Mwanamke mmoja kati ya 10 hujifungulia nyumbani Tanzania

January 19, 2023 12:29 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ripoti mpya yasema asilimia 14.9 ya wanawake wanajifungulia nyumbani.
  • Wanawake wa vijijini wanaongoza kujifungulia nyumbani kwa asilimia 18.8.
  • Upungufu wa huduma za afya hasa za uzazi wachangia. 

Dar es Salaam. Licha ya Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya, mwanamke mmoja katika ya 10 hujifungulia nyumbani nchini Tanzania, jambo linawaweka katika hatari ya kupata matatizo ya kiafya wao na watoto wao ikiwemo vifo vya mapema. 

Ripoti ya Utafiti wa Kufuatilia Hali ya Kaya Tanzania (NPS) ya mwaka 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni imeeleza kuwa asilimia 14.9 ya wanawake nchini Tanzania walijifungua watoto wao wakiwa nyumbani mwaka juzi.

Idadi kubwa ya wanawake wanaojifungulia majumbani ni wale wanaoishi vijijini ambako huduma za afya ikiwemo zahanati ziko mbali na maeneo wanayoishi au hazipo kabisa. 

Baadhi ya wanawake vijijini hutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo za uzazi na wengine hujifungulia njiani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoandaliwa na NBS kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), asilimia 18.8 (takriban wanawake wawili kati ya 10) wanaoishi vijijini hujifungulia nyumbani. 

Hali ni tofauti na mjini ambako ni asilimia 3.3 tu ya wanawake wanajifungulia nyumbani kutokana na upatikanaji wa uhakika wa huduma za afya ya uzazi ikiwemo kliniki za mama na mtoto.

Mathalan, katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, ni asilimia 1.1 ya wajawazito ndiyo hujifungulia nyumbani huku Zanzibar ikiwa ni asilimia 17.3 ikiwa juu kidogo ya wastani wa kitaifa wa asilimia 14.9.

Kwa Zanzibar, hiyo ni sawa na kusema takriban wanawake wawili kati ya 10 hujifungulia nyumbani.

Ripoti hiyo iliyozinduliwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba Januari 17, 2023, imeeleza kuwa wanawake wanne kati ya 10  walifujingua nyumbani mwaka 2020/21 huku waliojifungulia zahanati wakiwa asilimia 20.7. 

Hivi karibuni, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema matatizo mengi yanayosababisha vifo kwa wajawazito na watoto yanaweza kupungua kwa zaidi ya asilimia 80 kama mjamzito atahudhuria kliniki ya mama na mtoto kwa kipindi chote cha ujauzito wake na wakati ukifika akajifungulie katika vituo vya afya au hospitali.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila siku wanawake 830 hufariki duniani kutokana na matatizo wakati wa kujifungua na asilimia 99 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zinazoendelea.


Soma zaidi,


Athari za kujifungulia nyumbani

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti ya masuala ya afya (Tanzania Demographic Heath Survey mwaka 2015-2016 (TDHS)), zinaonyesha kila siku wanawake 30 hufariki dunia Tanzania kutokana na matatizo ya uzazi.

Matatizo hayo ya uzazi ni pamoja na kujifungulia nyumbani, huduma duni, umbali wa vituo vya afya na maeneo watokayo wajawazito hasa maeneo ya pembezoni.

Pia uhaba wa wakunga na wajawazito kwenda kujifungulia kwa wakunga wa jadi wasio na utaalamu na uhaba wa vifaa tiba katika vituo vya afya. 

Kwa mujibu wa shirika la Sema Tanzania linalohusika na afya ya uzazi, athari za kujifungua nyumbani husababisha matokeo mabaya ya watoto wachanga na wajawazito kama vile hatari ya kuambukizwa, kutokwa na damu baada ya kuzaa, na maambukizi ya VVU/Ukimwi kwa jamaa au wakunga wa jadi ambao hutoa huduma ya ukunga bila vifaa vya kinga. 

Changamoto kwa wajawazito kuendelea kujifungua majumbani inaweza kuzuilika iwapo hatua zinazofaa kwa wakati zitatumika. Wajawazito wanapaswa kukubali kuwa hospitali au vituo vya afya vilivyoidhinishwa ndiyo sehemu salama zaidi ya kujifungua.

Pia Serikali na wadau kuwekeza nguvu ya kusogeza huduma za afya ya uzazi hasa vituo vya afya hasa katika maeneo ya vijijini ambako tatizo ni kubwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW