Ni nani Makamu wa Rais wa Tanzania kwa sasa ?
- Wakili William Maduhu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anasema kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, Ibara ya 47, mtu hawezi kuwa kiongozi yeyote wa kisiasa kama hatoki kwenye chama cha siasa.
Dar es Salaam. Jana, Agosti 26, 2026, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilitangaza kumfukuza Dk. Nchimbi uanachama kwa madai ya kukiuka Katiba, kanuni na taratibu za chama ikiwa ni siku moja tu tangu atangaze kujiuzulu kutoka katika nafasi ya Makamu wa Rais.
Katika kikao hicho kilichokaliwa na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, CCM pia ilimpendekeza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, kushika nafasi ya Dk Nchimbi.
Hatua hiyo imeibua mjadala wa kikatiba kuhusu iwapo kufukuzwa kwake CCM kunamaanisha moja kwa moja kuwa amepoteza sifa ya kuendelea kuwa Makamu wa Rais, au atasalia katika cheo hicho hadi Septemba 4, 2026 siku aliyosema ataachia madaraka rasmi.
Siku 14 za kikatiba
Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 50(4) iwapo nafasi ya Makamu wa Rais itakuwa wazi kutokana na kifo au kujiuzulu Rais anatakiwa kumteua mtu mwingine kushika nafasi ya hiyo.
Uteuzi huo unatakiwa kufanywa ndani ya siku 14 tangu Makamu wa Rais kuachia madaraka, kisha mtu aliyependekezwa anatakiwa kuidhinishwa na Bunge kwa kura ya wengi ya wabunge kabla ya kuapishwa rasmi na kuanza kutekeleza majukumu yake.
Kwa mwongozo huo wa Katiba, Wakili Peter Majanjara kutoka Chika Attorneys aliiambia Nukta Habari kuwa baada ya Dk Nchimbi kuomba kujiuzulu, siku 14 za kikatiba zinazotoa nafasi ya kufanyika kwa mchakato wa kumpata Makamu wa Rais Mpya zingeanza kuhesabiwa kuanzia Septemba 4.
‘Hawezi kuwa makamu kama hana chama’
Katiba ya Tanzania, Ibara ya 50(2) inaorodhesha mazingira ambayo nafasi ya Makamu wa Rais inabaki wazi.
Miongoni mwa mazingira hayo ni pamoja na muda wake kumalizika, kufariki, kujiuzulu, kuapishwa kuwa Rais baada ya nafasi ya Rais kuwa wazi, kutiwa hatiani kwa kosa la jinai linaloonyesha kukosa uaminifu au uadilifu, Rais mwingine kuapishwa pamoja na Makamu wake au kuondolewa kwa ‘impeachment’ na Bunge.
Hata hivyo, Wakili William Maduhu kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) anasema kufuatia kufukuzwa uanachama Dk Nchimbi ameshapoteza sifa za kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Wakili Maduhu anasema kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 47, mtu hawezi kuwa kiongozi wa kisiasa kama hatoki kwenye chama chochote cha siasa.
Wakili Maduhu amesema tangu Dk Nchimbi kutangazwa kufukuzwa uanachama na Ndejembi kupendekezwa kushika nafasi hiyo, Tanzania iko katika siku 14 za kikatiba za kumpata Makamu wa Rais mpya.
“Nchi hii hatuna mgombea binafsi, hivyo hatua ya CCM kumfukuza uanachama, hata ilo takwa la kuendela kuwa Makamu wa Rais mpaka Septemba 4 linakoma,” amesema Wakili Maduhu.
Hata hivyo, Wakili Maduhu ameongeza kuwa uamuzi wa Dk Nchimbi kujiuzulu kabla ya kufukuzwa uanachama kutaendelea kumtambulisha kama Makamu wa Rais mstaafu akipata stahiki zake zote kikatiba.