Hizi ndio hifadhi tano kubwa za Taifa Tanzania
- Ni pamoja na hifadhi ya Nyerere, Ruaha na Serengeti.
- Mwaka 2022 hifadhi hizo zilitembelewa na jumla ya watalii milioni 1.4.
Dar es Salaam.Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo yamebarikiwa vivutio vingi vya utalii ambavyo sio tu vinapendezesha nchi bali ni chanzo kizuri cha mapato hususani fedha za kigeni ambazo hutumika kwa shughuli za maendeleo.
Tovuti ya runinga ya Tanzania Safari Channel ambayo hutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, inabainisha kuwa Asilimia 40 ya ardhi ya Tanzania imetengwa kwa ajili ya uhifadhi.
Hii inajumuisha hifadhi za Taifa 22, eneo la hifadhi ya Ngorongoro, mapori tengefu, hifadhi za misitu asilia na misitu ya kupandwa, maeneo ya kihistoria pamoja na hifadhi za bahari.
Maeneo yote hayo ndio kitovu kikubwa cha utalii nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2022, kinachotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) hifadhi za taifa ni moja kati ya vivutio vilivyotembelewa zaidi na watalii wa ndani na nje ya nchi.
Mwaka 2022 hifadhi hizo zilitembelewa na jumla ya watalii milioni 1.4 kati yao watalii 787,742 walitoka ndani ya nchi na watalii 697,264 kutoka mataifa mengine yaliyopo nje ya nchi.
Huenda wewe ni miongoni mwa watu wanaofahamu kuhusu uwepo wa hifadhi hizi lakini hujui ni ipi inaongoza kwa ukubwa, inapatikana wapi, na gharama za kufika huko.
Makala hii imeorodhesha hifadhi tano ambazo ndio kubwa zaidi nchini Tanzania pamoja na aina ya vivutio utakavyokutana navyo.
Watalii wakitazama mbwa mwitu katika hifadhi ya taifa ya Nyerere.Picha|Lake Manze Camp.
1.Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
Hifadhi hii sio kongwe sana, ilianzishwa mwaka 2019 baada ya kumegwa kutoka sehemu ya pori la akiba la Selous inayopatikana nyanda za juu kusini katika mikoa ya lindi na Ruvuma.
Hii ndio hifadhi kubwa zaidi barani Afrika, ikiwa na kilomita za mraba 30,893 ambapo ilipewa jina hilo ili kumuenzi muasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mbali na mandhari nzuri na mazingira tulivu yaliyopo katika hifadhi hii, utajionea wanyama wakubwa ‘The big five’(tembo, simba, nyati, kifaru na chui) pamoja na aina adimu za swala akiwemo Roan Antelope, Brindled Gnu, Kudu na wengine.
Burudani haijaishia hapo, bado unaweza kuamua kufanya utalii wa magari, boti au kutembea kwa miguu kufaidi uzuri wa mbuga hiyo iliyopo umbali wa kilomita 250 kutoka jiji la Dar es Salaam ikiwa utapitia barabara ya kibiti kwa usafiri wa basi.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) Ili kutembelea hifadhi hii itakulazimu kulipia Sh10,000 kwa mtu mzima mwenye umri wa zaidi ya miaka 16, kuanzai mika 15 hadi miaka mitano utalipia Sh2,000 na mtoto chini ya mitano ni bure.
Gharama hizo zinahusisha pia mtalii kutoka nchi zote za Afrika Mashariki, kwa watalii kutoka nje ya ukanda huo watalipa Dola za Marekani 70 (Sh170,515) kwa mtu mwenye umri wa zaidi ya miaka 16, na Dola za Marekani 20 sawa na Sh48,718 kwa watoto chini ya miaka 16.
Kwa raia wa mataifa mengine waishio Tanzania wenye umri wa zaidi ya mika 16 wanaotakiwa kulipa Sh73,078 sawa na Dola za Marekani 30 huku watoto chini umri huo mpaka miaka mitano wakichajiwa Sh24,359 kwa siku moja.
2.Ruaha
Hifadhi ya Ruaha ni ya pili kwa ukubwa nchini, ikiwa na jumla ya kilometa za mraba 20,226 zitakazokupa nafasi ya kuwaona wanyama mbalimbali wakiwemo tembo ambao wakati wa kiangazi hutumia muda mwingi kuchimba mashimo kutafuta maji.
Kama unapendelea utalii wa puto la juu (balloon) Ruaha ndiyo penyewe, utapata nafasi ya kuwaona wanyama ukiwa angani huku ukipata huduma mbalimbali kama chakula na vinywaji zikazofanya safari yako katika mbuga hiyo ilipo katika mikoa ya Iringa, Mbeya na Dodoma kuwa ya kipekee.
Kipindi kizuri wa kutembelea mbuga hii ni wakati wa kiangazi, wakati huu ndipo utakaposhuhudia wanyama wengi zaidi kwa mkupuo kwani wengi hutafuta maji kwenye mto Ruaha na vyanzo vingine vya maji,
Baada ya kipindi cha mvua hifadhi hiyo itakupatia muonekano mzuri wa majani na maua yasiyo kifani hasa maua aina ya daisy, cleome, swathes na ipomoeas.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ipo kilomita 130 kutoka Iringa mjini njia ambayo inapitika kwa urahisi mwaka mzima. Ikiwa utatokea Dar es Salaam itakulazimu kutembea takriban kilomita 625 kuifikia hifadhi hiyo na kilomita 480 ikiwa unatokea Jiji la Mbeya.
Gharama za kiingilio katika kivutio hiki ni Sh5,000 kwa wageni wenye umri zaidi ya miaka 16 wanaotoka ndani ya ukanda wa Afrika mashariki, huku watoto wakitakiwa kulipa Sh2,000.
Kwa wageni wanaotoka nje ya ukanda wa Afrika mashariki wanatakiwa kulipa Dola za Marekani 30(Sh73,078) na watoto wa miaka 15 hadi mitano wanatakiwa kulipa Dola za Marekani 5 sawa na Sh12,179.
Soma zaidi
-
Mapato vituo vya makumbusho ya taifa yaendelea kupaa Tanzania
-
Mataifa 10 yaliyoongoza kuleta watalii wengi Tanzania Oktoba 2022
3.Serengeti
Hii ni moja kati ya hifadhi maarufu iliyopo Kaskazini mwa Tanzania, inayotajwa kuwa na vivutio lukuki zaidi ya hifadhi nyingine zilizopo nchini.
Hifadhi hii ni maskani ya idadi kubwa ya nyumbu, pundamilia, Simba, duma, fisi na swala. Pia utafurahia uzuri wa anga yenye usiku wa baridi utakaofanya ziara yako kwenye hifadhi hii kuwa ya kushangaza.
Serengeti ni jina linalotokana na neno la kimasai “Siringiti” lenye maana ya uwazi usio na mwisho na utafaidi upekee wake endapo utatembelea mbuga hii kuanzia Mei hadi Oktoba kila mwaka kwa sababu miezi mingine inatawaliwa na msimu wa mvua.
Mbuga hii inafikika kwa usafiri wa anga na barabara kupitia mageti ya Naabi Hill, Seronera, Ndutu, Kusini, Kirawira, Handajega, Ikoma, Tabora ‘B’, Lamai, Lobo, Ndabaka, Machochwe na Kleins.
Gharama za kutembelea kivutio hiki ni sawa na zile zinazochajiwa katika hifadhi ya Nyerere kwa watalii wa ndani na nje ya Afrika Mashariki.
4.Kigosi
Hifadhi ya Kigosi iliyopo katika mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga na Tabora ina jumla ya kilometa za mraba 7,460 zenye mandhari nzuri yanayovutia kwa macho.
Hata hivyo, miezi kadhaa iliyopita Bunge la Tanzania lilipitisha azimio la kuifuta hifadhi hiyo na kuridhia kuanzishwa kwa hifadhi ya misitu ya Kigosi itakayosimamiwa na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Akiwasilisha makubaliano ya Azimio hilo Bungeni, Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Nchengerwa amesema licha ya kupitishwa kwa azimio hilo shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ufugaji nyuki, uvuvi wa samaki pamoja na shughuli za kimila zinaruhusiwa kufanyika katika msitu huo.
Kma unapenda utalii wa kutazama nyota wakati wa usiku hifadhi ya Taifa Burigi-Chato inaweza kukufaa.Picha|TANAPA.
5.Burigi-Chato
Burigi-Chato ni hifadhi yenye sehemu kubwa ya pori inayojumuisha maziwa ya maji safi, vilima virefu, miamba ya miinuko, mabonde yaliyo sehemu ya misitu, tambarare wazi, na mamia ya kilomita za mraba za savanna yenye miti, nyasi za kati na ndefu.
Hifadhi hiyo yenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,707 inapatikana kaskazini mwa Tanzania katika maeneo ya Biharamulo, Muleba, Ngara, Karagwe (Kagera Region) na Chato mkoani Geita.
Mbali na uoto wa asili unaonogesha eneo hilo utajionea mandhari nzuri ya ziwa Burigi ambalo ni la tatu kwa ukubwa nchini pamoja na ndege wa aina mbalimbali.
Kufika katika eneo hilo ni rahisi tu ikiwa utatumia usafiri wa ndege au usafiri wa basi kupitia mji wa Chato au Biharamulo.
Gharama za kutembelea kivutio hiki ni sawa na zile zinazochajiwa katika hifadhi ya Nyerere kwa watalii wa ndani na nje ya Afrika Mashariki.
Latest



