OPEC kujadili kupanda bei ya petroli duniani leo
- Watajadili namna ya kuongeza mafuta yanayopelekwa sokoni.
- Hatua hiyo itasaidia kushusha bei ya mafuta duniani.
- Kwa sasa mafuta yanauzwa Dola za Marekani 80 (Sh184,487) kwa pipa.
Dar es Salaam. Wakati bei ya mafuta ya petroli na dizeli ikiendelea kuwa juu, Shirika la nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) pamoja na washirika wake watakutana leo kujadili kuongeza kiwango cha mafuta wanachopeleka katika soko dunia.
Licha ya juhudi mbalimbali za kukabiliana na athari za janga la Corona katika sekta ya mafuta, bei ya bidhaa hiyo bado iko juu ambapo kwa sasa inauzwa kwa Dola za Marekani 80 (Sh184,487) kwa pipa.
Bei ya mafuta imekuwa juu kwa miaka mitatu na imechangiwa pia na ongezeko la bei ya gesi iliyofikia asilimia 300 huku pipa moja ya bidhaa hiyo ikiuzwa kwa dola 200 (Sh461,000) kutokana na usambazaji mdogo na kiwango cha chini cha uzalishaji wa mafuta.
Mwezi Julai mwaka huu, OPEC na washirika wake ikiwemo Urusi walikubaliana kuongeza kiwango cha mafuta kufikia mapipa 400,000 kwa siku kila mwezi hadi Aprili mwaka 2022.
Hatua hiyo ya kuongeza uzalishaji imechochewa na baadhi ya nchi zikitaka kupunguzwa kwa bei ya mafuta kwa sababu mahitaji ya bidhaa hiyo yamerejea katika hali ya kawaida kuliko ilivyotarajiwa katika maeneo mbalimbali duniani.
Huenda ongezeko la kiwango cha mafuta kinachopelekwa sokoni kikaanza mwezi Novemba baada ya mkutano wa leo.
Ikiwa hilo litafanikiwa litasaidia kupunguza bei yamafuta hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ambazo zimeathirika zaidi na mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.
Serikali ya Tanzania ilisitisha bei za mafuta zilizotakiwa kuanza kutumika Septemba 1, 2021 na kuunda timu ya kuchunguza na kuangalia viashiria vinavyofanya kupanda kwa bei.
Hatua hiyo ni baada ya bei kupanda na kubaini kuwa itaendelea kupanda, hivyo Serikali iliamua kuchukua hatua ya kusitisha ili bei zilizokuwa zinatumika mwezi Agosti ziendelee kutumika.
Viwango tofauti vya mafuta vilivyopanda kwa mwezi Septemba kutoka bandari ya Dar es Salaam, petroli ilipanda kwa Sh84, dizeli 29 wakati mafuta ya taa bei ikiongezeka kwa sh18.
“Bandari ya Tanga petroli iliongezeka kwa Sh53, dizeli 14 na bandari ya Mtwara, petroli iliongezeka Sh108 na dizeli Sh46. Hata hivyo, bei hizo hazikutumika kama ilivyoelekezwa.
Latest