Wanafunzi wabuni suluhu ya kuongeza uzalishaji mazao Singida

November 5, 2021 1:53 pm · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Washauri wakulima wa mtama, ulezi na alizeti kupanda mbegu zinazostahimili ukame.
  • Wasema mafuriko yachangia kuongeza chumvi kwenye ardhi.
  • Pia wakulima washauriwa kuipumzisha ardhi walau mwaka mmoja. Singida.

Dar es Salaam. Hakuna shaka kiu ya wazazi wengi ni kuona watoto wao wakiyaandika majina yao kwenye vibao vya jamii kwa kutatua changamoto ambazo zinawasumbua Watanzania na hata dunia kwa ujumla.

Kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dr Salmin Amour ya mkoani Singida, changamoto waliyoiona ni mafuriko kuwa tatizo kwa wakulima pamoja na ustawi wa kilimo mkoani humo.

Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wao kutoka Shirika la Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), wanafunzi Fadhili Shabani na Shufaa Omari  wanaosoma kidato cha tatu, wametafuta suluhu ya changamoto ya wakulima wa mazao ya mtama, ulezi na alizeti.

Kwa mujibu wa wasilisho la wanafunzi hao, Shabani amesema Mkoa wa Singida una maziwa mawili ambayo ni Ziwa Kindai na Ziwa Singidani ambayo hufurika kipindi cha mvua na hivyo maji kufikia makazi na mashamba.

Mafuriko hayo husafirisha chumvi inayopatikana kwenye maji ya maziwa hayo na kuiacha kwenye udongo ambao unategemewa na wakulima.

Shabani amesema, kiasi kingi cha chumvi kwenye udongo kinasababisha udumavu katika ukuaji wa mazao.

“Aina za mimea zinatofautiana kwa jinsi zinavyovumilia ardhi iliyoathiriwa na chumvi. Mimea mingine inaweza kuvumilia kiasi kingi cha chumvi na mimea mingine haiwezi,” amesema Shabani.

Kwa upande wake Omari amesema utafiti wao ulilenga kugundua kama kiwango cha chumvi ya ardhini kinachangia kwa namna yoyote uotaji wa mbegu.

“Majawabu ya utafiti wetu yatasaidia wakulima kujua sehemu zinazofaa kupanda mazao na muda gani pia,” amesema Omari.

Washindi wa mashindano ya Wanasayansi chipukizi mwaka 2021 Fadhili Shabani (kulia) na Shufaa Omari (kushoto). Picha| YST.

Changamoto yafahamika

Wanafunzi hao wamesema, changamoto iliyopo ni kuwa ardhi kuwa na chumvi nyingi ni sawa sawa na ardhi kuwa na ukame na hivyo wakulima wanapopanda mbegu zao kwenye ardhi hiyo, wanaishia kupata mavuno madogo ikilinganishwa na kabla ya kipindi cha mafuriko ya mwaka 2020.

Wanafunzi hao wamesema, hiyo inasababishwa na mbegu kuchukua muda mrefu kuota na pia zingine kufa kutokana na changamoto zingine za ardhi.


Suluhu hii hapa

Omari na shabani wamesema, ili wakulima wa mkoani humo wasipate hasara inatakiwa wapande kwa wingi mbegu za mahindi, mtama na ulezi na siyo alizeti kwani alizeti ndiyo inaathirika zaidi.

Endapo wakitaka kupanda mbegu za alizeti, wanafunzi hao wameshauri watumie mbegu zilizo na uvumilivu wa ukame na mbegu zinazostawi kwa uharaka.

Mgunduzi mwenza wa YST, Dk Gozibert Kamugisha amesema mwaka huu mashindano hayo yanaadhimishwa kwa mara ya 11 na lengo la YST ni kuhakikisha wanafunzi wengi wanashiriki na kupata hamasa ya kisayansi.

“Inashauriwa wakulima kutokuilima ardhi kwa mfululizo. Walau waipumzishe ardhi kwa msimu mmoja bila kuilima ili ardhi irudie nguvu yake,” wamesema Omari na Shabani.

Wanafunzi hao wamewatoa hofu wakulima ya kuwa hali haitokuwa hivyo milele bali endapo mvua za wastani zitanyesha, hali ya uchumvi kwenye ardhi itapungua.

Mashindano ya wanasayansi chipukizi mwaka huu yamefanyika kwa ngazi ya nchi nzima yakihusisha mikoa 24 ya Tanzania Bara.

Prof Ndalichako amesema maono ni kuona kila shule na kila mwanafunzi anafikiwa na mashindano hayo. Picha| YST.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa, Joyce Ndalichako akitoa zawadi kwa wanafunzi hao amesema  kwa mwaka 2021, mashindano hayo yamehusisha shule 248 na wanafunzi 1,158.

“Wale ambao hawakubahatika kuingia katika washindi ambao hawatazawadiwa leo hii, mimi ninawaambia wote ni washindi,” amesema Prof Ndalichako.

Waziri huyo wa elimu amewasihi wanafunzi kujiamini na kuthubutu kushindana kwenye mashindano ya kielimu ikiwemo Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (Makisatu).

Matarajio ya Prof Ndalichako ni kuona mashindano hayo yanashuka kwa ngazi ya wilaya kutoka ngazi ya mkoa ili kufikia shule na wanafunzi wengi zaidi.

“Lengo kuu la kufanya yote haya ni kuhakikisha kila shule, kila mwanafunzi, anashiriki katika utafiti wa kisayansi na ugunduzi wa kiteknolojia,” amesema Prof Ndalichako.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV