Mwelekeo mpya utatuzi mgogoro wa uhifadhi Ngorongoro
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro, katika ukumbi wa mikutano wa Ngorongoro Mkoani Arusha Februari 17, 2022. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Serikali yasema wanaotaka kuhama eneo hilo wako huru.
- Yaandaa mpango kuboresha eneo hilo.
- Itaendelea kukutana na wadau kupokea maoni zaidi.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wanaotaka kuhama kwa hiari yao wajitokeze na waseme wanataka kwenda wapi ili Serikali iwahudumie huku akisisitiza utulivu wakati ikitafutwa suluhu ya mgogoro wa uhifadhi wa eneo hilo.
Kumekuwa na maoni tofauti kuhusu mgogoro wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambapo baadhi ya watu wameshauri Serikali iwaondoe wafugaji wa kijamii ya kimasai ambao idadi yao imekuwa ikizidi kuongezeka siku hadi siku na kutishia uhifadhi wa wanyama katika eneo hilo.
Hata hivyo, wengine wanadai kufanya hivyo itakuwa kinyume na haki za binadamu kwa sababu wafugaji hao wamekaa kwa muda mrefu katika eneo hilo ambalo ni sehemu muhimu kuendeleza maisha yao.
Majaliwa amesema kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kunakoleta changamoto katika uhifadhi, watu wanaotaka kuhama kwa hiari yao wako huru kufanya hivyo.
“Kama yuko mtu wa aina hiyo, awe huru kwenda kwa DC (Mkuu wa Wilaya) kajiandikishe na Serikali itakuhudumia vizuri. Hayo ni maamuzi ya mtu binafsi, kusiwe na mtu wa kumshinikiza fulani asifanye maamuzi yake. Kama yuko aachwe afanye maamuzi yake, aseme anataka kwenda wapi na sisi tutamhudumia,” amesema Majaliwa.
Majaliwa ametoa kauli hiyo jana jioni (Februari 17, 2022) wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kwenye kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya zamani ya NCAA, wilayani Ngorongoro.
Amesema Serikali ina nia njema ya kumaliza mgogoro huo bila kumuathiri mtu yoyote, hivyo ushirikiano wa wadau mbalimbali unahitajika.
“Hakuna jambo linataka kufanywa kwa trick (njama) kwa kutaka kumuathiri Mtanzania, hakuna Serikali ya namna hiyo. Kila jambo linalozungumzwa kwenu ni jema tu, linafanywa kwa nia njema,” amesema Majaliwa kwa wakazi wanaoishi karibu na hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro.
Zinazohusiana:
- Saadani: Mahali unapoweza kuwaona simba, twiga wakila upepo wa ‘beach’
- Waziri Kigwangalla awapa kibali wananchi kujenga shule ndani ya hifadhi ya Ngorongoro
- Mgogoro uhifadhi Ngorongoro bado ngoma mbichi
Aidha, Majaliwa amesema Serikali imepokea kauli ya wakazi wa Ngorongoro kwamba wako tayari kupokea maelekezo ya Serikali na kushirikiana pamoja katika kuulinda utalii na uhifadhi wa eneo hilo.
Amesema, kama ambavyo Serikali imetoa nafasi ya kusikiliza maoni ya wananchi wa tarafa hiyo, nao hawana budi kuipa nafasi Serikali kuendelea na mpango wa maboresho wa maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa uhakiki ili ije na mpango bora wa kuliendeleza eneo hilo.
Amesema atapitia changamoto alizokabidhiwa na Diwani wa Naiseko, James Moringe na akawataka wakazi hao waendelee kuiamini Serikali yao kwa sababu ina nia njema na wananchi wake.
“Endeleeni kuiamini Serikali yenu kwani ina njema na nyie. Tunahitaji kuona shughuli za ufugaji zikiendelea na utalii ukiendelea. Na kwa maana hiyo, mnakubaliana na Watanzania wanaotaka kuona utalii ukiendelea. Na kwa maana hiyo tufuate misingi ya uhifadhi.
“Na mnapotoka hapa, kila mmoja wetu akatafakari kuhusu changamoto ya kuongezeka kwa mifugo na idadi ya watu. Muwe watulivu wakati Serikali ikifanyia kazi maoni yenu. Tutapokea pia maoni ya taasisi na asasi za kiraia, nazo pia tutazifanyia kazi,” amesisitiza.
Amesema Serikali itaratibu maoni yanayotolewa na pande zote kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Waziri Mkuu amesema muendelezo wa vikao anavyofanya katika Wilaya ya Ngorongoro ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka viongozi wakutane na wakazi hao na kuwasikiliza maoni yao.