Unayopaswa kuyafahamu kuhusu Google Pixel 9 series

August 22, 2024 6:42 pm · Hemed Suleman
Share
Tweet
Copy Link
  • Ina muonekano wa kishua, kioo chake kina upana wa hadi inchi 6.3 huku Pixel 9 Pro XL yenye inchi 6.8.
  • Simu hizo zitawafaa zaidi watengeneza maudhui na waandishi wa habari.

Dar es Salaam. Unatumia simu aina ya Google Pixel? Huenda ukahitaji kujisasisha na matoleo mapya ya simu hiyo yaliyoingizwa sokoni hivi karibuni.

Ni Google Pixel 9 series, iliyokuja na matoleo manne Pixel 9, Pixel 9 Pro, Pixel 9 Pro XL na Pixel 9 Pro Fold zitakazokufanya utambe katika ulimwengu wa simu janja na teknolojia siku zijazo.

Katika matoleo hayo mapya kuna mengi ya kuvutia ikiwemo teknolojia ya AI (Gemini AI) lakini pia teknolojia ya Tensor G4 itakayosaidia utendaji kazi na uhifadhi wa data kwa usalama zaidi.

Muonekano wa kishua

Kwa wale wanaopenda simu zenye muonekano wa kishua basi Google Pixel series 9 ndiyo yenyewe. Ina kioo angavu chenye upana wa hadi inchi 6.3 isipokuwa Pixel 9 Pro XL yenye inchi 6.8 na Pixel 9 Pro Fold ambayo ni simu ya kukunja pia kioo cha ndani kina kikubwa inchi 8 na cha nje inchi 6.3.

Ubora na upana wa kioo hicho umeongezeka kwa inchi 0.1 kulinganisha na toleo la Google Pixel 8 iliyokuwa na kioo chenye inchi 6.2.

Muonekano wa toleo jipya la Google Pixel 9 series.Picha| Android police.

Kamera kali ya kujidai na marafiki

Kuhusu ubora wa kamera Google Pixel hawajawahi kuyumba, toleo jipya la simu hiyo limekuja na kamera yenye ubora wa hadi Mega Pixel 50 kwa kamera ya nyuma na Megapixel 42 kwa kamera ya mbele ikiwawezesha watumiaji kutunza kumbukumbu za matukio kwa ubora wa hali ya juu.

Kwa upande wa Google Pixel Pro Fold yenyewe ina ubora wa Megapixel 48 kwa kamera ya nyuma na kamera ya mbele ni Megapixel 10.

Mwaka jana toleo la Google Pixel 8 na 8 Pro lilikuwa na kamera zenye Megapixel sawa kwa ubora wa Megapixel 50 kwa kamera ya nyuma na Mega Pixel 10.5 kwa kamera ya mbele.

Teknolojia ya Tensor G4 na uwezo wa simu kuhifadhi data

Tensor G4 ni processor (chip) mpya iliyotengenezwa na Google kwa ajili ya Google Pixel 9 series. Processor hii ni sehemu kuu ya uhifadhi wa taarifa za simu na ina jukumu muhimu katika kuboresha utendaji wa simu. 

Tensor G4 ni toleo la nne katika mfululizo wa (chips) za Tensor ambazo Google imezindua na inachukua hatua kubwa katika kuongeza uwezo wa akili bandia (AI) na utendaji wa vifaa vya Google Pixel.

Teknolojia hiyo iliyotengenezwa kwa kutumia teknolojia ya 4nm ina nguvu kubwa inayowezesha usindikaji wa data kwa kasi na utendaji bora huku zikiwa na Gigabyte 16 isipokuwa Pixel 9 ya kawaida yenye Gigabyte 12.

Toleo la Google Pixel 8 na Pixel 8 Pro, lilikuwa na Gigabyte 8 hiyo kwa Pixel 8 na Gigabyte 12 kwa Pixel 8 Pro.

Mohamed Mohamed muuzaji wa simu Ubungo Mawasiliano, jijini Dar  es Salaam amesema toleo jipya la Google Pixel limekuja kuleta ushindani sokoni kutokana na maboresho mengi yaliyofanyika.

“Google Pixel 9 imeletwa kwa malengo mahususi, kwanza mwanzo walikuwa wanasema Google Pixel zinaubora kwenye kamera tu …Kuleta teknolojia mpya kwenye Pixel 9 kutaleta ushindani mkubwa sana.” amesema Mohamed.

Watengeneza maudhui kunufaika zaidi

Watengeneza maudhui pamoja na waandishi wa habari ni miongoni mwa wanaotarajiwa kunufaika zaidi na maboresho mapya katika toleo jipya la Google Pixel.

Roben Philemon muuza simu Kariakoo, jijini Dar es Salaam amesema kuwa ubora wa kamera wa simu hizo utayafanya makundi hayo kuikimbilia zaidi simu hiyo kushinda aina nyingine ya simu.

“Google Pixel series 9, imelenga watu wote kwa sababu unaweza kutumia kwenye mazingira yoyote …ukiwa na simu leo mwandishi wa habari ninaamini hakutakuwa na haja ya kamera kubwa,” amesema Philemon.

Watengeneza maudhui kupitia hizo simu wataweza kupata picha zilizo nzuri kwa ajili ya maudhui yao na wataweza kubuni maudhui mengine kupitia akili bandia AI.

Hata hivyo, bado matoleo yote ya simu hizo hayajasambaa katika maeneo mengi barani Afrika na nchini Tanzania hali inayoibua sintofahamu miongoni mwa wahitaji wa simu hiyo nchini.

Kwa mujibu wa wauzaji wa simu jijini Dar es Salaam ni Google Pixel Pro XL pekee inayopatikana nchini licha ya kupita wiki moja tangu izinduliwe rasmi.

Kuhusu changamoto nyingine za simu hizo Philemon amesema bado ni mapema sana kuzigundua, inaweza kuchukua siku, miezi hata mwaka mpaka watu watakapoanza kuzilalamikia simu hizo.

Wanaotegemea simu zilizotumika (used) au zilizochakatwa upya (refubrished) huenda wakakutana na changamoto lukuki ikiwemo betri kuisha chaji mara kwa mara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks