Miili ya mashabiki wawili wa Yanga yaopolewa Mwanza
- Ni kati ya watu watano ambao waliopotea Agosti 5 baada ya mtumbwi wao kuzama maji ndani ya Ziwa Victoria.
Mwanza. Miili ya watu wawili kati ya watano waliopotea baada ya mtumbwi waliokuwa wanasafiria kuzama majini ndani ya Ziwa Victoria imepatikana leo hii na vikosi vya uokoaji huku jitihada zikiendelea kuwasaka waliosalia.
Kuonekana kwa miili hiyo kunafanya idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na ajali hiyo iliyotokea usiku wa Agosti 5 mwaka huu kufikia watatu baada ya mwili mmoja kuonekana muda mfupi baada ya tukio hilo lililohusisha mashabiki 23 wa timu ya soka ya Yanga.
Watu 17 wengine walinusurika katika ajali hiyo ambayo polisi wanaendelea kuchunguza chanzo cha ajali licha kueleza kuwa huenda ilitokana na mtumbwi wao kugonga mwamba.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa ameeleza katika taarifa kwa vyombo vya habari leo Agosti 7 kuwa miili hiyo imeopolewa majira ya saa11 alfajiri katika eneo la Butala Mawe Mawili katika kisiwa cha Yozu.
Miili hiyo imepatikana baada ya jitahada zilizofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi wa wilaya ya Sengerema.
Mutafungwa amewataja marehemu hao kuwa ni Mashauri Ishabakaki (42) mkazi wa Mbugani na Jonathan Mutasyoba (50) mkazi wa Kanyara waliozama maji usiku wa Agosti 5, 2024 wakati wakisafiri kutoka kisiwa cha Yozu kuelekea kitongoji cha Itabagumba kata ya Burihaeke.
Watu walikuwa wakitoka katika sherehe za kuadhimisha kilele cha Wiki ya Mwananchi ya Yanga zilizofanyika mwishoni mwa juma.
“Jitihada za kutafuta watu wengine watatu zinaendelea ambao ni Masaka Angote ( 60), mkazi wa Burihaeke, Edward Kachelemi, (46), mkazi wa Burihaeke na Shija Paschal(30) mkazi wa Yozu ambao bado hawajapatikana,” amesema Mutafungwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa miili ya marehemu waliopatikana imekabidhiwa kwa ndugu kuendelea na taratibu za mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.