Miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara katika namba
Rais Samia Suluhu Hassan leo Desemba 8, 2021 amelihutubia Taifa ikiwa zimebaki saa chache kwa Watanzania kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) baada ya kukombolewa kutoka kwa mkoloni Muingereza. Picha| Ikulu.
- Rais Samia ataja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana.
- Ataka amani, utulivu na mshikamano vudumishwe.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania wanatakiwa kujivunia miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo afya huku akiwataka kuongeza kasi ya kukuza uchumi na kujiletea maendeleo.
Rais Samia amelihutubia Taifa ikiwa zimebaki saa chache kwa Watanzania kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) baada ya kukombolewa kutoka kwa mkoloni Muingereza.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi katika hotuba yake ametaja mambo sita makuu ambayo Tanzania Bara imeyapata tangu ilipopata uhuru Desemba 6, 1961 ikiwemo kujenga mshikamano wa kitaifa na kuimarisha uchumi na kupunguza umaskini.
Pia mafanikio mengine ni kuongeza upatikanaji na kuboresha huduma za jamii, kujenga heshima ya nchi na ushawishi wa kikanda na kimataifa na kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria.
Katika hotuba hiyo iliyokuwa ikirushwa mubashara katika vyombo vya habari, Rais ametaja baadhi takwimu ambazo zinaonyesha mabadiliko makubwa yaliyotokea miaka 60 iliyopita.
“Wastani wa pato kwa mtu kwa mwaka 1961 lilikuwa Sh776 na mwaka jana 2020 ni Sh2.6 milioni. Jambo hili linaongeza hadhi yetu machoni mwa jumuiya za kimataifa na kutuondolea unyonge na unyanyapaa,” amesema Rais Samia.
Amesema wakati tunapata uhuru, wakoloni walituachia kilomita za lami zisozidi 1,360 na sasa mtandao wa barabara za lami zimefikia 11,186 na kazi inaendelea ya kujenga nyingine hasa maeneo ya vijini ili kuwawezesha wakulima kuinuka kiuchumi.
Sambamba na hilo ni kuboresha kwa huduma za usafiri wa majini ambapo kabla ya uhuru kulikuwa na meli sita na kwa sasa kuna meli 14 zinazofanya kazi katika maziwa ya Nyasa, Tanganyika na Victoria.
“Kabla ya uhuru, nchi yetu ilikuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 17.5 tu za umeme. Leo hii tunazalisha megawati 1,909 na tunaratajia kuongeza megawati 2,115 tutakapokamilisha bwawa la Nyerere,” amesema Rais.
Zinazohusiana:
-
Rais Magufuli afuta sherehe za Uhuru kwa mara ya tatu
-
Rais Magufuli afuta sherehe za uhuru kwa mara ya pili
Katika hotuba hiyo pia ameeleza kuwa Tanzania Bara imefakiwa kuongeza upatikanaji wa maji kutoka asilimia 25 ya mwaka 1961 hadi kufikia asilimia 72.3 vijijini na asilimia 86 mijini mwaka 2020.
Aidha, mageuzi makubwa yamefanyika katika sekta ya afya ambapo miaka ya nyuma daktari mmoja alikuwa anahudumia watu 25,000 lakini mpaka miaka 10 baadaye daktari mmoja anahudumia watu 20,000.
“Tunaendelea kuboresha sekta hii kwa kuhakikisha tunaajiri madaktari ili tuweze kufikia viwango vya Shirika la Afya Duniani vinavyopendekezwa kwa uwiano wa daktari 1 kuhudumia watu 3,000,” ameahidi Rais na kuongeza kuwa,
“Mwaka wa kilimo 1986/78 uzalishaji (wa mazao ya chakula kitaifa) ulikuwa tani milioni 6.8 ukilinganisha na tani milioni 18.4 kwa mwaka wa kilimo 2020/21.”
Kwa sasa Watanzania wanaishi kwa muda mrefu ikilinganishwa na zamani, hivyo kuchangia nguvukazi inayohitajika katika ukuaji wa uchumi ambapo wakati nchi inapata uhuru, umri wa kuishi wa Mtanzania ulikuwa ni miaka 37 na sasa ni wastani wa miaka 67.
“Wakati tunapata uhuru, nchi yetu ilikuwa na wabunge 80, ikilinganishwa na nafasi za wabunge kwa sasa ambao ni 393 lakini waliopo 391 ambao kati ya hao wanawake 147 sawa na asilimia 37,” amesema Rais Samia.
Licha ya mafanikio hayo, amewataka Watanzania kudumisha amani,umoja, mshikamano na muungano na kuendelea bila kusita kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na kufanya mageuzi ya kiuchumi kila inapolazimu kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia.
Aidha, Wametakiwa kutunza mazingira na kuyalinda kwa wivu mkubwa ili kulithisha vizazi vijavyo.
Latest