Ufanye nini unapokuwa katika njiapanda ya kikazi?

April 15, 2021 6:40 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Licha ya kuwa baadhi ya vijana wamepata elimu hadi ngazi ya chuo kikuu, wengine hawana furaha na kazi wanazozifanya.
  • Hiyo husababishwa na mambo kadha wa kadha ikiwemo kutokupata muda wa mapumziko na kukosa hamasa.
  • Kuepukana na hilo, inashauriwa kuyafanya mazingira ya kazi yako kuwa rafiki au kufanya kitu unachokipenda.

Dar es Salaam. Hivi karibuni nilipata muda wa kukutana na jamaa zangu ambao huenda majukumu na maisha yalitufanya tusipate muda wa kuwa karibu mara kwa mara kama zamani. 

Licha ya kuwa tulipata wasaa mzuri pamoja baadhi yao hawakuweza kuvumilia kuzisema changamoto ambazo wamekuwa wakizipitia ikiwemo “kuwamba” na njia panda ya maisha.

Siyo kwamba hawana taaluma, wote ni wahitimu wa chuo. Wengine wamesomea sheria, wengine wamesomea usimamizi wa rasilimali watu na wengine ni wanahabari kama mimi na wengine wameamua kufanya biashara.

Hata hivyo bado, wanahisi kuna kitu kinapungua katika maisha yao. Wanahisi kitu wanachokifanya hakitoshi kuwafanya wafikie ndoto zao za kimaendeleo ikiwemo kununua viwanja, gari na kumiliki mali zifaazo hata kuanzisha familia.

“Nina miaka 26 sasa hivi hata kiwanja sina, nikiangalia kazi yangu, huenda ikanichukua miaka 1,000 kufikia ndoto zangu,” alisema mmoja wa rafiki zangu katika mazungumzo hayo. 

Kwa kulitazama hilo kama changamoto, huenda dondoo hizi ambazo tulizijadili na kushauriana zikakusaidia hata wewe ambaye unasoma makala hii:

Endapo kuna kitu ambacho unapenda kufanya na una uhakika ndiyo furaha yako, siyo mbaya ukaachana na kazi usiyoipenda na kufanya kitu unachokipenda. Picha| Poornima University.

Panua wigo wako wa vyanzo vya kipato

Pengine umeajiriwa na huenda kazi yako haikulipi kama ulivyotarajia ulipokuwa chuoni. Kuwa na matarajio siyo dhambi lakini pale yanapogeuka kuwa tofauti na ualisia, unahitaji kutafuta njia mbadala za kuyafikia matarajio yako.

Mathalan huenda unaendesha akaunti zako za kijamii kwa maisha binafsi. Badala ya kuzitumia kwa kuonyesha maisha yako, unaweza kuanza kuzitumia kwa kufanya biashara katika muda ambao haupo kazini.

Zipo biashara ndogo ndogo kama kuuza nguo, manukato na kadhalika ambavyo havihitaji mambo mengi sana bali muda mchache.

Endapo una pesa, usiziache zikajazana katika akaunti yako ya benki, tafuta mshauri wa uwekezaji na kisha uziwekeze ili zitengeneze pesa nyingi zaidi.

Chukua likizo kwa ajili ya kujipanga

Mara nyingine, huenda unaona kazi yako haifai kwa sababu umeifanya mfululizo bila kupumzika hivyo unaiona kama inakutesa. 

Kama una hali hiyo, unaweza kuchukua likizo ya muda mfupi ili upumzishe akili na kuona maisha bila kazi hiyo yanavyokuwa.

Pengine ni mazingira ya kazi ndiyo yanakufanya uone kazi yako inakuchosha au haikufai hivyo ukiyabadili kidogo, hali inaweza kuwa sawa.


Soma zaidi:


Yafanye mazingira yako ya kazi kuwa mazuri

Kama unatumia saa nane na zaidi ofisini au kazini, unahitaji kufanya mazingira hayo kuwa rafiki kwako ili ujisikie vyema na huru kuwa katika mazingira hayo.

Weka meza yako sawa, hakikisha unapata chakula kizuri. Pia weka picha za uwapendao katika meza yako zinaweza kukupa ari ya kufanya kazi.

Mfano endapo ukiweka picha ya familia yako, kila ukiwatazama utapata ari ya kufanya kazi kwani utayaelewa majukumu uliyo nayo.

Fanya maamuzi magumu

Wakati mwingine umekuwa daktari kwa ajili ya kufurahisha wazazi wako lakini taaluma hiyo siyo kitu kinachokufanya uwe na furaha maishani. 

Kutokufurahia kazi yako ni chanzo cha kutokuifanya kwa ufanisi na kuwa na makosa ya hapa na pale ya kiutendaji.

Endapo kuna kitu ambacho unapenda kufanya na una uhakika ndiyo furaha yako, siyo mbaya ukaachana na kazi usiyoipenda na kufanya kitu unachokipenda.

Ni matumaini yangu umepata masuala mawili matatu ya kujifunza kupitia makala hii. Endapo utakuwa wa swali au dukuduku lolote, nifikie kupitia +255 677 088 088. 

Enable Notifications OK No thanks