Spiro yazindua pikipiki ya umeme kuchochea usafiri salama, nafuu Tanzania
- Betri ya pikipiki hiyo iliyochajiwa ina uwezo wa kutembea wastani wa kilomita 100 mpaka 130 ambapo gharama ya kuchaji ni Sh4,100.
Dar es Salaam. Kampuni ya kutengeneza pikipiki za umeme ya Spiro, imezindua rasmi bidhaa hiyo nchini Tanzania, ili kurahisisha upatikanaji wa usafiri salama kwa mazingira na gharama nafuu.
Upatikanaji wa bidhaa hiyo nchini huenda ukaleta ahueni ya panda shuka ya bei ya mafuta ambayo imekuwa ikiwaumiza wamiliki wa vyombo vya moto pamoja na madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda.
Ismail Insha, Meneja Mauzo wa Spiro Tanzania aliyekuwa akizungumza na wanahabari wakati wa uzinduzi wa pikipiki hiyo amewataka Watanzania kuichangamkia bidhaa hiyo kwa kuwa inautofauti na nyinginezo ikiwemo kupatikana kwa gharama nafuu na kuwa na waranti ya kila kifaa inapotokea uharibifu wa dharula.
“Tumeshaisambaza pikipiki hii kwa mawakala wetu hapa Dar es Salaam, wateja wataipata kwa Sh2,950,000 na bei hiyo inahusisha bima, usajili, kofia ngumu mbili, jaketi la upepo pamoja na kiakisi mwanga(reflector),” amesema Insha.
Insha ameongeza kuwa watumiaji wa pikipiki hiyo hawapaswi kuhofia kuhusu usalama wake kwa kuwa inakifaa maalumu cha kufuatilia (GPS) hivyo hata ikiibiwa ni rahisi kuifuatilia na mwizi hataweza kuitumia.
Mpaka sasa kampuni hiyo imefungua vituo sita vya kuchaji pikipiki hizo jijini Dar es Salaam ambapo kimoja kipo Tazara, Gongo la Mboto, Mbagala, Kigamboni, Bonyokwa pamoja na Kamata ambapo inakusudia kufungua vituo vingine katika maeneo ya Chanika na Tegeta kutegemeana na mahitaji.

Pamoja na kupungua kwa gharama za uendeshaji pikipiki hizo ni rafiki wa mazingira kwa kuwa hazizalishi hewa ukaa kama zile zinazotumia mafuta. Picha l Goodluck Gustaph/Nukta Africa
Umeme kiduchu, umbali mrefu
Afisa mauzo msaidizi kutoka Spiro, Antony Mtatiro ameiambia Nukta Habari kuwa betri ya pikipiki hiyo iliyochajiwa ina uwezo wa kutembea wastani wa kilomita 100 mpaka 130 ambapo gharama ya kuchaji ni Sh4,100.
Mtatiro anasema gharama hiyo ni nafuu kwa kuwa pikipiki inayotumia mafuta inahitaji lita tatu mpaka tano za mafuta kwa umbali wa kilomita 100 ambapo kwa bei ya sasa inaweza kufikia Sh14,735 ambapo lita moja ya mafuta ya petroli inauzwa Sh2,947 kwa mujibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Hata hivyo, pamoja na kupungua kwa gharama za uendeshaji pikipiki hizo ni rafiki wa mazingira kwa kuwa hazizalishi hewa ukaa kama zile zinazotumia mafuta.
Ni salama kwa mazingira
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Mkoa wa Dar es Salaam Michael Massawe amesema pikipiki hizo zimekuja wakati muafaka kwa kuwa sasa waendesha bodaboda wanaweza kuungana na ajenda ya ulimwengu ya kupunguza uchafizi wa mazingira unaochochea mabadiliko ya tabia ya nchi na athari zake.
“Tunasaidiana na kaulimbiu ya ulimwengu ya kutunza hewa, kwa kutozalisha uchafu wenye hewa ukaa, madereva wa pikipiki tumeipokea bidha hii, tunaifurahia, na tutaelimishana ili wote tuweze kuelewa umuhimu wake,” amesema Massawe.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA), pikipiki za magurudumu mawili na matatu zinachangia karibu nusu ya mauzo yote ya vyombo vya usafiri barani Afrika, hivyo vyombo vivyo kuwa vya umeme kunaweza kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na usafiri kwa hadi asilimia 30 katika miji yenye msongamano mkubwa ikiwemo Dar es Salaam.
Aidha, Spiro inakusudia kuifikisha bidhaa hiyo katika maeneo mengine ambapo kipaumbele kipo katika majiji ikiwemo Dodoma, Mwanza, Arusha pamoja na Mbeya.
Latest



