Waokoaji waendelea kuwasaka watano waliozama maji Mwanza
- Manusura wa ajali hiyo waeleza kuwa maji yalijaa ndani ya mtumbwi baada ya kukosa kifaa cha kuyapunguza, kisha kuzamisha kifaa hicho.
Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linaendelea kuwatafuta watu watano waliopotea baada ya mtumbwi waliokuwa wanasafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria usiku wa kuamkia Agosti 5 mwaka huu wakati wakitoka kwenye sherehe za Wiki ya Mwananchi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilibroad Mutafungwa, amesema watu hao watano ni sehemu ya watu 23 walikuwa wakitoka kusherehekea maadhimisho ya kilele cha wiki ya timu ya mpira wa miguu ya Yanga maarufu kama Wiki ya Mwananchi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mutafungwa amesema ajali hiyo iliua mtu mmoja huku wengine 17 wakinusurika baada ya wavuvi waliokuwa karibu na eneo hilo kuwaokoa mapema baada ya tukio hilo.
“Watu hao walikuwa wanasafiri kutoka kisiwa cha Yozu kuelekea Kijiji cha Itabagumba kilichopo kata ya Bulyaheke wilayani Sengerema ndipo mtumbwi huo ulipoanza kuingia maji na kuanza kuzama,” amesema Mutafungwa.
Hadi sasa bado hawajapata undani wa chanzo cha ajali hiyo, ila amesema taarifa za awali zimebaini huenda ilichangiwa na mtumbwi huo kugonga mwamba.
Hata Hivyo, Kamanda Mutafungwa amesema jeshi la polisi kwa kushirikiana na wananchi, wavuvi na timu ya uokoaji inaendelea na zoezi la uokoaji wa watu hao watano.
Ajali za boti na mitumbwi hutokea mara kwa mara ndani ya Ziwa Victoria na kusababisha majeruhi na vifo kwa wakazi wanaotumia vyombo vya usafiri katika eneo kutokana na kutofuata kikamilifu taratibu za usalama majini.
Julai mwaka jana watu 13 wengi wao wakiwa ni watoto walifariki dunia baada ya mitumbwi miwili kuzama maji wilayani Bunda mkoani Mara.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na wakazi wa kisiwa cha Yozu kilichopo wilaya ya Sengerema wakati alipofika kwa ajili ya kuendelea na operesheni ya kuwatafuta watu watano ambao wamezama kwenye mtumbwi ndani ya Ziwa Victoria. Picha| Mariamu John/ Nukta.
Wakosa kifaa cha kupunguzia maji
Baadhi ya manusura wa ajali hiyo wameeleza kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya mtumbwi waliokuwa wanasafiria kuanza kuingia maji na kushindwa kuyatoa kutokana na kukosa chombo cha kuyachotea.
“Baada ya mtu kuanza kujaa maji mmoja kati yetu alitoka kwenda kuita wavuvi ili waje watuokoe na baada ya wavuvi hao kufika tayari wenzetu watano walikuwa hawaonekani na mmoja alikuwa amekufa,” amesema Dotto Ng’ongolo.
Majeruhi mwingine, Prisca Mafuru amesema walikuwa wamealikwa kwenda kushiriki sherehe hizo za kilele cha Wiki ya Mwananchi. ajali hiyo njiani wakati wanarudi kutoka katika sherehe zao na isingekuwa uokoaji wa haraka wa wavuvi wa jirani wengi wangepoteza maisha.
Ili kutokomeza ajali hizo siku zijazo, jeshi la polisi limeanza kutoa elimu ya usalama wa usafiri wa majini kwa kuwaelimisha wakazi katika kisiwa hicho kuhakikisha mitumbwi wanayotumia kusafiria kuwa na vifaa vya uokozi likiwemo boya la kujiokoa.
“Tumeagiza mitumbwi yote ikaguliwe na iwe na vifaa maalum vya kusaidia uokozi hali itakayosaidia iwapo changamoto yoyote itakayojitokeza,” amesema Mutafungwa.
Latest



