Ndoa ndoano? Maswali lukuki kuhusu ndoa na jinsia
Kabla ya kufundwa unyagoni. Nilijifunza kuhusu jinsia, jinsi utofauti kati ya msichana na mvulana ulivyo taji na tajiri. Nilidhani mvulana ni yule anavaa kaptura na msichana ni yule anavaa gauni, tayari na hiari kwa kuolewa.
Ilikuwa ni akili mbovu na pofu. Sikuona kwamba, mwanadamu ni zaidi ya kuoa na kuolewa. Kuna kuona na kutazama. Kutazama ni hulka ya kibiologia, ila kuona ni maamuzi.
Wengi hatupendi kuona, “because it compromise” yaani huleta muafaka usioridhisha. Macho pamoja na kuona yana kazi ya kutoa machozi. Eti, utasikia: “mwanaume hatoi machozi, kivipi, wakati kila kitu maishani ni mapenzi? Kwa kweli, jamii inatuchanganya!
Na pia nilipaliwa na swali lingine: jinsi ya kujua jinsia ya mimea na wanyama, ambao hawavai suruali wala sketi? Utofauti wa jogoo na tetea, ulionekana machoni na jogoo ndiye aliwika. Fikra zangu kuhusu ndoa na mahusiano zilikuwa za vitu kama suti, gauni jeupe, maua kwa mke. Mume “mkamilifu” na wife material! (Mke mwema).
Namna gani naweza kutambua kama paka ni jike au dume?
Alasiri moja, tumeketi uvulini mimi, baba na mama, tunachapa soga basi nikatumia ile nafsi kuuliza swali.
Baba, namna gani naweza kutambua kama paka ni jike au (na) dume? Niliuliza.
Mama alikaza uso na kutoa sauti kavu. “Isaac, hapana! Isaac, hapana”. Bado, nakumbuka vizuri sana!
Baba alicheka kwa ulimi na meno, akajibu. “Ni rahisi, paka dume ndiye mwindaji na jike ndiye mtunza watoto”. Kila fikra zina nyakati zake, sasa sio hivyo, leo hii mke anaweza kuwinda na baba akatunza watoto na kupika iwapo tukutumia msingi wa maneno ya baba ya kutofautisha jinsia ya paka kutokana na majukumu yao.
Nilikubali maelezo ya baba bila kuamini, kwa sababu ule uso na sauti ya mama ulinena kwa sauti zaidi kuwa nilikuwa nakanyaga ardhi katazwa.
Baadae sana, katika kuwaza na kuwazua, nilitambua kuwa mama alijibu vile, ili kuninusuru, labda baba angeweza kunifokea kwa sababu ya maswali.
Na kama baba angesema ukweli wa tofauti hizo, mimi ningeweza kuhitimisha kilojikia kwa kupinga mtizamo na mfumo dume, unaodumisha jamii kwamba mwanamke ni dhaifu, ajifunze kupika ili aolewe, na mwanaume daima ni shupavu, this is toxic masculine (Hii ni sumu kali ya kidume dume). Mafao na mafanikio ya mwanamke ni zaidi ya kuolewa. Heshima yake isifungwe katika kuwa na pete kidoleni.
Naam, upeo na maono yangu kuhusu mapenzi ulikaribiana na yale niliyaona kati ya jogoo na tetea. Bado nilitatizwa na kushangazwa na hali ya jogoo kumfukuzia tetea aliyejitetea kwa kukimbia. Bado jogoo alimkamata na kumpanda juu. Baada ya muwasho wa maswali, ilibidi nimfate tena mzee, safari hii akiwa pekee yake. Nilimbandika swali, kwa nini majogoo walifanya kitendo kile cha ushamba na kinyama?
Mzee alijibu kwamba kile kitendo cha jogoo kumpanda tetea ni adhabu kwa kosa ambalo tetea ametenda. Sikuelewa, ila nilipandwa na chuki. Jibu lake lilinifunulia wito wangu; kutetea haki za wanyonge. Kutoka siku ile, jogoo walinikoma kwa mawe na manati.
Miaka 30 kwa mwanamke si “expire date”
Jamii imewajaza wanawake uoga katika kudai haki na mbaya zaidi ukiziwi katika kulaani vitendo vya kikatili batili.
Jamii hiyo hiyo pia imefanya wanawake kujiona wamefikia “expire date” kwa Kiingereza yaani umri wao umefikia magharibi ama “mitumba” wanapofikia umri kama miaka 30.
Utasikia kauli kama “yeyote atakayekuja sasa naolewa naye” bila hata kuangalia kama mnapendana kweli. Kumbuka, mtu anaweza kuwa mpenzi wako, lakini akawa hatoshi kuwa mke/mume na mama/baba wa watoto wako. Imefika wakati watu waachwe wafanye uamuzi wao juu ya nani awe mwenza wao wa maisha bila kujali umri.
Vipi kuhusu wale waficha mimba kwa aibu?
Siku nyingine tena, nilikuwa na mama mtaani. Ghafla niliona mwanamke pembeni anahangaika na kuteseka, alikuwa anaficha tumbo la ujauzito kwa aibu (mie nilifikiri ni kitambi cha kawaida). Nilichomoza jicho la pili na kusema: “mama ona tumbo la yule mwanamke……”
Kabla sijamaliza sentensi, mama alinikatiza. Labda, sikuruhusiwa kuongea vile wala kutaja “mwanamke mjamzito. Ndio, tuliambiwa tusiseme “mwanamke anajifungua” bali ni “mgonjwa tu”. Hi ni moja tu ya mambo ambayo vijana wa kiume tulifichwa kuhusu watoto wa kike.
Wazo mjarabu na mtambuka hapa ni kwamba toka enzi, iwe nyumbani au shuleni ilikuwa nadra sana kushirikishwa mambo ya wasichana kama vile hedhi na pedi, ukeketaji, masuala ya uzazi, mimba na ndoa za utotoni…hii ilikuwa ni miiko.
Nakumbuka mama alinikataza kusimama na kuongea na wasichana. Dada alipofikisha umri fulani, aliulizwa kwa nini haolewi, lakini hilo hilo swali halikuelekezwa kwa kaka. Msichana ilibidi ajilinde asipoteze ubikira kabla ya ndoa na kuwa mke mwema. Hayo yote yalinichanganya!
Hapana shaka ukosefu wa ushirikishwaji wa wavulana tangu mwanzo kwa kiasi fulani kunachangia kufumbia macho visa na mikasa katili kila uchao katika jamii zetu. Tuungane kukemea, lakini zaidi kuelimishana.
Kutokuolewa sio doa
Jaribu kufikiria mwanamke kama hana watoto na hajaolewa anadharauliwa na kuitwa majina ya ajabu ajabu. Eti, mwanamke anapokuwa amefanikiwa na kujitegemea, anaambiwa asijioneshe sana atakosa mume. Mambo mengi yasiyofaa kama kudhalilisha wanamke, kuzuia msichana asirudi shule kisa mimba, ukeketaji, yanafichwa nyuma ya pazia la “kulinda mila.”
Fikra hizi ni sumu. Ndio maana, sishangai leo hii, tunachangishana michango zaidi watu kuolewa na kuoa kuliko kusomesha au kufungua biashara. Sherehe ya ndoa inapewa maana kuliko ibada yake. Kumbuka, kamati ya maisha ya ndoa ni muhimu kuliko ile ya sherehe. Tujisahihishe!
Katika moja ya semina nilizohudhuria, mtoa mada alisema kuwa: “Kuoana kuna masharti yake kama; kujimudu na kujitambua vizuri. Ndoa ni maagano sio mkataba”.
Ndoa si utani wala ushikaji wa kawaida. Jamii isiwalazimishe watu kuingia kwenye ndoa bila uamuzi wao binafsi. Picha|psych2go.net.
Kwa mana hiyo ya ndoa, nafikiri hata tendo la ndoa pia ni zaidi ya kukutana kimwili, ni zaidi ya mikuno na kukata viuno ambavyo baadhi yetu hufundishwa unyagoni. Ndoa ni jinsi ya ndani kabisa ya kuonesha upendo. Upendo pekee pia katika ndoa zama hizi hautoshi, lazima kuinuana kiuchumi na kimakuzi.
Mambo mengi yasiyofaa kama kudhalilisha mwanamke, kuzuia msichana kurudi shule kisa mimba, ukeketaji, yanafichwa nyuma ya pazia la “kulinda mila”. Na upendo pekee katika ndoa hautoshi, lazima kuinuana kiuchumi na kimakuzi.
Ndoa (kutokuolewa) sio doa, hakumpungizii mtu utu na heshima yake. Hata lugha zetu tuzibadilishe, “sio mume anaoa na mwanamke anaolewa” bali wanaoana. Ndoa inapogeuka ndoano ya kukabana koo haifai. Wakati mwingine, ni sawa to kukubaliana kutokukubaliana na kuheshimu tofauti zenu.
Picha ya mbele|psych2go.net.