Mgogoro uhifadhi Ngorongoro bado ngoma mbichi
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Februari 14, 2022 wakati akizungumza na wadau wa uhifadhi kwenye kikao kilichofanyika Wasso-Loliondo ambapo amesema Serikali imepokea maoni waliyoyatoa, yatayojumuishwa na kuyawasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Serikali yazungumza na wafugaji kutafuta suluhu.
- Baadhi ya wapinga wafugaji kuondolewa eneo hilo.
- Ongezeko la watu ladaiwa kuhatarisha utalii wa hifadhi hiyo.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaangalia utaratibu kutafuta suluhu ya kudumu ya suala la uhifadhi katika eneo la Loliondo lililopo kwenye Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha.
Kauli hiyo ya Serikali imekuja wakati kukiwa na maoni tofauti kuhusu mgogoro wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambapo baadhi ya watu wameshauri Serikali iwaondoe wafugaji wa kijamii ya kimasai ambao idadi yao imekuwa ikizidi kuongezeka siku hadi siku na kutishia uhifadhi wa wanyama katika eneo hilo.
Hata hivyo, wengine wanadai kufanya hivyo itakuwa kinyume na haki za binadamu kwa sababu wafugaji hao wamekaa kwa muda mrefu katika eneo hilo ambalo ni sehemu muhimu kuendeleza maisha yao.
Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Februari 14, 2022 wakati akizungumza na wadau wa uhifadhi kwenye kikao kilichofanyika Wasso-Loliondo ambapo amesema Serikali imepokea maoni waliyoyatoa, yatayojumuishwa na kuyawasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Katika mjadala wetu wa leo, mmetoa maoni nasi tumeyapokea. Bado Serikali inayaangalia maslahi mapana ya umma. Tutawashirikisha pia ni lipi lina maslahi mapana kwa Watanzania,” amesema Majaliwa.
Kiongozi huyo mkuu wa shughuli za Serikali amesema kuwa idadi ya watu na mifugo imeongezeka ndani ya hifadhi ambapo wasipotafuta suluhisho la kudumu hifadhi hiyo itaathirika na shughuli za kibinadamu.
“Sisi sote tunatambua eneo hili ni la utalii, lazima tufike mahali tuamue kama tunataka utalii au la,” amesema.
Zinazohusiana:
- Saadani: Mahali unapoweza kuwaona simba, twiga wakila upepo wa ‘beach’
- Waziri Kigwangalla awapa kibali wananchi kujenga shule ndani ya hifadhi ya Ngorongoro
- Twiga hatarini kutoweka duniani
Aidha, Majaliwa amesema alichoenda kufanya leo ni utekelezaji wa ushauri uliotolewa na wabunge kwa Serikali kupitia Mwenyekiti wa Kamati wa Maliasili na Utalii iliyoielekeza Serikali iende katika maeneo ya Loliondo, Ngorongoro na Sale na kuzungumza na wananchi.
“Kama ambavyo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza lazima tuimarishe utalii na kuhakikisha wananchi wanashirikishwa, waheshimiwa Wabunge ambao ndiyo wawakilishi wametoa maoni yao ikiwemo kushauri suala la ushirikishwaji na ndio maana leo nimekuja hapa kuwasikiliza,”
Katika kikao hicho, wananchi wa makundi mbalimbali walipewa nafasi kutoa maoni yao wakiwemo mbunge, madiwani, malaigwanan, wanamije (batemi) na wenyeviti wa vijiji.
Katika maoni yao, wengi wao wamesema wako tayari kushirikiana na Serikali kuendelea kutunza rasilimali za Taifa.
Waliomba wapatiwe elimu ya uzazi wa mpango, wapimiwe ardhi za vijiji ili kupunguza migogoro inayojitokeza mara kwa mara katika Wilaya ya Ngorongoro yenye tarafa tatu za Loliondo, Sale na Ngorongoro.
Latest