Namna ya kuepuka kupokea barua pepe usizozihitaji
- Ni pamoja na kuzuia (kumblock ) mtumaji ujumbe na kufuta usajili
- Unaweza kutumia njia hizo kwenye vifaa vyote vya mawasiliano kama simu na kompyuta
Dar es Salaam. Barua pepe ni miongoni mwa nyanja rasmi miongoni mwa njia mbalimbali za mawasiliano, njia hii hutumiwa sana na taasisi au mashirika katika utoaji wa huduma au uuzaji wa bidhaa.
Baadhi ya watu hutumia njia hiyo ili kukipa uzito kile kinachozungumzwa katika mawasiliano hayo, ingawa imeibuka changamoto ambayo inawakabili watu wengi wanaotumia barua pepe, ya kupokea jumbe wasizozihitaji jambo ambalo husababisha kero na usumbufu.
Barua pepe za hizo wakati mwingine huwa za vitisho, utapeli au matangazo ambayo yanavunja sheria za matumizi ya mtandaoni, hivyo kujiondoa kwenye barua pepehizo kunaweza kukuondoa kwenye changamoto hizo.
Makala hii inaangazia njia mbalimbali unazoweza kutumia ili kujiepusha na kadhia hiyo.
Fanya haya kujiondoa au kuzuia usipokee jumbe
Kwa mujibu wa kituo cha msaada cha Mtandao Google (Google help centre) zipo njia mbalimbali zinazoweza kutumika kujiondoa kwenye barua hizo ambazo hutaki kuendelea kuzipokea.
“Unaweza kuzuia(block),kujiondoa (unsubscribe) kutoka kwa mtumaji, au kuripoti ujumbe kwa Gmail,” kimesema kituo hicho.

Barua pepe nyingine huja na ujumbe unaowekwa juu unaokutaka kujiondoa.Picha|How to Greek.
Kujiondoa kwa ku-block mtumaji wa ujumbe
Kama ambavyo unaweza kuzuia mtu asikupigie simu (ku-block) au kukutuma ujumbe mfupi, mbinu hiyo inaweza kutumiwa kujiondoa katika barua pepe za tovuti hizo.
Danford Kijana mshauri na mtengenezaji wa mifumo ya kompyuta anasema unachotakiwa kufanya ili kujiondoa kwenye tovuti hizo ni kufungua program tumizi (application) ya Gmail iliyopo katika simu yako kisha fungua barua pepe ambayo hutaki kuendelea kuipokea.
“Ukishafungua bonyeza vitufe vitatu vilivyopo upande wa kulia kisha chagua neno lilioandikwa ‘block’ kwa kufanya hivyo utakuwa tayari umezuia ujumbe huo kutumwa tena kwenye barua pepe yako,” amesema Kija
Soma zaidi
Yafahamu matunda yanayoweza kutibu na kukupa kinga ya maradhi
Jinsi ya kuhariri na kuficha meseji zako WhatsApp
Njia hii inafanya kazi kwa aina zote za simu na kompyuta.
Kujiondoa kwa kujitoa kwenye huduma (ku-unsubscribe)
Mbinu nyingine inayoweza kuzuia ujumbe wa mara kwa mara katika barua pepe yako ni hii ya kujiondoa (unsubcribe) ambayo tunaweza kusema ni sawa na kufuta usajili wako katika tovuti hizo.
Hii ni kwa wale ambao wamewahi kupata huduma katika tovuti fulani au taasisi na hawahitaji tena kuendelea kupata huduma hizo
Kituo cha msaada cha google kinasema Ili kujiondoa kwa njia hii ni lazima ufungue barua pepe ambayo hutaki kuendela kuipokea kisha utafute sehemu iliyoandikwa Unsubscribe.
Mara nyingi sehemu hii hukaa chini kabisa mwisho wa barua pepe , ukibonyeza hapo hutapokea tena jumbe hizo. Hata hivyo kituo hicho kinasema hatua hii itachukua siku chache kukamilika.

Kuripoti ujumbe wa barua pepe kwa google ni moja ya njia rahisi na ya uhakika inayoweza kuzuzia akaunti yako isipokee tena barua pepe kutoka tovuti hizo.Picha|Pc Mag.
Ripoti ujumbe kwa Google
Mara nyingi mbinu hii hutumika kuripoti uvunjifu wa sheria za kimtandao(cyber security laws) kama udhalilishaji matusi na utapeli.
Hata hivyo mbinu hii pia inaweza kukupunguzia adha ya kupokea jumbe nyingi usizozihitaji cha kufanya ukishafungua ujumbe ambao hutaki kuendelea kuupokea tafuta sehemu iliyoandika ‘report spam’.
Sehemu hii ipo juu kabisa yabarua pepe yako, ukishabonyeza itakutaka uhakikishe uamuzi wako na baada ya hapo utakuwa umeshajiondoa.
Tumia program tumizi kujiondoa
Mtaalamu wa kompyuta Danford Kija anasema kuwa kuna program tumizi ambazo zimetengenezwa kwa ajili ya kuzuia baadhi ya ujumbe usiingie katika email yako.
Costantine Madalali ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Coxstore kupitia ukurasa wake wa twitter anasema moja ya program tumizi unazoweza kutumia kujiondoa kupokea ujumbe kwenye email ni ‘Unrol.me’.
Program tumizi hii inakusanya barua pepe zote ulizojisajili na kukusaidia kujiondoa katika zile usizotaka.
Hata hivyo program hii haifunguki kwenye simu nyingi zilizopo nchini ili kuifungua ni lazima utumie mtandao wa kibinafsi (VPN).
Mtandao huo utakuwezesha kubadilisha anwani ya nchi ulipo hivyo kuweza kuipakua na kuitumia kwa urahisi.
Ni muhimu kuwa makini unapojisajili katika majukwaa mbalimbali kupata huduma ili kujua kwa undani ni aina gani ya hudma utaenda kupata hii ni pamoja na kusoma sera za faragha za mtandao au taasisi husika ili kuepuka usumbufu baadae.