Piga moyo konde, pambazuko liko mbele yako
- Usikate tamaa kwa magumu unayopitia bala jipe moyo kuwa yatakwisha.
- Jielekeze katika kutimiza ndoto na mipango mizuri uliyojiwekea.
Dar es Salaam. Katika maisha kuna wakati unaweza kuhisi kuwa kila kitu unachofanya unakosea na unahitaji kuachana navyo ili ujipange upya.
Wapo wanaoamua kufunga biashara zao, wapo wanaoamua kuvunja mahusiano yao na wapo wanaoenda mbali na kuacha kufukuzia ndoto zao. Hicho ni kipindi cha giza la kimaisha na kihisia.
Hivi karibuni, sikuwa katika kipindi kizuri zaidi katika maisha yangu. Nilikuwa nikiwaza kama kweli uandishi wa habari ndiyo fungu langu, kama kuna haja ya kuendeleza biashara yangu za juisi au niachane nayo na kama huenda ndiyo muda wa mimi kuanza kufuata ndoto zangu kimuziki na mitindo au laa.
Ni wakati ambao ulikuwa umejaa mawazo. Niwe kwenye daladala, niwe kazini na hata wakati mwingine, ilifanya nishindwe kulala kabisa nibaki nikijigeuza geuza kitandani bila hata lepe la usingizi.
Kama nilivyosema awali, haukuwa muda mzuri zaidi kuwahi kutokea katika maisha yangu hasa nikiwa kijana ambaye huwa na furaha na kazi ambazo nazifanya.
Nilirudi vipi katika hali ya kawaida?
Haikuwa rahisi kupotezea mawazo hayo. Licha ya kwamba ilinilazimu kuendelea kuhudhuria kazini, kuendelea kutengeneza juisi na kufanya kazi zingine za kila siku lakini niliwaza mazuri yanayoendelea maishani ikilinganishwa na uhalisia.
Unahitaji muda wa kukaa pekee yako na kutafakari kuhusu maisha na mstakabali wa maisha yako. Picha| K15Photos.
Niliongea na watu ninaowaamini
Baada ya kuongea na rafiki zangu wa karibu na walezi wangu kitaaluma (mentors) walinifumbua macho kuona kuwa hakuna kazi wala kitu kinachokuja kiurahisi.
Rafiki yangu wa karibu sana ambaye jina lake nalihifadhi yeye alinishauri kuhusu kazi yangu ya uandishi ambayo ninaifanya. aliniambia, “kama unafikiri kuacha kazi, acha kazi tu pale unapoona kuwa kazi yako inaingilia biashara yako,” maneno haya yalipita hadi kwenye kiini cha moyo wangu.
Binti huyo alinishika bega akaniambia, “wewe ni mwandishi mzuri sana na ni kitu ambacho naona unakifanya vyema.” nilichukua muda wangu kuvimba kichwa kidogo na kisha kurudi katika uhalisia.
Rafiki yangu mwingine ambaye nimemuona wakati mwingine akifanya kazi hadi saa nane za usiku alishauri niwe mvumilivu kwani hata mji wa Roma haukujengwa kwa siku moja.
Aliniambia nitafute njia nzuri za kuifanya kazi yangu huku naifurahia ikiwa ni pamoja na kuifanya kwa wakati na kupata muda wa kupumzika.
Zinazohusiana:
- Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa
- Ndoa ndoano? Maswali lukuki kuhusu ndoa na jinsia
Nilipunguza muda wangu na simu
Kuna wakati nilihisi kuwa nimebaki nyuma sana na mambo yangu yanaenda taratibu sana na nilibaini kuwa ni kwa sababu nimekuwa nikikaa sana mtandaoni na kupata presha ya maisha kutoka kwa watu ambao ninawafahamu.
Kaka yangu wa karibu, Huyu namtaja bila haya, Daniel Mwingira aliniambia kuwa kwa sasa nikubali kujenga ujuzi wangu kwani sasa hivi nina muda wa kuwekeza katika kupata maarifa ambayo yatanipatia mafanikio baadaye.
Kaka yangu huyo aliniorodheshea mazuri ambayo yapo upande wangu na mazuri ambayo yanakuja huku akinipatia stori ya maisha yake ambayo ilinihamasisha hata mimi.
Baada ya hapo nilipunguza kukesha kwenye ‘status’ za watu na kurasa za mitandao ya kijamii na kuendelea na yanayonihusu. Niliona ambayo nilikuwa siyaoni ikiwemo uwezo wangu.
Matumaini ya kupambazuka
Safari ya maisha ninapenda kuifananisha na namna muenendo wa siku nzima ulivyo. Magumu yote nayafananisha na giza na mazuri nayafananisha na mchana / mwangaza.
Kuna kipindi ambacho giza litaingia maishani kiasi cha kutaka kukata tamaa lakini pale unapofikia katika hatua hiyo, kumbuka kuwa giza hilo ni mpito.
Tumia giza hilo kujifunza, kujipanga na kuwekeza katika uwezo wako ili jua na mwangaza vinapokuja vikukute tayari una uwezo wa kuvipokea.
Sali kwa muumba wako, weka juhudi zako na kisha chapa kazi ili Mungu anapokubariki iwepo sehemu ya kukubarikia. Iwe ni kazi, kipaji, biashara na hata elimu yako.
Usingojee baraka huku ukiwa haufanyi kitu. Zitapitia wapi hizo baraka?
Hadi wiki ijayo, Wako katika mapendo, Rodjazz
Latest
