Ukosefu wa umeme wakwamisha vijana, wanawake ‘kutoboa’ kiuchumi
- Ukosefu wa umeme unavyokwamisha vijana, wanawake ‘kutoboa’ kiuchumi
- Baadhi ya wanakijiji Maswa hutumia nauli ya Sh10,000 kwenda kupiga photocopy ya Sh200.
- Wanawake waeleza kuwa umeme ungekuwepo ungewasaidia kujikwamua kiuchumi.
- Halmashauri ya Maswa yasema vijiji visivyo na umeme vitaunganishwa siku za hivi karibuni.
Simiyu. Baada ya kupambana na changamoto za kukosa huduma kutokana na kutokuwa na kitambulisho cha Taifa mapema mwaka 2020, Neema Dengeli alilazimika kusafiri kwenda kijiji cha jirani kupata huduma ya nakala maarufu kama ‘photocopy’.
Safari hiyo ya Neema ya takriban kilomita tano ilikuja baada ya kijiji chao cha Mwamihanza kukosa umeme.
“Kitambulisho cha Nida ni muhimu inakubidi tu uende na bodaboda ili uweze kupata kile kitu,” anasema Neema.
Gharama ya kutoa photocopy ya nyaraka alizokuwa akihitaji ilikuwa Sh200 tu ila alilazimika kutoboa mfuko zaidi na kupoteza muda wa zaidi ya saa tatu kwa kuwa huduma hiyo haipatikani kijijini kwao.
Atumia Sh10,000 kupiga photocopy ya Sh200
“Safari ya kwenda na kurudi Isulilo pamoja na photocopy ilinigharimu Sh10, 000 lakini umeme ungekuwepo hapa huenda ningetumia Sh200 tu,” anasema Neema.
Neema mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa ni miongoni mwa Watanzania ambao wanajikuta wakitumia fedha nyingi kupata huduma kwa kuwa maeneo yao hayana umeme wa uhakika.
Ukosefu wa umeme ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili baadhi ya wakazi wa vijiji vya Maswa mkoani mkoani Simiyu.
Serikali inasema zaidi ya asilimia 83 ya vijiji wilayani humo tayari vina umeme kiasi cha kuifanya kuwa wilaya yenye vijiji vingi vinavyopata nishati hiyo mkoani Simiyu.
Soma zaidi:
- Hali halisi ya walimu shule za msingi Pangani
- Uamuzi mgumu UN: Nani apatiwe msaada wa chakula Afrika Mashariki?
Kuchelewa kuwekwa umeme katika baadhi ya vijiji kikiwemo cha Mwamihanza na vitongoji ambavyo havijaunganishwa kunazidi kuwanyima fursa vijana wengi wanaohaha kujiajiri kupitia nishati hiyo.
Mfano, Richard Pius, Mkazi wa Mwamihanza iwapo anahitaji huduma za kuchomelea vyuma hulazimika kusafiri hadi ama Maswa kilomita 39 kutoka kijijini kwao ama Malampaka ambapo hutakiwa kuwa na nauli isiyopungua Sh10,000 kwenda na kurudi.
Pius anasema huduma za uchomeleaji ni fursa ambayo ingesaidia vijana wengi wa kijiji chao wenye ujuzi huo kujiajiri na kujikwamua na umaskini.
Umeme ungewaokoa na umaskini
Kwake umeme ni zaidi ya nishati ya kutoa mwanga nyumbani kwa kuwa unaweza kusaidia shughuli za uzalishaji zinazoingiza kipato.
“Sisi kama vijana tungefanya kazi za ukinyozi, tungeteneza vitu mbalimbali kama kuchomelea mageti, matumizi ya kompyuta,” anasema.
“Hapa mtaani wapo vijana waliosomea hayo mambo lakini kwa kuwa hawana umeme wanashindwa kutumia ujuzi wao,” anaongeza Richard.
Katikati ya kijiji chao kuna saluni inayotumia umemejua kwa kutumia paneli ndogo ya sola jambo linalofanya nishati yake isikidhi mahitaji wakati wote.
Hii ni tofauti na vijiji kama Lalago ambako kuna umeme ambapo vijana wengi wamejiajiri kwa kutumia umeme. Kijiji hicho kimechangamka na wanawake wa kijiji hiki wamefungua migahawa yenye umeme jambo linalowafanya wauze mpaka usiku.

Baadhi ya vijana katika Kijiji cha Lalago wilayani Maswa wakifanya shughuli za uchomeleaji vyuma. Upatikanaji wa umeme umesaidia kupunguza tatizo la ajira na kusogeza huduma katika kijiji hiki. Picha|Nukta TV.
Bado kuna vijiji havina umeme Maswa
Ni vitongoji vichache vya vijiji vya Lalago na Gula ambavyo havina umeme lakini baadhi ya wakazi wamejiongeza kwa kuweka sola ndogo kwa ajili ya kupata mawasiliano.
Wasio na uwezo wa kununua sola kama Neema wa Mwamihanza wanabaki kutamani maendeleo ya wenzao.
Neema anasema umeme ungewasaidia sana wanawake kujikwamua na umaskini kwa kuwa wangefanya shughuli za uzalishaji mali.
“Umeme ungekuwepo hapa ningeuza barafu, ningetengeneza juisi na kuziweka kwenye friji, ningenunua ‘blender’ (mashine ya kutengenezea juisi) ili niweze kufanya biashara. Sola haiwezi vyote hivyo, jua lisipokuwepo sola haiwezi kufanya kazi vizuri,” anasema.
Ukosefu wa umeme anasema unaathiri baadhi ya masuala ya kijamii ikiwemo ndoa.
“Hapa una hamu na juisi baridi hupati, unataka kunyoosha nguo huwezi kwa sababu hakuna pasi ya umeme. Mme wangu naye huwa anavaa nguo hivyo hivyo hazijanyooshwa kwa sababu hakuna umeme, anaona hali halisi,” anasema Neema.
Benki ya Dunia: Umeme uchochea maendeleo
Benki ya Dunia (WB) inasema kuwa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa bei nafuu unasaidia kuongeza uzalishaji unaochochea ongezeko la ajira, kuboresha maisha ya kaya na kuchagiza kufanikisha malengo ya ukuaji wa kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, tayari kuna nguzo za umeme kijijini hapo ambazo zilisimikwa katika robo ya mwisho ya mwaka 2021.
Pamoja na kusimikwa nguzo hizo, wanakijiji wa Mwamihanza hawana imani kuwa watapata nishati hiyo siku za hivi karibuni.
“Kusimikwa kwa nguzo si kwamba umeme umeanza kutumika mpaka tushuhudie umewashwa na tumeunganishiwa. Wakituunganishia tumejiandaa kuutumia vizuri huo umeme,” anasema Pius.
Kwa Neema, kilio chake ni Serikali kuharakisha mchakato wa kupeleka umeme katika kijiji hicho ambacho kinakaliwa na wakulima pamoja na wafugaji.
Serikali imeshaweka nguzo kwenye sehemu ya Kijiji cha Mwamihanza lakini ni zaidi ya miezi minne sasa bado hawajaunganisha umeme jambo linalowapa wasiwasi baadhi ya wakazi wa eneo hili kuwa huenda ukachelewa zaidi. Picha|Nukta TV.
‘Tutatatua tatizo’
Serikali inasema Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wanaendelea kupeleka huduma katika maeneo ya vijiji na vitongoji vilivyosalia ili kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo nao wanafaidika na nishati hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Maswa, Vivian Christian wilaya ya Maswa ni moja ya wilaya zenye vijiji vingi vyenye umeme katika mkoa wa Simiyu na kwamba katika mwaka huu wa fedha 2021/22 vilivyosalia vitakuwa vimefikiwa.
“Ni kweli kuna maeneo ambayo umeme ulifika baadhi ya vitongoji na baadhi ya taasisi zetu kama shule, zanahati, sekondari hazikupata umeme, kwa hiyo kwenye mpango huu wa kukamilisha vijiji vyote 120 vinapata umeme na maeneo ambayo taasisi hazina umeme utawekwa,” anasema Christian.
Tangazo:

Umeme umechochea maendeleo Maswa
Kiongozi huyo wa halmashauri anasema umeme umesaidia sana mambo mengi kwenye vijiji vyenye umeme kwa kusaidia watu wamejiajiri kupitia shughuli za uchomeleaji vyuma, saluni na maeneo mengi wananchi wamejenga nyumba bora.
“Kuna vijiji takriban 100 vina umeme. Ni vijiji 20 hivi havina umeme… kwa mwaka wa fedha 2021/22 kupitia wenzetu wa Tanesco wilaya na mkoa vijiji vyote vinatarajiwa kupatiwa umeme,” anasema.
“Tuombe tu kila kitu kiende sawa kwa sababu Serikali haiwezi kumaliza tatizo lote la umeme kwa wakati mmoja lakini tunaamini watamaliza na uzuri wakandarasi wa REA wapo ‘site’ (kazini),” anaongeza Vivian.
Katika kuhakikisha maeneo yenye umeme vijana na wanawake wanatumia ipasavyo fursa za nishati hiyo, Vivian amesema wamepanga kuanzisha maeneo ya kibiashara yatasaidia wengi kufanyia biashara ambapo mfanyabiashara atapewa hati inayoweza kusaidia kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha.
“Tunawahimiza wajiunge kwenye vikundi waweze kujiajiri,” anasema.