo mtu akipita nayo kwenye unasema kuna pikipiki imepita,” amesema Julius.
Kwa mujibu wa Apple, hali hiyo inaweza isiwasumbue watu wanaotumia pikipiki za umeme aina ya “mopeds” na “scooters”.
Latest
