Rais Samia aridhia Makamu wa Rais Dk Nchimbi kujiuzulu

August 25, 2026 9:43 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Hatua hiyo inakuja saa chache baada ya Nchimbi kung’atuka na kueleza kuwa Rais Samia anatamani mabadiliko.
  • Katiba ya Tanzania inaeleza kuwa mara baada ya kiti hicho kuwa wazi, ndani ya siku 14 Rais anapaswa kumteua mtu mwingine atakayethibitishwa na zaidi ya nusu ya wabunge.

Dar es Salaam. Saa chache baada ya Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Emmanuel Nchimbi kutangaza kujiuzulu, Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi hilo, hatua inayofungua mchakato mpya wa kumpata mrithi wa kiongozi huyo atakayemsaidia kuongoza katika kipindi cha zaidi ya miaka minne iliyosailia. 

Mapema leo asubuhi (Agosti 25, 2026) Dk Nchimbi alieleza katika taarifa yake kwa umma kuwa amemjulisha Rais Samia juu ya adhma yake ya kustaafu siasa na utumishi wa umma na kwamba atang’atuka katika kiti hicho kuanzia Septemba 4, 2026. 

Katika taarifa hiyo kwa umma iliyoibua mjadala na mshtuko nchini, Nchimbi amesema alimwahidi Rais Samia Agosti 27 mwaka jana kuwa angemsaidia yeye na nchi kwa uwezo wake na kwa uaminifu. 

“Pia, nilimuhakikishia kuwa siku yeyote akiona anahitaji makamu mwingine wa rais, nitaachia nafasi hii. Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa mheshimiwa Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu,” amesema Nchimbi katika taarifa hiyo. 

Kutokana na uamuzi huo, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka amesema katika taarifa yake kuwa Rais Samia amepokea barua hiyo na kuridhia kujiuzulu kwa Dk Nchimbi kuanzia Septemba 4, 2026. 

“Taratibu za kikatiba za kumpata Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwingine zitachukuliwa,” amesema Balozi Kusiluka.

Makamu wa Rais mpya ndani ya siku 14?

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, mara baada ya kiti cha Makamu wa Rais kuwa wazi ndani ya siku zisizozidi 14, mapema iwezekanavyo Rais atamteua mtu atakayekuwa Makamu wa Rais kushika madaraka yake na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura za wabunge walio wengi.

Bunge la Tanzania linatarajiwa kuanza vikao vyake vya mkutano wa nne wa Bunge la 13 kesho Agosti 26, 2026 na hapana shaka wabunge watakuwa na kibarua cha kumpigia kura makamu wa rais ajaye. 

Kujiuzulu kwa Dk Nchimbi kunaingia kwenye rekodi ya matukio makubwa ya siasa nchini ya vigogo wa juu wa chama na Serikali kung’atuka ndani ya miaka mitano iliyopita. Katika kipindi hicho, Spika wa Bunge Job Ndugai alijiuzulu wadhifa wake Januari 2022 baada ya kukosolewa vikali kutokana na maoni yake juu ya wasiwasi uliotokana na kuendelea kupaa kwa deni la taifa. 

Miaka takriban miwili baadaye, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo naye alitangaza kung’atuka katika wadhifa huo kwa kile alichokiita kuchafuliwa kwenye mitandao. 

Kujiuzulu kwa Dk Nchimbi kumekuja mwezi mmoja tu tangu aeleze kuwa kama moja ya mambo angetamani awaambie Watanzania basi ni wapambanie katiba mpya inayojumuisha makubaliano ya wadau wote na inayolinda uhai na haki za watu. 

“Katiba inayoheshimu haki za raia wake…katiba inayotupeleka kwenye maendeleo, si maendeleo  ya mali tu na uchumi lakini maendeleo ya heshima na utu wa binadamu anayeishi katika Tanzania,” alisema Dk Nchimbi wakati wa Mkutano Mkuu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) jijini Dar es Salaam. 

Wiki iliyopita Idara ya Huduma za Habari (Habari Maelezo) ililifungia gazeti la Mwanahalisi kwa kipindi cha miezi sita baada ya kuchapisha habari iliyokuwa inaeleza kuwa Dk Nchimbi alikuwa amegoma kujiuzulu kwa madai ya kukiuka Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
25 Aug, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
25 Aug, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Elimu ya kodi mwarobaini wa wafanyabiashara kuikwepa TRA, ianzie shuleni

Elimu ya kodi mwarobaini wa wafanyabiashara kuikwepa TRA, ianzie shuleni

Nukta TV

Rais Samia: Serikali chini ya Magufuli haikutaka kuyumbishwa kukamili kwa JNHPP

Rais Samia: Serikali chini ya Magufuli haikutaka kuyumbishwa kukamili kwa JNHPP

Nukta TV

Rais Samia: Umeme wa SGR hautoingiliwa, Dodoma umeme uhakika 24/7

Rais Samia: Umeme wa SGR hautoingiliwa, Dodoma umeme uhakika 24/7

Nukta TV