Mauaji ya kutisha yatikisa Mwanza kwa miezi miwili
- Watu watano wauwawa kwa nyakati tofauti.
- Mauaji hayo yanahusishwa na wivu wa kimapenzi, ushirikina na tamaa ya pesa.
- Serikali yaahidi kuyakomesha na kuimarisha usalama wa raia.
Mwanza. Kifo cha utata cha Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, Boniphace Kwangu kimekuwa sehemu ya matukio ya mauaji ya kutisha yaliyotokea ndani ya miezi miwili katika Mkoa wa Mwanza na kuacha maswali mengi yasiyo na majibu kwa wananchi juu ya usalama wao.
Askofu Kwangu (61) alikutwa amekufa na mwili wake ukielea juu ya maji katika Ziwa Victoria karibu na linapojengwa daraja la Kigongo-Busisi maarufu kama JPM.
Taarifa ya Jeshi la Polisi kwa waandishi wa habari iliyotolewa Disemba 2, 2022 inasema kuwa Askofu Kwangu aliondoka nyumbani kwake Mtaa wa Shibula wilayani Ilemela Novemba 28 majira ya asubuhi na kuelekea wilayani Sengerema kwa ajili ya kupokea malipo ya mwisho ya Sh2.5 milioni baada ya kuuza eneo lake pamoja na nyumba.
“Kwa mujibu wa maelezo ya familia, Asofu Kwangu alikuwa ameuza shamba lake hilo kwa kanisa la KKKT-Sengerema.
“Hata hivyo hakuweza kulipwa kiasi hicho cha fedha kwa kuwa wanunuzi walimtaka awasilishe nyaraka ya umiliki wa eneo hilo hivyo alirudi mjini kwa ajili ya kushughulikia nyaraka hizo,” amesema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa katika taarifa hiyo.
Amesema ilipofika jioni ya siku hiyo hakurudi nyumbani, hivyo familia ikawa na wasiwasi kuhusu alipo Askofu huyo ndipo wakaamua kutoa taarifa kituo cha polisi kwa ajili ya uchunguzi.
Disemba Mosi majira ya saa 10:00 jioni zilipatikana taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna mwili unaelea ndani ya maji karibu na kunapojengwa daraja la JPM Kijiji cha Kigongo wilayani Misungwi.
Kamanda Mtafungwa amesema baada ya askari kwa kushirikiana na wananchi kuopoa mwili huo ulitambulika kuwa ni wa Boniphace Kwangu.
Mwili huo umehifadhiwa hospitalini huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo ambapo wanawaomba wananchi kutoa ushirikiano ili ziweze kufanyiwa kazi.
Askofu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza, Boniphace Kwangu, Boniphace Kwangu amekutwa amekufa na mwili wake ukielea kando ya Ziwa Victoria karibu na kunapojengwa daraja la JPM. Picha | Mariam John.
Mwanza yatikiswa na mauaji
Kifo cha Askofu Kwangu ni mfululizo wa mauaji yaliyotokea mkoani Mwanza ndani ya miezi miwili huku yakiacha maswali mengi kwa wananchi juu ya hatma ya maisha yao ikizingatiwa kuwa yanahusisha watu muhimu kwenye jamii.
Taarifa za kifo hicho zimekuja wakati Jeshi la polisi linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kumuua Hamida Mussa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) tawi la Mwanza. Tukio hilo lilitokea Novemba 28 mwaka huu katika Mtaa wa Buzuruga wilayani Ilemela.
Marehemu Hamida aliuawa kwa kunyongwa shingoni na mtandio akiwa nyumbani kwake na linadaiwa kutekelezwa na binti wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Sara Mwendesha (15).
Matukio mengine ni pamoja na lile lililotokea Octoba 7 mwaka huu katika Kijiji cha Nyashoshi kata ya Buhumbi wilayani Magu ambapo Jesto Lukas (34) alimuua baba yake mzazi pamoja na mke wake kwa kuwakata mapanga kisha na yeye kujinyonga kwa shuka huku chanzo kikitwaja kuwa ni wivu wa mapenzi.
Novemba 4 mwaka huu katika Kijiji cha Ngulla wilayani Kwimba, Joseph Msongoma (49) ambaye ana ulemavu wa ngozi (ualbino) aliuawa kwa kukatwa na panga katika mkono wa kulia.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shivyawata), Alfred Kapole alilihusisha tukio hilo na imani za kishirikina baada ya aliyetekeleza mauaji hayo kuondoka na mkono wa marehemu.
Mbali na tukio hilo, mkazi mwingine wa Kijiji cha Mahaha wilayani Magu mkoani Mwanza, Zawadi Msagaja (20) anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumzika mtoto wake wa miezi miwili akiwa hai ili apate mali.
Zawadi kwa kushirikiana na dada yake Elizabeth Kaswa pamoja na shemeji yake ambaye ni mgaga wa kienyeji Mussa Mazuri walimzika mtoto huyo huku wakimpa kitisho mama wa mtoto asipofanya hivyo yeye atauawa.
Soma zaidi:
-
Mauaji ya mwanaharakati wa ujangili: 11 wahukumiwa kunyongwa hadi kufa
-
Watatu washikiliwa na polisi mauaji ya mhadhiri SAUT
Viongozi wa dini wananchi wanasemaje?
Sophia Masanza ni mjasirimali katika soko la Buhongwa jijini Mwanza anasema kwa sasa hofu imeanza kutanda kwa kuwa watu wanajichukulia sheria mkononi, wengi watakuwa wanaogopa kutoka kazini usiku wakihofia kutekwa na kuuawa.
“Kwa kweli tunahofu sana hasa kila siku tunapofungua mitandao ya kijamii na kukutana na vifo vya kuuliwa, ni huzuni hadi tunahofia kufanya kazi usiku,” amesema Masanza.
Akizungumza na Nukta habari (www.nukta.co.tz), Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Shekh Hassan Kabeke amesema sababu kubwa ya matukio hayo ni ukosefu wa maadili na ubovu wa malezi kutoka chini.
Shekh Kabeke amesema viongozi wa dini na jamii kwa ujumla wanao wajibu wa kuhakikisha wanarudisha maadili kwenye mstari.
“Mimi nasema ipo sehemu kama jamii tumelegalega katika kuhimiza malezi bora na tukifanikiwa kurejesha huko tutakuwa na jamii bora na hakutakuwa na matukio ya kikatili kama haya,” amesema Shekh Kabeke.
Ameiomba Serikali na mahakama kutenda haki pale mtuhumiwa anapobainika kuhusika moja kwa moja kwenye matukio hayo ili kuondoa dhuruma zinazoweza kutokea iwapo kutakuwa na ubabaishaji kwenye maamuzi ya kesi.
“Changamoto nyingine ni kwenye suala la maamuzi pale watendaji wanapopindisha ukweli ndipo dhuruma inapoingia, na hayo yote yanachangiwa na kuwa na malezi mabovu kutoka chini,” amesema Shekh Kabeke.
Hata hivyo, amesema viongozi wa dini wataendelea kukemea matukio hayo kwa kuwa hayakubaliki kwenye jamii na yanatakiwa kulaaniwa na kila mtu.
“Maandiko katika Uislam yanatueleza kuwa mtu yeyote anayeua nafsi ya mtu mmoja anafananishwa na kuua nafsi za maelfu ya watu, na yeyote anayetenda haki kwa mtu mmoja naye anafanyanishwa kuwatendea haki maelfu ya watu hivyo tuzidi katika kutenda haki na kuchukia uovu,” amesema.
Tangazo

Mikakati ya Jeshi la Polisi kukomesha matukio hayo
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mtafungwa amesema moja ya mikakati ya jeshi hilo mkoani Mwanza ni kuhakikisha linadumisha amani na kukomesha matukio ya uhalifu yakiwemo mauaji ya watu kujichukulia hatua mkononi.
Amesema hivi sasa wameanzisha doria kila eneo kuhakikisha wanakomesha vitendo vya kihalifu si mauaji peke yake lakini pia vitendo vya kihalifu kama wizi, ubakaji na hata uporaji wa mali ambavyo pia vinashamiri jijini Mwanza.
Amesema katika matukio ya hivi karibuni mengi yanasababishwa na wivu wa mapenzi, visasi pamoja na kutaka utajiri kwa njia za kishirikina jambo ambalo siyo sahihi kwa kuwa mali zinapatikana kwa kufanya kazi kwa bidii.
“Nitoe wito kwa wananchi kuacha imani potofu za kishirikina ambazo zimekua zikipoteza maisha ya watu na wengine kuingia kwenye matatizo ya vifungo vya maisha jela, vilevile ninawasisitiza kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume na sheria,” amesisitiza Kanda Mtafungwa.