Ahueni: Rais Samia aagiza tozo za mafuta kupunguzwa Tanzania
- Ni zile zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta.
- Tozo hizo zina thamani ya Sh102 bilioni.
- Hatua hiyo itawapa unafuu wananchi wanaotumia nishati hizo.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu ameagiza kupunguzwa kwa tozo zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta zenye thamani ya Sh102 bilioni kwa mwaka ili kupunguza bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini Tanzania.
Hatua hiyo itawapa unafuu wananchi wanaotumia nishati hizo kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuendesha magari.
Taasisi zinazoguswa na maelekezo ya kupunguzwa kwa tozo hizo ni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ambayo imepunguziwa tozo ya udhibiti, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) (tozo ya miundombinu) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tozo ya kuchakata taarifa.
Nyingine ni Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imepunguziwa tozo ya kupima ubora wa mafuta kwenye meli na gharama ya uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta, Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) (tozo ya uhakiki wa ujazo wa mafuta melini), Wakala wa Usimamizi wa Meli (TASAC) (tozo ya forodha) na Mamlaka ya Serikali za Mitaa imepunguziwa ushuru wa huduma kwenye halmashauri nne zenye maghala ya kupokea mafuta kwa jumla.
Halmashauri hizo ni Kigamboni na Temeke za Jijini Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Oktoba 5, 2021 wakati akipokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa wizara hiyo kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.
Serikali ilielekeza EWURA kusitisha bei mpya za mafuta zilizopaswa kuanza kutumika Septemba 1 mwaka huu na zile ambazo zilikuwa zinatumika mwezi Agosti ziendelee kutumika na kuunda tume maalum kwa ajili ya kuangalia bei zinavyopangwa na viashiria mbalimbali vinavyosababisha bei iendelee kupanda.
Utekelezaji wa maagizo ya Rais umeenda sambamba na marekebisho ya kanuni mbalimbali zinazohusiana na tozo na zitachapishwa katika Gazeti la Serikali leo Oktoba 5, 2021.
Rais Samia amechukua hatua hiyo ili kukabiliana na upandaji wa bei za mafuta katika soko la dunia ambapo kwa muda mrefu imekuwa ikipanda kwa kiwango kikubwa na kuathiri watumiaji wa bidhaa hiyo hapa nchini.
Hadi kufikia Septemba 4, pipa moja la mafuta lilikuwa linauzwa kwa Dola za Marekani 80 (Sh184,487) katika soko la dunia.
Jana Shirika la nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani (OPEC) pamoja na washirika wake walikutana kujadili kuongeza kiwango cha mafuta wanachopeleka katika soko dunia hadi kufikia mapipa 400,000 kwa siku kila mwezi hadi Aprili mwaka 2022.
Ikiwa hilo litafanikiwa litasaidia kupunguza bei ya mafuta hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ambazo zimeathirika zaidi na mabadiliko ya bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.
Aidha, Rais Samia ameagiza ufanyike mchakato wa kuzifanyia marekebisho sheria nyingine zinazohitaji marekebisho ili kumlinda Mtanzania na gharama za maisha zinazotokana na kupanda kwa bei ya mafuta.
Muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano huo, Waziri Makamba amesema watayafanyia kazi maagizo yote ya Rais.
Tumepokea maelekezo ya Mhe Rais na leo tuta-gazette upunguzaji wa tozo nane za Serikali zinazochangia kwenye bei za mafuta ili kupunguza makali ya ongezeko la bei za mafuta duniani. Kuanzia kesho, taasisi kadhaa zitaacha kukusanya jumla ya bilioni 101 ili kutoa nafuu kwa wananchi https://t.co/qGMxuKVRSC
— January Makamba (@JMakamba) October 5, 2021
Latest
