Namna Tanzania inavyotaka kulinda viwanda vya ndani bajeti 2025/26

June 14, 2025 5:54 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kupitia msamaha wa kodi, kuondoa misamaha isiyo na tija pamoja na kufanya mabadiliko kwenye kodi na ushuru wa forodha kwa bidhaa za nje.
  • Lengo ni kutoa nafuu kwa wazalishaji wa ndani, kuvutia uwekezaji, kulinda masoko ya ndani, kupanua wigo wa ajira, pamoja na kuongeza mapato ya Serikali.

Dar es Salaam. Hapana shaka Serikali ya Tanzania imepanga kukuza na kulinda viwanda vya ndani baada ya kupendekeza maboresho mengi ya kodi, tozo na ushuru wa forodha wa bidhaa katika bajeti ya mwaka 2025/26. 

Hatua hizo ni mwendelezo wa Serikali kukuza sekta ya viwanda ambayo ni moja ya vichocheo vikubwa vya ukuaji wa uchumi kwa kutoa ajira na kuzalisha bidhaa zinazopunguza matumizi ya bidhaa kutoka nje ya nchi.

Uchambuzi wa hotuba ya bajeti hiyo uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa sehemu kubwa ya hatua hizo za kisheria zilizolenga kufanyia marekebisho sheria 28, Serikali imelenga kutoa nafuu kwa viwanda vya ndani kupitia msamaha wa kodi, kuondoa misamaha isiyo na tija pamoja na kufanya mabadiliko kwenye kodi na ushuru wa forodha kwa bidhaa za nje.

Hatua hizo ni mwendelezo wa Serikali kukuza sekta ya viwanda ambayo ni moja ya vichocheo vikubwa vya ukuaji wa uchumi kwa kutoa ajira na kuzalisha bidhaa zinazopunguza matumizi ya bidhaa kutoka nje ya nchi. Picha | Wizara ya Fedha.

Hatua hizo pia zimelenga kuvutia uwekezaji, kulinda masoko ya ndani, kupanua wigo wa ajira, pamoja na kuongeza mapato ya serikali ambayo ina presha kuwa na fedha za kutosha kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo reli ya kisasa (SGR). 

Nafuu viwanda vya ndani kupitia msamaha wa kodi

Katika bajeti hiyo itakayoanza kutekelezwa Julai mosi mwaka huu, Serikali imependekeza msamaha wa kodi kwa baadhi ya bidhaa zinazotumika kama malighafi katika viwanda nchini. 

Miongoni mwa bidhaa zilizopendekezwa kusamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni pamoja na mafuta ya kula yanayozalishwa nchini kwa kutumia mbegu zinazolimwa ndani ya nchi. Katika pendekezo hilo, kwa mwaka mmoja, mafuta hayo yatakuwa na VAT ya kiwango cha sifuri.

Hatua hii, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, inalenga kutoa unafuu kwa viwanda vya kuchakata mafuta ya kula ili kuongeza uzalishaji, kuhimiza matumizi ya malighafi ya ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa za kula kutoka nje. 

Miongoni mwa bidhaa zilizopendekezwa kusamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ni pamoja na mafuta ya kula yanayozalishwa nchini na nguo. Picha | Wizara ya Viwanda na Biashara.

Ili kukuza viwanda vya nguo, Serikali imependekeza kusamehe VAT kwa nguo zinazozalishwa kwa kutumia pamba inayolimwa nchini. Mapendekezo haya ni hatua ya kulinda viwanda vya nguo ambavyo vimekuwa vikikumbwa na ushindani mkali kutoka kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa bei nafuu. 

Kwa kuondoa VAT kwa mwaka mmoja kwa bidhaa hizo, Dk Nchemba anasema Serikali inalenga kufufua viwanda vya nguo, kuongeza thamani ya zao la pamba, na kusaidia kuongeza ajira hasa kwa vijana na wanawake katika sekta ya ushonaji na usindikaji wa vitambaa.

Nguo ni miongoni mwa bidhaa zinatumiwa zaidi nchini lakini wazalishaji wa ndani wanakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka China na mataifa mengine yanayozalisha mavazi hayo kwa gharama nafuu. 

Malighafi, zana za Kilimo zapatiwa nafuu ya kodi

Katika kusaidia sekta ya kilimo cha viwanda, ambayo hutegemewa kama chanzo cha malighafi kwa viwanda vya ndani, Serikali pia imependekeza kusamehe VAT kwenye baadhi ya zana za kilimo kama matairi ya matrekta, shoka, reki na forks. 

Aidha pia, mbolea inayozalishwa ndani imepewa nafuu kwa kutozwa VAT ya sifuri kwa kipindi cha miaka mitatu. Ikiwa ni moja ya sehemu ya kuongeza uzalishaji wa kilimo kinacholisha viwanda, kupunguza gharama za uzalishaji na hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani katika soko la ndani na nje.

Kuondoa misamaha hatarishi ukuaji wa viwanda vya ndani

Katika kuhakikisha viwanda vya ndani vinakuwa na mazingira bora ya ushindani, Serikali imependekeza kufuta baadhi ya misamaha ya VAT ambayo ilikuwa inahamasisha uingizwaji na ununuji wa bidhaa nchini. 

Bidhaa hizo ni pamoja na ‘gaming supply’ (vifaa vya michezo ya kubahatisha) na lami (bitumen), ambazo serikali sasa imeamua kutotoa msamaha tena. 

Uamuzi huu umechukuliwa kwa lengo la kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa hizo hapa nchini.

Kwa muda mrefu wamiliki wa viwanda, wataalamu wa uchumi na wabunge wamekuwa wakiitaka Serikali kulinda viwanda vya ndani kwa kuweka kodi wezeshi na kudhibiti uingizaji wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Kodi, ushuru mpya bidhaa za nje

Hata hivyo, pamoja na kutoa nafuu, Serikali imechukua hatua madhubuti za kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka kwa bidhaa za nje. 

Kupitia mabadiliko ya ushuru wa forodha, baadhi ya bidhaa zinazotengenezwa nchini na zinazoagizwa kwa wingi kutoka nje zimeongezewa kodi ili kupunguza uingizaji wa bidhaa hizo. Dk Nchemba amesema lengo la hatua hiyo ni kulinda viwanda vya sabuni, siagi ya karanga na viberiti vilivyopo nchini ambavyo vina uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo kwa ubora unaokubalika. 

Bidhaa hizo ni pamoja na sabuni, ambazo sasa zitatozwa ushuru wa bidhaa wa asilimia 10, Viberiti kutoka nje vitatozwa Sh400 kwa kila kilo, huku siagi bandia au majarini zikitozwa Sh500 kwa kila kilo. 

Serikali pia imependekeza ongezeko la ushuru wa forodha kwa bidhaa za chuma, mabati, chumvi na marumaru kutoka nje. Kwa mfano, bidhaa za chuma zitalipiwa ushuru wa forodha wa hadi asilimia 35 au Dola za Marekani 500 kwa tani, kulingana na aina ya bidhaa. 

Serikali imechukua hatua madhubuti za kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani usio wa haki kutoka kwa bidhaa za nje. Picha | Mwananchi.

Katika mapendekezo hayo ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, mabati yanayoingizwa kutoka nje yameongezewa ushuru wa kiwango kama hicho, lengo kuu likiwa ni kulinda viwanda vya bidhaa hizo ambavyo vinaendelea kuwekeza nchini. Chumvi kutoka nje sasa itatozwa ushuru wa asilimia 50, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15 kutoka kiwango cha awali cha asilimia 35. 

Hii, anasema, inalenga kuimarisha viwanda vya chumvi vya ndani ambavyo vimekuwa vikikumbwa na ushindani mkubwa kutoka kwa bidhaa za nchi jirani.

Chumvi ni bidhaa muhimu ya chakula na ambayo uzalishaji wake huusisha wakulima wa chumvi hususan wanaoishi pembezoni mwa bahari ikiwemo wale wa mikoa ya Lindi, Pwani, Mtwara na Tanga.

Tozo mpya ya maendeleo ya viwanda

Mbali na kodi na ushuru, serikali imependekeza Tozo ya Maendeleo ya Viwanda kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, ambazo tayari huzalishwa nchini. Tozo hii inalenga kuimarisha mapato ya serikali na kuweka mazingira ya ushindani kwa wazalishaji wa ndani. 

Miongoni mwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje zitakazoathirika ni marumaru na vigae, ambavyo vitatozwa tozo ya asilimia 10 au Sh4,500 kwa kila mita ya mraba, pamoja na vioo vya aina mbalimbali vitakavyotozwa tozo ya asilimia 10 ya thamani. 

Hatua hii imechukuliwa kutokana na ongezeko la uingizaji wa bidhaa hizo ambazo tayari huzalishwa na viwanda vya ndani vilivyo katika harakati za kujiimarisha.

“Hatua hizi za Kodi ya ongezeko la thamani kwa ujumla wake zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 833,829.13,” imeeleza Hotuba ya Bajeti 2025/2026. 

Serikali imependekeza Tozo ya Maendeleo ya Viwanda kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka nje, ambazo tayari huzalishwa nchini. Tozo hii inalenga kuimarisha mapato ya serikali na kuweka mazingira ya ushindani kwa wazalishaji wa ndani. Picha | Wizara ya Viwanda na Biashara.

Sehemu kubwa ya mapato haya inatokana na kufutwa kwa misamaha isiyo na tija na kuongeza ushuru wa bidhaa kutoka nje ambazo tayari huzalishwa ndani ya nchi.

Kwa ujumla, bajeti ya mwaka 2025/2026 imeweka msisitizo mkubwa katika kujenga msingi imara wa uchumi wa viwanda kwa kutoa motisha kwa wazalishaji wa ndani na wakati huo huo kupunguza uingizaji wa bidhaa ambazo zinaweza kuzalishwa nchini. 

Ikiwa hatua hizi zitasimamiwa ipasavyo na mapendekezo haya yatapitishwa na Bunge, zinaweza kuwa kichocheo cha mapinduzi ya viwanda, kuongeza ajira, kukuza uchumi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Huenda mapendekezo ya hatua hizi kutoka kwa Serikali zinakwenda kujibu malalamiko ya wadau na wawekezaji wa viwanda nchini ikiwemo wabunge ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia na kuishauri Serikali kuvilinda viwanda vya ndani kwa kupunguza uingizaji wa bidhaa ambazo huzalishwa pia nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks